TUSIMFISHE MTOTO WA MWENYE SHAMBA

 



Adeladius Makwega – DODOMA

“Leo ni Jumapili ya 27 ya Mwaka A wa Liturujia ya Kanisa.” Katika Injili ya leo, Yesu anatumia mfano kutufundisha kuhusu Mungu, ambaye ndiye mmiliki wa kweli wa Ufalme wake.

 

Kulikuwa na mwenye shamba aliyepanda shamba la mizabibu, akaliweka mikononi mwa wakulima wapangaji na kuwaamini walitunze na kulisimamia.

 

Wakati wa mavuno ulipofika, mwenye shamba aliwatuma watumishi wake kwenda kuchukua sehemu ya mazao yake. Lakini wapangaji waliwakataa watumishi hao, wakawatesa na hata kuwaua.

 

Hatimaye, mwenye shamba akamtuma mwanawe, akifikiri kwamba wapangaji wangemheshimu. Lakini wao pia walimkataa mwanawe na kumuua.

 

Ndugu wapendwa, walifikiri kwamba kwa kumuua mwana wa mwenye shamba, wangeweza kujipatia urithi wake.

 

Kupitia mfano huu, Bwana anatufundisha kwamba Mungu anajenga Ufalme wake kwa njia ya Neno lake, kwa kuwatumia watu anaowatuma kulitangaza Neno hilo, na kwa upendo na utunzaji wake kwa wanadamu.

 

Lakini swali muhimu tunalopaswa kujiuliza ni hili: Je, tuko tayari kuupokea utendaji wa Mungu katika kujenga Ufalme wake, au tunataka kujijengea falme zetu wenyewe?

 

Tunapaswa kutambua kwamba sisi ni watunzaji tu wa yale ambayo Mungu ametukabidhi. Maisha yetu, vipaji vyetu, familia zetu na kila tulicho nacho ni zawadi kutoka kwake. Mungu anatarajia tuzae matunda mema na tuyatumie kwa ajili ya Ufalme wake.

Basi, tumwombe Mungu ili Ufalme wake uendelee kuzaa matunda ndani yetu na kupitia maisha yetu. Tuwe tayari kusikiliza Neno lake, kuwapokea wajumbe wake, na kutekeleza mapenzi yake kwa upendo na uaminifu.

Amina.

 

Haya ni maneno ya Kadinali Luis Antonio Tagle, Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki, inayojihusisha na Uinjilishaji wa Watu ndani ya Kanisa Katoliki ulimwenguni.

 

Huku hapa Tanzania:

Jumapili hii, Oktoba 4, 2026, Mwanakwetu alisali Misa hiyo katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

 

Misa iliendeshwa vizuri huku Padri Mwaudama, aliyesalisha Misa hiyo, akitoa nafasi kwa wale Wakristo waliozaliwa mwezi wa tisa kupita mbele na kupokea baraka.

 

Walijongea madhabahuni wakiwa karibu watu kumi; mwanaume mmoja, kina mama sita na watoto wawili. Huyu mwanaume mmoja alikuwa Mwanakwetu. Wakapokea baraka na kurudi vitini huku wakiimbiwa wimbo wa Happy Birthday.

Wakati wa matangazo, msomaji wa matangazo hayo alisoma taarifa ya makusanyo ya sadaka ya parokia hii:

 

“Sadaka kwa Jumapili iliyopita ilikuwa ni shilingi 5,001,000, huku zaka kwa mwezi Septemba 2026 ikiwa ni shilingi 10,090,800. Asanteni kwa wote mliotoa.”

 

Kutokana na tangazo hili, Mwanakwetu alitamani kueleza kwa kina mwongozo wa Kanisa kuhusu namna sadaka na zaka zinavyopaswa kutumika kulingana na kanuni na sheria za Kanisa (Canon Law), maana misingi hii imewekwa kitambo sana.

 

Canon Law haitoi asilimia maalum, kwa mfano 60% kwa parokia na 40% kwa Jimbo, kwa sadaka ya kawaida ya Jumapili. Mgao huo, kama upo, unatokana na kanuni au utaratibu wa Jimbo husika, si kutoka katika Canon Law yenyewe. Hata hivyo, Canon Law inampa Askofu wa Jimbo mamlaka ya kuweka kanuni hizo.

 

Canon 531 inaelekeza kwamba sadaka zinazopokelewa katika shughuli za parokia ziingizwe katika mfuko wa parokia, isipokuwa pale ambapo nia ya mtoaji kuhusu sadaka hiyo imeelezwa wazi kuwa ni kwa madhumuni mengine.

 

Katika kulifafanua hili, mathalani, muumini Mwanakwetu anaweza kutoa shilingi milioni moja kwa ajili ya huduma za kiroho vijijini au maboresho ya vigango vya Parokia XYZ. Hapo hakuna mjadala: fedha hiyo inapaswa kuelekezwa kwenye kusudi lililotajwa katika nia ya muumini.

Au muumini Kazingoma ametoa shilingi milioni tatu ziende kwa ajili ya yatima wa Parokia WYZ; fedha hiyo inapaswa kuelekezwa huko, kama sheria namba 531 inavyoelekeza.

 

Isitoshe, Canon 537 inasema kila parokia inapaswa kuwa na Baraza la Uchumi la Parokia (Parish Finance Council). Baraza hilo linamsaidia paroko katika usimamizi wa mali za parokia, kwa kufuata kanuni za Askofu wa Jimbo na sheria za Kanisa. Hii ina maana kwamba paroko anasimamia mali za parokia kwa niaba ya Kanisa na kwa mujibu wa sheria za Kanisa. Huku Canon 532 pia ikiweka jukumu kwa paroko kuhakikisha mali za parokia zinasimamiwa kwa mujibu wa sheria.

Nadhani msomaji wangu, tupo pamoja.

 

Kwa mujibu wa Canon Law, mali za Kanisa zinapaswa kutumika kwa malengo yanayofaa kwa Kanisa, hasa ibada na maisha ya kiroho, gharama za ibada, liturujia, vifaa vya kanisa, uinjilishaji na katekesi, mahitaji ya kichungaji ya parokia, matengenezo ya kanisa na majengo ya parokia, kuwasaidia wahitaji na kazi za huruma, wakiwamo wagonjwa na maskini, kuwahudumia na kuwawezesha wahudumu wa Kanisa kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa, pamoja na kuchangia mahitaji ya Jimbo pale ambapo kuna utaratibu wa Jimbo wa kufanya hivyo. Pia yapo mahitaji mengine halali ya Kanisa yaliyoidhinishwa na mamlaka husika.

 

Canon 1260 inatambua haki ya Kanisa kupata kile kinachohitajika kwa ajili ya malengo yake, na Canon 1262 inaelekeza waamini kusaidia Kanisa kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na Mkutano wa Maaskofu.

Kwa maelezo hayo,

“Sadaka za Jumapili zinaweza kuwa na nafasi katika mahitaji ya kichungaji ya parokia, matengenezo ya kanisa na majengo ya parokia, kuwasaidia wahitaji na kazi za huruma, na kuchangia mahitaji ya Jimbo pale ambapo kuna utaratibu wa Jimbo wa kufanya hivyo.”

 

Mwanakwetu anasema nini:

 

“Kama Wakristo tumejipanga vizuri tangu jumuiya hadi Jimboni, haiwezekani Mkatoliki miongoni mwetu akafa kwa njaa kisa umasikini, akakosa elimu kisa umasikini, akafariki kisa kakosa pesa ya dawa. Lakini tukumbuke kama tumejipanga vizuri...”

Ndiyo maana Kadinali Luis Antonio Tagle Jumapili hii anasema:

 

“Tunapaswa kutambua kwamba sisi ni watunzaji tu wa yale ambayo Mungu ametukabidhi. Maisha yetu, vipaji vyetu, familia zetu na kila tulicho nacho ni zawadi kutoka kwake.”

 

Tunapokwenda kinyume na wajibu huo, tunamfisha yule Mtoto wa Mwenye Shamba katika shamba lake tukidhani tutakadhiwa  hilo shamba, ambapo mtoto wa mwenye shamba ni Yesu Kristo.Kwa hiyo Tusimfishe Mtoto wa Mwneye Shamba.”

Mwanakwetu, upo?

Kumbuka:

“TUSIMFISHE MTOTO WA MWENYE SHAMBA.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments