Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa — Dodoma
Watumishi wa umma na sekta binafsi nchini wametakiwa kuchangamkia matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku ili kuendana na mabadiliko ya kiteknolojia yanayoendelea duniani.
Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Uhifadhi wa Nyaraka za Taifa, Athanas Kolokota, Oktoba 26, 2026, wakati akifungua mafunzo ya siku mbili kwa watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa jijini Dodoma.
Ndugu Kolokota amesema matumizi ya teknolojia ya kidijitali katika utumishi wa umma si jambo la hiari tena, bali ni hitaji muhimu katika kuboresha ufanisi, kuongeza kasi ya utoaji wa huduma na kurahisisha utekelezaji wa majukumu ya kikazi.
“Najua hapa kila mmoja anayo simu janja, na kila mmoja anatekeleza majukumu yake kupitia kompyuta. Hii ndiyo habari ya mjini,” amesema Kolokota, akisisitiza umuhimu wa watumishi kuendana na mabadiliko ya teknolojia katika ulimwengu wa sasa.
Katika mada ya kwanza ya mafunzo hayo, Afisa TEHAMA, Joseph Mushi, aliwaelimisha watumishi kuhusu matumizi ya sahihi ya kidijitali (Digital Signature) katika mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa nyaraka za ofisi (e-Office).
Mushi amesisitiza kuwa nyaraka za umma zinazoshughulikiwa kupitia mfumo huo zinapaswa kusainiwa kwa njia ya kielektroniki kulingana na taratibu zilizowekwa, badala ya kutegemea sahihi za kawaida za mkono pekee.
Ameeleza kuwa sahihi ya kidijitali ina mchango mkubwa katika kuimarisha usalama wa nyaraka, kuthibitisha utambulisho wa msaini na kuhakikisha kuwa taarifa zilizowasilishwa hazijabadilishwa baada ya kusainiwa.
Kwa mujibu wa Mushi, teknolojia hiyo hutumia mbinu za usimbaji fiche (cryptography) kusaidia kulinda uhalisi na uadilifu wa nyaraka za kielektroniki.
Aidha, amesema matumizi ya sahihi ya kidijitali hurahisisha uhifadhi na upatikanaji wa nyaraka, kwa kuwa nyaraka hizo zinaweza kuhifadhiwa katika mifumo ya kompyuta na kupatikana kwa urahisi zinapohitajika, bila kutegemea mafaili ya karatasi pekee.
Akichangia katika mada hiyo, Afisa Msaidizi wa Kumbukumbu, Ritha Matabaro, aliuliza iwapo sahihi ya kidijitali ina muda wa uhalali unaoweza kuisha.
Akijibu swali hilo, Nduggu Mushi amesema sahihi hizo zina utaratibu wa kuhuisha uhalali wake, akieleza kuwa kwa mfumo unaotumika katika mazingira hayo, mchakato wa kuhuisha hufanyika kila mwaka. Ameongeza kuwa mtumiaji huarifiwa kupitia barua pepe na kufanyiwa usajili upya na Afisa TEHAMA.
Akizungumza kando ya mafunzo hayo, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Ndugu Dismas Mbando, ameeleza kuwa matumizi ya sahihi ya kidijitali yana manufaa mbalimbali katika usimamizi wa nyaraka za umma.
Ndugu Mbando amesema miongoni mwa manufaa hayo ni uthibitishaji wa utambulisho, unaosaidia kuhakikisha kuwa nyaraka imesainiwa na mtu aliyeidhinishwa, pamoja na ulinzi wa uadilifu wa taarifa, unaosaidia kubaini mabadiliko yaliyofanywa kwenye nyaraka baada ya kusainiwa.
Ameongeza kuwa matumizi ya sahihi ya kidijitali huokoa muda na gharama kwa kupunguza ulazima wa kuchapisha nyaraka, kuzisaini kwa mkono, kuzichanganua na kuzituma kwa njia za kawaida.
“Matumizi ya mifumo ya kidijitali yanarahisisha michakato ya kikazi, yanaongeza ufanisi na kupunguza muda unaotumika kushughulikia nyaraka,” amesisitiza.
Mbando pia amebainisha kuwa kupunguza matumizi ya karatasi kupitia mifumo ya kielektroniki kunachangia utunzaji wa mazingira na kuunga mkono utekelezaji wa shughuli za ofisi kwa njia zinazozingatia matumizi bora ya rasilimali.
Mafunzo hayo ya siku mbili yanalenga kuwajengea watumishi uelewa na uwezo wa kutumia teknolojia ya kidijitali katika kutekeleza majukumu yao, kwa msisitizo wa kuboresha usimamizi wa nyaraka, kuimarisha usalama wa taarifa na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.
makwadeladius@gmail.com- 0717649257
.gif)




















.gif)
Post a Comment