ADELADIUS MAKWEGA
Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma
Nyaraka unayoiona hapo juu inaonesha barua iliyoandikwa na afisa wa Serikali kutoka ngazi ya chini, yaani Kata ya Mvumi, mkoani Dodoma, akimweleza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma kuhusu mlipuko wa ugonjwa wa NDUI katika eneo la Mvumi, Novemba 9, 1961.
Hii ni miongoni mwa nyaraka zilizohifadhiwa na Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa kwa zaidi ya miaka 65 sasa.
Nyaraka hii inaeleza pia namna viongozi wa ngazi za chini walivyokuwa wakiwasiliana na viongozi wa ngazi za juu mara baada ya kutokea kwa milipuko ya magonjwa hatari kama NDUI.
Aidha, nyaraka hii inatoa mwanga kuhusu namna Serikali ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa zilivyokuwa zikikabiliana na ugonjwa huo.
Ugonjwa wa NDUI ulitangazwa kutokomezwa duniani Desemba 9, 1979. Miezi mitano baadaye, yaani Mei 1980, Mkutano Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) ulitoa tamko rasmi la kuthibitisha kuwa ugonjwa huo ulikuwa umetokomezwa duniani.
Wataalamu wa afya wanaeleza kuwa:
“Kuna aina mbalimbali za magonjwa yanayofanana na ndui kwa binadamu na wanyama, wakiwemo nyani na kuku. Hata hivyo, ndui ya wanyama na ndege bado ipo.”
Ugonjwa wa NDUI una historia kubwa nchini Tanzania. Kwa Watanzania wengi, hasa waliozaliwa katika kipindi ambacho chanjo ya ndui ilitolewa, kuna alama inayojulikana kama kovu la chanjo katika sehemu ya juu ya mkono, karibu na bega. Alama hiyo ilitokana na mbinu ya utoaji wa chanjo iliyojulikana kama scarification.
Swali la msingi: Je, NDUI ya kuku na nyani inaweza kuwaambukiza binadamu?
Kwa mujibu wa maelezo ya kisayansi, ndui ya kuku haiambukizi binadamu, wakati virusi vya ndui ya nyani vinaweza kuambukiza binadamu. Hata hivyo, ugonjwa huo unafuatiliwa na kudhibitiwa kupitia mifumo ya afya ya umma.
Historia inaonesha kuwa ugonjwa wa NDUI ulikuwa miongoni mwa magonjwa yaliyosababisha vifo vingi katika historia ya binadamu.
Inakadiriwa kuwa ugonjwa huo ulisababisha vifo vya takribani watu milioni 300 katika karne ya 20 pekee. Inaaminika kuwa ugonjwa huo ulikuwepo tangu takribani miaka 10,000 kabla ya Kristo.
Ushahidi wa kihistoria unaohusishwa na ugonjwa huu pia ulionekana katika mwili wa Farao Ramses V wa Misri, aliyefariki mwaka 1157 kabla ya Kristo, ambaye mwili wake ulikuwa na alama zinazofanana na vipele vya ugonjwa huo.
makwadeladius@gmail.com
-0717649257
.gif)



.gif)
Post a Comment