RUSHWA HAINA MSHINDI

ADELAIUS MAKWEGA – OFISI YA RAIS, IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA, DODOMA

 

Mwanakwetu: Tunajifunza nini katika mapambano dhidi ya rushwa?

 

Mapema Oktoba 5, 2026, Mwanakwetu

akiwa katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, alikutana na Bi. Entuja Philip Mbwambo, ambaye ni Mkutubi, na kufanya naye mazungumzo kuhusu rushwa nchini Tanzania.

 

Katika mazungumzo hayo ya dakika nne, Bi. Mbwambo alisimulia kisa hiki:

 

“Kuna mama mmoja alikuwa na ndugu yake mgonjwa. Alimpeleka katika hospitali ya umma ili aweze kupatiwa matibabu. Alipofika hospitalini, mgonjwa alipatiwa huduma za vipimo vizuri na baadaye akaambiwa kuwa atapangiwa daktari bingwa ili aweze kufanyiwa upasuaji.

Suala la kumpangia daktari lilichukua muda, huku mgonjwa akiwa bado amelazwa wodini. Katika hali ya kushangaza, wagonjwa wengine waliofika baada yake walipangiwa daktari huyo huyo na kufanyiwa upasuaji, lakini mgonjwa wa mama huyu hakupangiwa daktari.

 

Hoja hii ilileta maswali. Mama huyu alipowauliza ndugu wa wagonjwa wengine, walimjulisha kuwa wao walitoa shilingi 250,000 na ndiyo maana wagonjwa wao walipangiwa haraka. Wakamwambia, ‘Ukisubiri utachoka, maana mkono mtupu haulambwi.’

Mama huyu alijiuliza: Afanye nini? Tatizo ni wapi atakapopata pesa hizo, wakati wao wanatoka kijijini na hawana A, B, C wala D?

 

Walipowajulisha ndugu zao kuhusu suala hilo, walisema kutoa shilingi 250,000 haiwezekani. Kwanza, kwao msimu wa kilimo ulikuwa umepita. Pia, walijiuliza: kumpa mtu pesa hiyo si utaratibu? Je, pesa hiyo inatolewa risiti? Jibu likawa hapana.

 

Ndugu mmoja miongoni mwao akasema yeye anajua pa kuipata pesa hiyo, na hilo likafanyika vizuri ili mgonjwa aweze kutibiwa.

 

Pesa ikapatikana. Siku iliyofuata, ndugu hawa wakaambatana na pesa yao na kuitwa kwa tabibu ili kulipa na mgonjwa wao apangiwe siku ya kufanyiwa upasuaji.

 

Walipofika ndani ya chumba cha tabibu, ndugu mwenye pesa na mgonjwa wakaingia na kumkabidhi daktari pesa yote taslimu. Mgonjwa akapangiwa siku ya upasuaji kuwa ni kesho yake.

 

Ndugu na mgonjwa wakawa wananyanyuka kwenye kiti ili watoke nje. Mara ghafla, askari kanzu wawili wakaingia ndani ya chumba cha tabibu.

 

Wakasema, ‘Daktari, upo chini ya ulinzi. Umepokea hongo ya shilingi 250,000. Sisi ni maafisa wa kuzuia na kupambana na rushwa. Kwa mamlaka tuliyopewa, upo chini ya ulinzi na sasa tunakukagua kama kweli unayo pesa hiyo.’

 

Kweli, ndani ya chumba cha daktari upekuzi ukafanyika, lakini daktari huyu hakukutwa na hata shilingi moja. Alikutwa na peni, kipima presha na dawa za maumivu aina ya diclofenac mfukoni.

 

Jambo hili likaleta utata. Wale askari kanzu wakawageukia ndugu wa mgonjwa na kuwauliza, ‘Pesa yetu iko wapi?’

Askari kanzu wakaanza kuwaadhibu ndugu wa mgonjwa waliodai kuwa pesa hiyo walikuwa wamempa daktari.

Ndugu huyu akasema kuwa pesa hiyo amemkabidhi daktari kama ilivyo.

Naye daktari akakana kwamba hajachukua pesa hiyo na kwamba hana pesa hiyo mifukoni mwake.

Hapa sasa daktari na ndugu wa mgonjwa wakawa chini ya ulinzi.

 

Kumbuka, yule mgonjwa alipangiwa kufanyiwa upasuaji siku iliyofuata. Mgonjwa alirudi wodini, lakini daktari na ndugu wa mgonjwa wakapelekwa mahabusu.

 

Siku iliyofuata, mgonjwa hakufanyiwa upasuaji. Huku hospitalini kukawa na taharuki juu ya tukio hilo, viongozi wa madaktari wakihangaika huku na kule, huku uongozi wa hospitali ukipanga namna ya kulimaliza jambo hili.

 

Siku ya tatu, kule hospitalini, hali ya yule mgonjwa ilikuwa mbaya sana. Hatimaye akafariki dunia, huku mahabusu daktari na ndugu wa mgonjwa wakiwa bado ndani.

 

Kumbuka, ile shilingi 250,000 ilikuwa pesa ya serikali iliyopotea katika hali ya utata. Je, jambo hili linatuliwaje?

Uongozi wa madaktari pamoja na Mganga Mkuu wakaketi pamoja na kuamua kutoa shilingi 1,000,000 ili kulimaliza jambo hili kwa wahusika kimya kimya. Jambo hili likajadiliwa na kuwekwa sawa, wahusika wakakabidhiwa kiasi hicho na ndugu hao wakaachiwa huru na kurudi majumbani mwao.

 

Ndugu wa mgonjwa wakarudi hospitalini, wakakabidhiwa mwili wa mgonjwa wao, kisha wakarudi zao nyumbani kimya kimya.

Wakachukua maiti ya ndugu yao na kwenda kuzika nyumbani kwao.”

 

Mkutubi Entuja Mbwambo akauliza:

 

“Katika tukio hili tunajifunza nini?”

 

Mwanakwetu akasema:

“Huko unapokwenda ni mbali sana. Kwanza nataka kujua ile pesa ya hongo aliyopewa daktari, baada ya kuipokea aliifikisha wapi? Mbona hakukamatwa nayo?”

Bi. Entuja akasema:

“Mle ofisini kwa daktari, kiti cha tabibu kilikuwa jirani na upenyo wa mbao uliokuwa ukielekea kwenye chumba cha pili. Alipopokea pesa hiyo, aliipenyeza haraka nyuma ya upenyo huo, na muuguzi wa chumba cha pili akaipokea kwa madaha na kuondoka nayo bila mgonjwa na ndugu yake kujua.”

 

Mwanakwetu ndipo akasema:

“Suala la mapambano dhidi ya rushwa si suala la taasisi moja yenye dhamana nalo tu, kama vile PCCB, bali ni jukumu la kila mmoja wetu. Kama kila mmoja akiwa na nia njema, rushwa tunaweza kupambana nayo. Lakini kila mmoja akiwa na lake, mambo yatakuwa hayo hayo kama ilivyo katika kisa hiki.”

 

Baada ya mazungumzo hayo, Entuja aliagana na Mwanakwetu na kila mmoja akachukua njia yake.

 

Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?

Haya ni makala kuhusu rushwa, ambapo Bi. Entuja Mbwambo, Mkutubi kutoka Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, hapa Dodoma, amesimulia kisa hiki.

 

Wewe msomaji wangu unajua nini kuhusu rushwa?

 

Kama unapenda kumfahamu zaidi Bi. Entuja alisoma Shule ya Msingi Amani jijini Dodoma na baadaye Shinghatini Sekondari, Kilimanjaro, na kisha Chuo Kikuu cha Mzumbe, mkoani Morogoro.

Mwanakwetu upo? Kumbuka.

“Rushwa Haina Mshindi.”

Nakutakia siku njema.

Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717 649 257


















 

 




0/Post a Comment/Comments