Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kwa muda wa wiki mbili Nuru alikuwa akiona mama yake akitoka sebuleni na kwenda kuzungumza kwa simu chumbani. Kila alipomuuliza alikuwa akizungumza na nani, mama yake alimjibu kuwa ni mambo ya kikazi. Nuru hakutilia maanani jambo hilo mpaka siku moja alipokuta mama yake akifuta machozi huku akishikilia simu yake.
Akiwa na umri wa miaka kumi na miwili Nuru alikuwa amezoea kumweleza mama yake kila jambo lililotokea shuleni. Hata hivyo siku za hivi karibuni mama yake alikuwa akionekana mwenye mawazo mengi na wakati mwingine alisahau hata kumuuliza kuhusu masomo yake.
Siku moja jioni simu ya mama yake ilipokuwa mezani ujumbe uliingia. Nuru aliona jina la mjomba wake kwenye skrini na ujumbe uliosomeka “Usikate tamaa dada yangu mambo yatakuwa sawa".
Ujumbe huo ulimfanya Nuru awe na maswali mengi. Alianza kufikiri kuwa huenda mama yake alikuwa na tatizo kubwa ambalo hakutaka kumweleza.
Usiku huo aliamua kukaa karibu na mama yake badala ya kwenda chumbani kucheza kama kawaida. Alimsaidia kupanga vyombo na kumweleza kuhusu jambo la kuchekesha lililotokea shuleni. Mama yake alitabasamu lakini Nuru aliona bado alikuwa na huzuni.
Baada ya muda Nuru alimuuliza kwa upole kama kulikuwa na jambo lililokuwa likimsumbua. Mama yake alikaa kimya kwa muda kisha akamweleza kuwa alikuwa na changamoto za kifedha baada ya biashara yake kupata hasara.
Nuru alimsikiliza na kumkumbatia. Ingawa hakuwa na uwezo wa kutatua tatizo hilo alimwambia kuwa angeendelea kufanya vizuri shuleni na kusaidia kazi ndogo za nyumbani ili kupunguza majukumu yake.
Mama yake alifurahi kuona jinsi mwanawe alivyomjali. Alimweleza kuwa si kila tatizo la mtu mzima linapaswa kubebwa na mtoto lakini kuzungumza kwa uwazi na kusaidiana katika familia ni jambo muhimu.
Kuanzia siku hiyo Nuru aliacha kujenga hofu kutokana na mambo ambayo hakuyajua. Alijifunza kuuliza kwa upole badala ya kufanya hitimisho lake mwenyewe.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment