WATOTO WANAPASWA KUSAIDIA KAZI ZA NYUMBANI KULINGANA NA UMRI NA UWEZO WAO


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Ilipofika saa kumi na mbili jioni Rehema alikuwa amekaa sebuleni akitazama televisheni huku mama yake akihangaika jikoni kuandaa chakula. Ingawa mama yake alikuwa amechoka baada ya siku nzima ya kufanya biashara Rehema hakujali kumsaidia hata kwa kazi ndogo.

Rehema alikuwa na umri wa miaka kumi na mitatu na aliamini kuwa kazi za nyumbani zilikuwa jukumu la mama yake pekee. Kila alipoombwa kufagia, kuosha vyombo au kupanga vitu vyake alijibu kuwa alikuwa na kazi nyingi za shule hata siku ambazo hakuwa na kazi yoyote.

Siku moja mama yake alirudi nyumbani akiwa amechoka sana na kuumwa na kichwa. Alimwomba Rehema amsaidie kuandaa chakula kwa sababu hakuwa na nguvu za kusimama jikoni kwa muda mrefu.


Badala ya kumsaidia Rehema alijibu kwa hasira kuwa alikuwa akitazama kipindi alichokipenda na hakuwa tayari kukikatiza. Mama yake hakujibizana naye. Alikwenda chumbani kupumzika huku chakula kikiwa bado hakijaandaliwa.

Baadaye Rehema alipoingia jikoni kutafuta chakula alikuta hakuna kilichoandaliwa. Alijaribu kuandaa mwenyewe lakini alishindwa kufanya baadhi ya mambo aliyokuwa ameyazoea kufanyiwa na mama yake.

Alipomwona mama yake akiwa amelala kwa uchovu alianza kutafakari namna alivyokuwa akimpuuza kila siku. Alitambua kuwa mama yake alikuwa akifanya kazi nyingi ili kuhakikisha familia inapata mahitaji yake huku yeye akichukulia juhudi hizo kuwa jambo la kawaida.


Rehema aliamua kuandaa chakula kwa msaada mdogo wa mama yake kisha akaanza kujifunza kufanya kazi za nyumbani kulingana na uwezo wake.

Kuanzia siku hiyo alianza kumsaidia mama yake bila kusubiri kukumbushwa. Pia alijifunza kuwa kuishi pamoja kama familia kunahitaji ushirikiano wa kila mmoja.



emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments