SIKU ALIPOACHA KUJILINGANISHA NA MTOTO MWENZAKE


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Kila matokeo ya mtihani yalipotangazwa mtoto mmoja alikuwa na tabia ya kumlinganisha mwanafunzi aliyekaa karibu naye.

“Yeye amepata zaidi yangu"

Alianza kujiona hafai kwa sababu mwenzake alikuwa akipata alama za juu mara nyingi.

Hata alipofanya vizuri furaha yake haikudumu. Alikuwa akiangalia kwanza mwenzake amepata alama ngapi.

Siku moja mwalimu aliwapa kazi ambayo kila mwanafunzi alipaswa kuifanya kwa uwezo wake. Hakukuwa na mashindano wala nafasi za kulinganisha alama.


Mtoto huyo alipoanza kufanya kazi aligundua kuwa alikuwa na uwezo mkubwa kwenye sehemu fulani ambazo mwenzake hakuzimudu.

Alianza kujiuliza kwa nini alikuwa ametumia muda mwingi kuangalia maendeleo ya mtu mwingine badala ya kuangalia yake.

Kuanzia siku hiyo alibadilisha mtazamo wake. Alianza kuweka malengo yake mwenyewe kusoma vizuri zaidi, kumaliza kazi kwa wakati na kuongeza alama zake kidogo kidogo.


Matokeo yaliyofuata hayakuwa mazuri sana lakini yalikuwa bora kuliko yake ya awali.

Safari hii hakumtafuta mwenzake ili kujua amepata kiasi gani.

Aliangalia alama zake akatabasamu na kusema moyoni “Nimepiga hatua"




emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments