Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Baada ya kula vitafunwa wakati wa mapumziko wanafunzi wengi walikuwa wakitupa mifuko ya plastiki na karatasi chini ya miti na kwenye viwanja vya shule. Ingawa shule ilikuwa na mapipa ya taka wachache tu ndio waliokuwa wakiyatumia.
Siku moja upepo mkali ulivuma na kutawanya takataka katika uwanja mzima. Baadhi ya mifuko iliziba mifereji ya maji huku karatasi zikijaa kwenye njia zilizotumiwa na wanafunzi.
Asubuhi iliyofuata mwalimu alipofika shuleni aliwaomba wanafunzi waangalie mazingira yao kabla ya kuingia madarasani. Wengi walishangaa kuona shule yao ikiwa chafu kiasi hicho.
Badala ya kuanza masomo mara moja mwalimu aliwagawa katika vikundi ili wasafishe maeneo mbalimbali ya shule. Wakati wa usafi wanafunzi waligundua kuwa baadhi ya takataka zilikuwa zimekaa kwa muda mrefu na kufanya eneo fulani litoe harufu mbaya.
Baada ya kusafisha walikubaliana kuweka utaratibu wa kutumia mapipa ya taka na kuhakikisha kila mwanafunzi anawajibika kwa usafi wa mazingira.
Wiki zilizofuata shule ilianza kuonekana safi zaidi. Wanafunzi walijifunza kuwa mazingira bora hayategemei wafanyakazi wa usafi pekee bali pia tabia za kila mtu.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment