Adeladius Makwega-MBAGALA.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, aliwasili nchini Uingereza tarehe 7 Oktoba 2026 kwa ziara ya kikazi ya siku tano. Lengo ya Ziara hiyo ni kuimarisha fursa za biashara, kuvutia mitaji, na kuongeza uwekezaji kati ya Tanzania na Uingereza.
Mwanakwetu binafsi yake amekuwa anajiuliuza swali hili Je, Kwa mtanzania mwenye kipato cha chini, maana ya ziara hii ni nini ?
Kulijibu swali hili kupitia wadau kadhaa, vyanzo kadhaa na wataalamu kadhaa wa uchumi, majibu yalikuwa haya
Taarifa rasmi zinaonyesha kuwa Jukwaa la Uwekezaji Tanzania–Uingereza la tarehe 8 Oktoba 2026 linawaleta pamoja serikali, wawekezaji wa kimataifa na taasisi za fedha, likilenga maeneo kama madini, nishati, miundombinu, kilimo/uchakataji wa chakula na viwanda.
Kwa watu maskini wa Mbagala na kule Ilonga Mahenge, kwa akina Mwanakwetu, faida inaweza kuwa nini?Au viongozi wetu pamoja na timu yao wamekwenda Uingereza kutalii?
Majibu ya tija ya safari hii aliyoyaokota Mwanakwetu yalikuwa haya:
Mosi, Ajira zenye kipato bora
Hii ndiyo njia muhimu zaidi. Ikiwa kampuni za Uingereza zitawekeza katika
viwanda, kilimo cha kibiashara, nishati, usafirishaji au teknolojia, zinaweza
kuongeza ajira. Lakini si kila uwekezaji huleta ajira nyingi au zenye mishahara
mizuri. Benki ya Dunia imesisitiza kwamba changamoto Tanzania si ukosefu wa
ajira pekee, bali ukosefu wa ajira zenye kipato cha kutosha na tija.
Pili ni Masoko kwa wakulima na wafanyabiashara wadogo.
Uwekezaji katika kilimo na uchakataji wa mazao unaweza kuwa na maana kubwa
ikiwa kampuni zitanunua mazao kutoka kwa wakulima wa Tanzania, badala ya kuleta
bidhaa kutoka nje. Benki ya Dunia inapendekeza kuongeza uwekezaji katika
kilimo, pamoja na kuwaunganisha wakulima wadogo na pembejeo na masoko.
Tatu ni Teknolojia na ujuzi. Hapa Kampuni za kimataifa zinaweza kuleta teknolojia, mafunzo na ujuzi ambao baadaye Watanzania wanaweza kutumia katika biashara na ajira zao.
Nne ni Huduma na miundombinu bora
Uwekezaji katika nishati, usafirishaji na miundombinu unaweza kupunguza gharama
za kufanya biashara. Ikiwa gharama hizo zitashuka, biashara ndogo zinaweza
kupata nafasi kubwa zaidi ya kukua.
Lakini kwa ukweli wa Mungu kuna jambo muhimu sana hapa la kuzingatia.
Kuvutia uwekezaji moja kwa moja ni kupunguza umaskini.
Tanzania tayari ina ukuaji wa uchumi wa karibu 6%, lakini Benki ya Dunia inatuonya kwamba ukuaji huo bado haujawa na tija kubwa katika kupunguza umaskini.
Ripoti yake ya Oktoba 2026 inapiga kengele ya hatari kwetu na kunadi kuwa ukuaji wa uchumi unahitaji kutafsiriwa kuwa ajira zenye tija, zenye malipo bora na zilizo salama zaidi. Hapa ndipo Mwanakwetu anawakumbuka nduguze wa Mbagala, Ilonga Mrundu na Ketaketa.
Kwa hiyo, kwa masikini wa Tanzania, maswali muhimu baada ya ziara hii ni haya:
“Je mikataba gani halisi iliyosainiwa? Itazalisha ajira ngapi kwa Watanzania? Ajira hizo zitatupatia kiasi gani?
Wakulima na wafanyabiashara wadogo watanufaikaje? Ni kiasi gani cha thamani kitaongezwa Tanzania badala ya malighafi kusafirishwa nje? Mapato ya serikali yatakayopatikana yataelekezwa kwenye huduma gani za wananchi? Wawekezaji watawajibikaje kuhusu mazingira, kodi, ajira na haki za wafanyakazi? Haya ni maswali ambayo kila Mtanzania aliyepo katika ziara hii ya Waziri Mkuu ajiulize na awe na majibu mbele ya nafsi yake na mbele ya Mungu.”
Kwa mtazamo huo, Mwanakwetu anaona ziara hii inaweza kuwa na manufaa kwa Mtanzania maskini ikiwa kutakuwa na mtaji unaovutwa utazalisha ajira bora, masoko kwa wazalishaji wadogo, ujuzi, biashara za ndani na mapato ya serikali.
Bila hayo tutakuwa tumekuwa wali wenye chuya maana ongezeko la uwekezaji na GDP linaweza kuonekana kwenye takwimu tu huku familia maskini zikiendelea kutohisi mabadiliko makubwa.
Benki ya Dunia yenyewe inaonyesha kwamba sehemu kubwa ya Watanzania bado wanafanya kazi katika kilimo chenye tija ndogo kama vile pale Mrundi Ikangao au shughuli zisizo rasmi kama pale Mbagala Rangitatu.
Kwa kifupi: tusipime ziara hii kwa “amekutana na wawekezaji wangapi?” ; ipime kwa “uwekezaji utakaopatikana utaleta mabadiliko gani kwenye kipato, ajira na gharama za maisha za Mtanzania wa kawaida?”
Mwanakwetu upo? Ndugu zangu Watanzania mimejaribu kujiuluza maswali hayo na kuyajibu kupitia wataalamu na vyanzo kadhaa.
Hizi ni hoja binafsi za Mwanakwetu wa Mbagala.
Kumbuka:
“Ziara ya Waziri Mkuu Uingereza: Je, WaTanzania Masikini Watanufaikaje na Uwekezaji Unaotafutwa?.”
Nakutakia Siku Njema.
0717649257
.gif)










.gif)
.gif)
Post a Comment