Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kila siku asubuhi Daudi aliona aibu baba yake alipokuja kumchukua shuleni akiwa amevaa nguo zilizochakaa na kuendesha baiskeli ya zamani. Alitamani baba yake awe kama wazazi wa baadhi ya marafiki zake waliokuwa wakifika shuleni kwa magari.
Siku moja shule yao ilitangaza kuwa wanafunzi wangekutana na wazazi wao kwa ajili ya kuzungumzia maendeleo ya masomo. Daudi aliwaomba wanafunzi wenzake wasimwone baba yake siku hiyo kwa sababu aliona aibu hali yake ya maisha.
Baba yake alifika shuleni kama wazazi wengine lakini Daudi hakutaka kukaa karibu naye. Alijifanya kuwa anamtafuta mwalimu na kumwacha baba yake akiwa amekaa peke yake.
Aliporudi nyumbani baba yake hakumkaripia. Badala yake alimwuliza kama alikuwa na jambo lililomfanya ajisikie vibaya. Daudi alikaa kimya lakini baadaye alikiri kuwa alikuwa akiona aibu kwa sababu baba yake hakuwa na gari wala nguo nzuri kama wazazi wa wenzake.
Baba yake aliumia moyoni lakini alimweleza kuwa maisha hayafanani kwa kila familia. Alimwambia kuwa licha ya changamoto za kifedha alikuwa akifanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha Daudi anapata chakula, sare na mahitaji ya shule.
Maneno hayo yalimfanya Daudi aanze kufikiria upya mtazamo wake. Alikumbuka siku ambazo baba yake alitembea umbali mrefu kumpeleka hospitalini alipokuwa mgonjwa na jinsi alivyokuwa akifanya kazi hadi usiku ili kulipa gharama za shule.
Siku chache baadaye shule ilipofanya mkutano mwingine Daudi alikaa karibu na baba yake bila kujali watu wengine wangesema nini. Alimshukuru kwa kujitolea kwake na kumwomba msamaha kwa kumdharau.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment