URAFIKI WA KWELI HAUJENWGI KWA UTAJIRI, ZAWADI AU UMAARUFU BALI KWA UPENDO, UAMINIFU NA KUSAIDIANA



Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Siku moja wakati wa mapumziko wanafunzi wa shule moja ya msingi jijini Mwanza walikuwa wakicheza mpira uwanjani. Miongoni mwao walikuwa Kelvin na Musa.Marafiki waliokuwa wakikaa pamoja darasani na kusaidiana katika masomo.

Kelvin alikuwa mtoto aliyependa kuwa karibu na wanafunzi waliokuwa na vitu vizuri. Alipata rafiki mpya aliyeitwa Bryton ambaye familia yake ilikuwa na uwezo wa kifedha. Tangu aanze urafiki huo Kelvin alianza kumtenga Musa kwa sababu hakuwa na vitu vya gharama kama Bryton.

Siku moja Musa alifika shuleni akiwa na huzuni kwa sababu mama yake alikuwa mgonjwa na hakuwa na fedha za kununua vitafunwa. Alipomwomba Kelvin amsaidie kwa kumpa sehemu ya chakula chake Kelvin alikataa na kumwambia amuombe Bryton kwa sababu yeye ndiye rafiki yake wa karibu.

Musa aliondoka kimya kimya na kukaa chini ya mti. Mwalimu aliyekuwa akipita alimwona na kumuuliza kilichokuwa kimemsibu. Musa alimweleza kuwa alikuwa na matatizo nyumbani na pia alikuwa ameachwa na rafiki yake.

Mwalimu alimfariji na kumwambia kuwa urafiki wa kweli haupimwi kwa mali bali kwa namna watu wanavyosimama pamoja wakati wa shida.



Wiki iliyofuata Kelvin alisahau daftari lake la hesabu nyumbani. Alipofika darasani aligundua kuwa alikuwa na mtihani na hakuwa na daftari la kupitia maswali aliyokuwa amepewa. Bryton hakuweza kumsaidia kwa sababu alikuwa hajafanya maandalizi ya kutosha.

Musa ambaye alikuwa amesikia tatizo lake alimpa daftari lake ili Kelvin apitie maswali kabla ya mtihani kuanza.

Kelvin alishangaa kuona kuwa Musa alikuwa tayari kumsaidia licha ya jinsi alivyokuwa amemtendea. Alijisikia aibu na kuamua kumwomba msamaha.

Musa alimsamehe na wawili hao wakaanza tena urafiki wao. Kelvin alijifunza kuwa rafiki wa kweli si yule anayekuwa nawe wakati wa furaha pekee bali pia anayekujali wakati wa shida.

 

emakulatemsafiri@gmail.com

0653903872


0/Post a Comment/Comments