Adeladius Makwega – OFISI YA RAIS IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA- Dodoma
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, Mhashamu Wilbroad Henry Kibozi, amewashukuru waamini wa Parokia ya Chamwino Ikulu kwa kazi nzuri wanayoifanya katika kukuza na kuimarisha maisha ya mwanadamu kiroho na kimwili.
Amewahimiza kuendelea kulipenda Kanisa la Mungu na kudumu katika matendo mema ili waendelee kupata baraka za Mungu na hatimaye kila mmoja apate ujira kwa matendo yake mema.
Askofu Kibozi ameyasema hayo katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, wakati wa maadhimisho ya Jumapili ya 29 ya Mwaka A wa Liturujia ya Kanisa, ambapo ameongoza Misa Takatifu zote tatu zilizoadhimishwa katika parokia hiyo siku hiyo.
Askofu Kibozi awahimiza waamini kushiriki shughuli za Kanisa
Akizungumza katika mahubiri na hitimisho la Misa ya kwanza, Mhashamu Kibozi alisema:
“Nipo katika Parokia ya Chamwino kwa ajili ya kuadhimisha Misa Takatifu pamoja na kuwapokea wanachama wa Rita wa Akashia. Pia, ninawajulisha kuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam atakuwa katika Jimbo Kuu la Dodoma Jumamosi, Oktoba 24, 2026, na Jumapili, Oktoba 25, 2026. Naomba mjitokeze kwa wingi kumpokea, kwa kuwa ni mzaliwa na mwenye asili ya jimbo hili.
Ninawaomba waamini muendelee kumwombea Baba Mtakatifu Leo wa XIV, ambaye alikuwa amelazwa hospitalini, na kwa sasa hali yake inatengemaa.”
Akiendelea kuzungumza na waamini hao, Askofu Kibozi aliwakumbusha kuwa Jumapili hiyo ya 29 ilikuwa ni Jumapili ya Umisionari, hivyo akawahimiza kutambua umuhimu wa utume wa Kanisa na kuendelea kushiriki katika kazi za kueneza Injili.
Paroko Mwaudama aeleza mafanikio ya Parokia ya Chamwino Ikulu
Kwa upande wake, Paroko wa Parokia ya Chamwino Ikulu, Padri Mwaudama, alieleza kuridhishwa na mwenendo wa maisha ya kiimani wa waamini wa parokia hiyo, akibainisha kuwa wameendelea kushiriki ibada na kupokea sakramenti mbalimbali za Kanisa.
Akizungumza katika Misa hiyo, alisema:
“Imani ya waamini katika Parokia ya Chamwino imekuwa nzuri. Waamini wanashiriki Misa zote na kusali, wanapokea sakramenti zote, na hata katika suala la ndoa wanazingatia ipasavyo mafundisho ya Kanisa. Hapa, Baba Askofu, umesikia matangazo ya ndoa; kwa ujumla, tuna ndoa 49.
Waamini wanatoa matoleo, na kwa sasa matoleo yao yameongezeka. Kwa mfano, kwa mwezi tunapata kati ya shilingi milioni tano na milioni 11. Niseme wazi mbele yako kuwa waamini wa parokia hii wanafanya vizuri katika imani na utoaji wa matoleo.
Msalimu sana Askofu Mkuu. Tunawaombea nyote, nasi tunaomba mtuombee.”
Misa hiyo ya kwanza ilianza saa 12 kamili asubuhi, huku kanisa likiwa limejaa waamini waliohudhuria ibada hiyo katika hali ya utulivu.
Historia ya Ukatoliki na kilimo cha zabibu Dodoma
Historia ya Kanisa Katoliki katika maeneo ya mbuga za Dodoma inahusishwa na mwanzo wa karne ya 20, mwaka 1907. Kwa mujibu wa taarifa za kiserikali, wamisionari Wakatoliki walichangia kuanzishwa kwa kilimo cha zabibu katika eneo hilo mwaka 1938.
“Zao hili lilianzishwa kwa mara ya kwanza kama majaribio kupitia wamisionari wa Kanisa Katoliki katika Kituo cha Misheni cha Bihawana (Bihawana Misheni) kilichopo Dodoma. Baadaye, hatua kubwa za kiserikali zilifuata ili kukuza kilimo hiki:Mwaka 1974: Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya China ilirasimisha kituo cha mafunzo cha Bihawana Farmers Training Center (BFTC) ili kuwafundisha wakulima mbinu bora za kilimo cha zabibu. Mwaka 1978: Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI-Makutupora kilianzishwa mahususi kwa ajili ya kufanya utafiti wa aina mbalimbali za mizabibu.”
Takwimu za uzalishaji wa zabibu mkoa wa Dodoma zinaokeza haya
“Mwaka wa 2021/2022 tani 10,000, 2022/2023 tani 16,000, 2023/2024 tani 14000. 2024/2025 tani 17,000 ambapo katika soko la dunia tani moja inauzwa ziadi ya Euro 2000 na kila moja inauzwa kwa euro katika 1-2 kulingana na ubora wa zabibi.”
Kwa hiyo, kila msomaji wangu unapoona mashamba ya zabibu katika Mkoa wa Dodoma, yanakumbushwa historia ya uhusiano kati ya uwepo wa imani ya Kikatoliki na maendeleo ya kilimo katika eneo hilo.
Kilimo cha zabibu mkoani Dodoma ni miongoni mwa shughuli za kilimo zinazochangia uchumi wa eneo hilo na kwa mwaka 2038, Tanzania itatimiza miaka 100 tangu mwaka unaotajwa kuwa mwanzo wa kilimo cha zabibu nchini.
Maaskofu walioliongoza Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma
Katika historia ya uongozi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, mwandishi anawataja maaskofu wafuatao:
- Askofu Antony Jeremia Pesce (1953–1971).
- Askofu Matthias Joseph Isuja (1972–2005).
- Askofu Jude Thadaeus Ruwa’ichi (2005–2010).
- Askofu Gervas John Nyaisonga (2011–2013).
- Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya (2014–2026, kwa mujibu wa taarifa ya mwandishi).
Askofu Mkuu Beatus Kinyaiya amekuwa akisaidiwa na Askofu Msaidizi Wilbroad Henry Kibozi, ambaye aliteuliwa mwezi Februari 2024. Askofu Kibozi alitembelea Parokia ya Chamwino Ikulu tarehe 18 Oktoba 2026, na kuongoza Misa Takatifu katika parokia hiyo.
Hitimisho
Historia ya kilimo cha zabibu Dodoma ni sehemu ya simulizi pana kuhusu dini, jamii, kilimo na maendeleo ya uchumi katika eneo hili. Ni muhimu kuendelea kuitunza na kuichunguza historia hiyo ili vizazi vijavyo vifahamu mchango wa taasisi na jamii mbalimbali katika maendeleo ya Dodoma.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka kauli hii:
“Wakatoliki Walileta Zao la Zabibu Dodoma.”
Nakutakia siku njema!
makwadeladius@gmail.com 0717649257
.gif)











.gif)
Post a Comment