Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kila mwisho wa wiki familia nyingi zilipenda kutembelea ufukwe wa ziwa. Watoto walicheza kwenye mchanga wengine walifurahia kuona samaki huku wafanyabiashara wadogo wakipata wateja wengi.
Hata hivyo hali ilianza kubadilika baada ya baadhi ya watu kuanza kutupa chupa, mifuko ya plastiki na mabaki ya vyakula ufukweni. Harufu mbaya ilianza kusambaa na sehemu iliyokuwa ikivutia wageni ikawa chafu.
Mtoto mmoja aliyekuwa akimsaidia baba yake kuuza juisi karibu na ufukwe aligundua kuwa wateja walikuwa wakipungua. Alijiuliza kwa nini watu walikuwa wameacha kutembelea eneo hilo.
Alimweleza baba yake kuwa uchafu uliokuwa ufukweni ulikuwa ukiharibu mandhari na kuwafukuza wageni. Baba yake alipendekeza washirikishe wafanyabiashara wengine katika kutafuta suluhisho.
Walianzisha zoezi la usafi kila Jumamosi na kuweka mapipa ya taka katika maeneo mbalimbali. Pia waliweka mabango yenye ujumbe wa kuhamasisha utunzaji wa ufukwe.
Baada ya muda wageni walianza kurejea na shughuli za biashara zikachangamka tena.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment