SIKU AMBAYO SIRI YAKE ILIFICHUKA


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Jumatatu moja asubuhi wanafunzi walikuwa wakijiandaa kuingia darasani katika shule moja ya msingi jijini Mwanza. Miongoni mwao alikuwepo mtoto aliyekuwa na tabia ya kuficha ukweli kila alipofanya kosa. Alidhani kuwa kusema uongo kungemsaidia kuepuka adhabu bila kutambua kuwa tabia hiyo ilikuwa ikimfanya apoteze uaminifu wa watu waliomzunguka.

Siku hiyo mwalimu aliwaagiza wanafunzi kukamilisha kazi ya nyumbani ambayo walikuwa wamepewa Ijumaa. Mtoto huyo hakuwa ameifanya kwa sababu alitumia muda mwingi kucheza. Mwalimu alipomwuliza alidai kuwa daftari lake lilikuwa limepotea.

Mwalimu alimruhusu akatafute daftari hilo lakini mtoto alijua kuwa hakuwa na daftari lolote alilopoteza. Aliporudi nyumbani mama yake alipomwuliza kuhusu masomo alidai kuwa mwalimu hakuwa amewapa kazi yoyote.

Siku iliyofuata mama yake alipokutana na mwalimu shuleni alielezwa kuwa mtoto hakuwasilisha kazi yake. Mama yake alishangaa kwa sababu mtoto alikuwa amemweleza jambo tofauti kabisa.


Jioni hiyo alipofika nyumbani mama yake alimwita na kumweleza alichokisikia kutoka kwa mwalimu. Mwanzoni alijaribu kujitetea lakini baadaye alikiri kuwa alikuwa amesema uongo kwa sababu aliogopa kukemewa.

Mama yake alimweleza kuwa kufanya makosa ni sehemu ya kujifunza lakini kuficha ukweli kunafanya iwe vigumu kwa watu kumwamini. Alimshauri ajifunze kuwajibika badala ya kutafuta sababu za kujitetea.

Mtoto aliamua kubadilika. Siku iliyofuata alimwomba mwalimu msamaha na kuomba nafasi ya kukamilisha kazi yake. Ingawa alilazimika kutumia muda wake wa mapumziko kumalizia kazi hiyo aljisikia mwenye amani kwa sababu alikuwa ameamua kusema ukweli.

Kuanzia siku hiyo alianza kujifunza kuwa mkweli hata alipokosea.



emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872

.



0/Post a Comment/Comments