Adeladius Makwega
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Dodoma.
Novemba 2, 2026
Ilikuwa siku iliyoanza kwa namna ya kipekee kwa Mwanakwetu. Kama ilivyo kawaida yake, aliwasili kazini mapema sana. Hata hivyo, siku hiyo macho yake yalikutana na jambo lisilo la kawaida: gari jeupe lililokuwa limewabeba maafisa wa Serikali wapatao sita.
Kwa kuwatazama tu, Mwanakwetu alibaini kuwa hawa hawakuwa watumishi wa kawaida wa taasisi hiyo. Walikuwa wageni. Kwa bahati mbaya, walikuwa mbali kiasi kwamba haikuwezekana hata kuwapa salamu za asubuhi.
Mwanakwetu akaendelea na safari yake ya kuelekea ofisini, akijiandaa kukabiliana na majukumu ya siku, ambayo yalitanguliwa na vikao kadhaa. Kama ilivyo kawaida katika ofisi zetu, wakati mwingine vikao vinaweza kuwa vingi kiasi kwamba mtu akitoka kikaoni anahitaji kikao kingine ili kujadili kilichojadiliwa kwenye kikao cha kwanza!
Majira ya mchana, Mwanakwetu alikutana na watu wawili kati ya wale aliowaona asubuhi. Safari hii wakasalimiana na kupishana.
Lakini simulizi haikuishia hapo.
Majira ya saa 7:53 mchana, Mwanakwetu alikutana tena na maafisa hao wawili. Safari hii walikuwa jirani na dawati la Bi. Bujo Ngwale, Afisa Kumbukumbu.
Mbele yake alikuwepo kaka mmoja mrefu na dada mmoja mrefu, wote wakiwa wamependeza kiasi cha kumfanya Mwanakwetu kujiuliza kama walikuwa wamepangwa pamoja na hata mavazi yalikuwa yamefanana.
Walionekana kama mapacha wa kikazi. Kila mmoja alipokuwa, mwingine naye alikuwa jirani. Kwa kweli, ukimuona mmoja, mwingine hakuwa mbali.
Hapo ndipo mmoja wa wageni alipouliza:
“Samahani, Mwanakwetu ndiye nani?”
Bi. Ngwale akajibu kwa utulivu:
“Ni huyu hapa, huyu hapa mbele yenu.”
Mwanakwetu, bila kusubiri mahojiano yaendelee, akamgeukia kijana huyo na kumuuliza jina lake.
Kijana huyo akajitambulisha kuwa anaitwa Aniset Mark Kauky, Afisa Kumbukumbu Msaidizi katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Kanda ya Nyanda za Juu, ofisi iliyopo Mbeya.Mwanakwetu akampiga maswali kadhaa
Akafafanua:
“Nipo hapa tangu asubuhi. Tumetokea Mbeya nikiwa pamoja na wenzangu kadhaa katika kutekeleza majukumu yetu ya kikazi.”
Pembeni yake alikuwepo binti yule mrefu, ambaye naye alijitambulisha kwa jina la Juliana Maleko, Katibu wa Sheria kutoka Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Mbeya.
Mwanakwetu akapata jambo la kutafakari.
KURWA NA DOTO WA KIKAZI!
Mwanakwetu akasema moyoni:
“Wakili Mkuu wa Serikali amekuwa Kurwa, na Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imekuwa Doto? Maana tangu asubuhi nimekuwa nikiwaona hawa wawili pamoja. Mmoja mbele, mwingine nyuma; mmoja akisimama, mwingine yupo jirani. Kila unapomwona Bi. Maleko, ndugu Kauky naye yupo hapo hapo!”
Hapa Mwanakwetu hakuwa na lingine, bali alivutiwa na mshikamano wao wa kikazi na namna walivyoonekana kushirikiana.
Kwa kweli, ilikuwa picha nzuri ya watumishi wa umma wanaoweza kusafiri pamoja, kutekeleza majukumu pamoja na kuendeleza mawasiliano mazuri kazini.
Mwanakwetu akawauliza kuhusu safari yao kutoka Mbeya hadi Dodoma.
Ndugu Kauky akamweleza:
“Katika safari yetu tulikuwa na watumishi kadhaa wa umma. Tumesafiri salama, tukiwa pamoja kwa takribani saa 12 kutoka Mbeya hadi Dodoma. Wenzetu wengine walitoka Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mbeya, Kamanda wa Polisi Mbeya na Afisa mmoja mwingine. Kwa ujumla, safari yetu ilikuwa nzuri sana.”
Mwanakwetu akafurahi kusikia kuwa safari ilikuwa salama. Lakini kama mwandishi mwenye udadisi wa kutaka kujua hata yale yaliyobaki nyuma ya pazia, hakuishia hapo.
Mwanakwetu akauliza:
“Hebu niambieni, hali ya hewa ya Mbeya na Dodoma kwa sasa inalingana?”
Wakajibu:
“Hapana. Dodoma kuna joto kali sana, wakati Mbeya hali ya hewa imechanganyika. Kuna joto na baridi.”
Mwanakwetu akatabasamu moyoni.
Aha! Safari hii haikuwa tu ya kutoka Mbeya kwenda Dodoma, bali ilikuwa safari kutoka kwenye hali ya hewa ya joto na baridi kwenda kwenye joto kali.
Lakini bado alikuwa na swali moja muhimu zaidi.
Baada ya kusafiri kwa takribani saa 12, je, maafisa hawa walikuwa wakizungumza nini njiani? Je, walikuwa wakijadili maendeleo ya nchi, masuala ya kiutendaji, kumbukumbu za Serikali au walikuwa wanapanga namna ya kuikabili Dodoma yenye joto kali?
Mwanakwetu akauliza:
Maafisa hao wakajibu kuwa mazungumzo yao yaligusia masuala mbalimbali ya kijamii, hususan ndoa na changamoto zake katika maisha ya sasa.
Mmoja wao akaeleza:
“Unajua, kwa sasa maisha ya ndoa yana changamoto nyingi. Zamani wazazi wetu waliishi katika mazingira tofauti. Ilikuwa jambo la kawaida kwa mwanaume kumuoa mwanamke ambaye hafanyi kazi, huku yeye akigharamia mahitaji yote ya familia. Mama alitumia muda mwingi kulea watoto na kusimamia familia, wakati baba akijikita katika kutafuta fedha za kuendesha maisha ya nyumbani.
“Lakini sasa mambo yamebadilika. Wakati mwingine baba anafanya kazi, mama naye anafanya kazi, na wote wanarudi nyumbani wakiwa wamechoka. Swali linakuwa: nani atashughulikia watoto? Nani atapika? Nani atasimamia malezi? Na nani atapumzika kwanza?”
Hapo ndipo changamoto za kisasa zinapoanza kuonekana.
Maafisa hao walieleza kuwa baadhi ya familia zinakabiliwa na changamoto ya kupata muda wa kutosha wa kulea watoto, huku kukiwa na mabadiliko ya matarajio ya vijana kuhusu maisha ya ndoa.
Waligusia pia tabia ya baadhi ya vijana kupendelea maisha mepesi bila kuzingatia wajibu na majukumu yanayoambatana na kujenga familia.
Mwanakwetu akatafakari.
Kweli, zamani baba akitoka kazini alikuta chakula kimeandaliwa, lakini sasa baba akitoka kazini anaweza kukuta mama naye ametoka kazini, watoto wanahitaji msaada wa masomo, vyombo vinasubiri kuoshwa na jikoni kuna maswali mengi kuliko majibu!
Na hapo ndipo ndoa ya kisasa inapohitaji zaidi ya upendo: inahitaji ushirikiano, mawasiliano, uvumilivu na kugawana majukumu.
Kwa maana nyingine, mapenzi pekee hayawezi kuosha vyombo, kufua nguo, kusaidia watoto kufanya kazi za shule na kulipa bili za umeme!
Hayo yote yanahitaji ushirikiano wa wahusika.
Baada ya mazungumzo hayo, Mwanakwetu aliwaaga ndugu Kauky na Bi. Maleko huku kila mmoja akiendelea na majukumu yake ya kikazi.
Naye Mwanakwetu akaondoka akiwa na jambo la kutafakari na hatimaye kuandika makala haya.
Msomaji wa Mwanakwetu, hebu tutafakari safari hii.
Hii ni safari ya watumishi wa umma kutoka Mbeya hadi Dodoma, safari ya takribani saa 12, iliyowaunganisha katika majukumu ya kikazi na kuwapa nafasi ya kujadili masuala muhimu ya kijamii.
Lakini Mwanakwetu amevutiwa zaidi na tofauti ya hali ya hewa ya miji hii miwili na namna inavyoweza kutumika kama mfano wa kuelezea mabadiliko ya maisha ya ndoa.
Mbeya yenye joto na baridi inaweza kufananishwa na ndoa za zamani, ambazo zilikuwa na mfumo tofauti wa kugawana majukumu katika familia.
Dodoma yenye joto kali inaweza kufananishwa na ndoa za sasa, ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi zinazohitaji ushirikiano mkubwa wa wanandoa.
Hata hivyo, tusikose kuelewana. Mwanakwetu hasemi kuwa ndoa za zamani hazikuwa na matatizo au kwamba ndoa za sasa haziwezi kuwa na furaha.
Anachosisitiza ni kwamba kila kizazi kina mazingira yake, changamoto zake na namna yake ya kuyakabili.
Zamani majukumu yalikuwa na mgawanyo uliozoeleka katika familia nyingi. Leo mazingira yamebadilika, hivyo wanandoa wanahitaji kujifunza kuishi kwa kushirikiana badala ya kutegemea mifumo ya zamani bila kuzingatia uhalisia wa sasa.
Kwa hiyo, kama Mbeya kuna joto na baridi, na Dodoma kuna joto kali, basi hata kwenye ndoa kuna vipindi vya utulivu na vipindi vya changamoto.
Muhimu si kukimbia joto, bali kujua namna ya kukabiliana nalo!
Na kama safari ya Mbeya hadi Dodoma inaweza kuchukua saa 12, basi safari ya ndoa nayo inahitaji subira, maelewano na ushirikiano. Huwezi kuendesha ndoa kwa kasi ya gari la mashindano huku ukitarajia kila kitu kiwe sawa!
Mwanakwetu upo? Kumbuka:
Kutoka Joto Baridi Hadi Joto Kali!
Nakutakia siku njema yenye baraka, mafanikio na tabasamu.
makwadeladius@gmail.com
-0717649257

Post a Comment