IJUE FAIDA YA MACHUNGWA KWA WATOTO

Emakulata Msafiri

Mchungwa ni mojawapo ya matunda yenye thamani kubwa kiafya, hasa kwa watoto wadogo. Tunda hili lina ladha tamu na harufu nzuri na linapendwa na watu wa rika mbalimbali. Kwa watoto wadogo mchungwa si tu tunda la kufurahisha bali pia ni chanzo kikubwa cha virutubisho muhimu kwa afya na maendeleo yao ya mwili na akili.

Kwanza kabisa ,mchungwa una kiasi kikubwa cha vitamini C. Vitamini hii ni muhimu kwa kuongeza kinga ya mwili wa mtoto. Watoto wadogo huwa na kinga dhaifu kwa hivyo wanahitaji virutubisho vitakavyowasaidia kupambana na maradhi kama vile mafua homa na kikohozi. Kwa kuwapa watoto mchungwa mara kwa mara wazazi huwasaidia kulinda afya zao dhidi ya magonjwa ya mara kwa mara.

Pili, mchungwa una nyuzi lishe ambazo husaidia katika mmeng’enyo wa chakula. Watoto wengi hukumbwa na matatizo ya tumbo kama vile kufunga choo au tumbo kujaa gesi. Kwa kula mchungwa au kunywa juisi yake watoto hupata nafuu katika mmeng’enyo wa chakula na kuwa na choo laini, jambo ambalo ni muhimu kwa afya ya mtoto.



Faida nyingine kubwa ni mchango wa mchungwa katika ukuaji wa mifupa na meno. Mchungwa una madini kama kalsiamu na fosforasi ambayo huchangia sana katika ukuaji wa mifupa imara na meno mazuri. Katika kipindi cha ukuaji, mtoto huhitaji virutubisho vya kutosha ili kuimarisha mifupa yake, na mchungwa hutoa msaada mkubwa katika hilo.

Pia, mchungwa husaidia kuimarisha ngozi ya mtoto. Watoto wenye upungufu wa vitamini C mara nyingi huonekana kuwa na ngozi isiyo na afya. Kwa kuwapa watoto mchungwa, ngozi yao hubaki laini yenye unyevunyevu wa asili na yenye afya bora. Hii ni muhimu hasa kwa watoto wanaoishi kwenye maeneo yenye hali ya hewa kavu.

Zaidi ya hayo, mchungwa ni chanzo kizuri cha maji asilia. Kwa sababu mchungwa una maji mengi humsaidia mtoto kuwa na kiwango cha kutosha cha maji mwilini. Hii ni muhimu hasa katika hali ya joto au mtoto anapokuwa mgonjwa. Kunywa juisi ya mchungwa kunaweza kusaidia kuzuia upungufu wa maji mwilini (dehydration).



emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments