Adeladius Makwega – MBAGALA
Mara baada ya Mwanakwetu kusikia taarifa za kifo cha Profesa Mmari, taswira mbili zilimjia kichwani.
Taswira ya kwanza:
“Mzee mmoja mpole, anayependa kuvaa miwani na makoti ya mikono mifupi ya samawati yenye mifuko mikubwa mikubwa.”
Taswira ya pili:
“Nikiwa mwanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa katika miaka ya 2005–2010, nilikuwa nikimuona mzee huyu katika baadhi ya vikao vya ndani na mikutano ya wazi ya Vyuo Vikuu vya Tumaini niliyohudhuria kama Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa. Huyu mzee alikuwa Provost wa Tumaini Dar es Salaam?”
Baada ya taswira hizo mbili, safari ya taswira nyingine ndogo ndogo ilipamba moto. Niliwakumbuka wanahabari wawili: kwanza, Mhe. Godwin Gondwe, ambaye ni Mkuu wa Wilaya, na Mohammed Kherefu, ambaye ni mtangazaji, mhariri na mwandishi wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani.
“Godwin Gondwe amesoma Shahada ya Kwanza ya Habari katika Chuo Kikuu cha Tumaini Iringa kuanzia mwaka 2003 hadi 2006. Kulikuwa na wakati ambapo alikuwa mhadhiri msaidizi TUDARCo. Huyu Profesa Mmari amefanya kazi na Gondwe.”
Mwanakwetu nikasema moyoni:
“Kwa namna ninavyomfahamu Godwin Gondwe, najua atakwenda kumzika Profesa Mmari.”
Safari ya fikra iliendelea. Fikra zangu nyingine zikaja katika hili:
“Mwanahabari, mtangazaji na mhariri wa Shirika la Utangazaji la Ujerumani, Mohammed Kherefu, alikuwa Makamu wa Rais wa Serikali ya Wanachuo wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam. Ngoja niangalie katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, ameandika chochote kuhusu msiba huu? Mohammed Kherefu tulikuwa tukikutana naye pamoja na maprofesa hawa katika baadhi ya vikao, na Kherefu alikuwa amekaa karibu na Profesa Mmari.”
Baada ya wazo hili, nilitingwa na kazi na sikupata nafasi ya kwenda kukagua kurasa za mitandao ya kijamii za Mohammed Kherefu.
Majira ya mchana wa Oktoba 13, 2026, nikatumiwa ujumbe huu na Lukas Masunzu kutoka Tabora:
“Kaka Makwega, kwema? Kama ninavyosoma makala yako ya Profesa Mmari, hapa kando yangu kuna mwalimu niliye naye ambaye anasema: ‘Amefundishwa na mke wa Profesa Mmari katika Shule ya Msingi Bungo, mkoani Morogoro, mwaka 1983.’
Huyu mama ni mwalimu mwenzangu. Anasema:
‘Baba wa Profesa Mmari alikuwa mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, na hata baba wa mke wa Profesa Mmari alikuwa mtoto wa mchungaji wa kanisa hilo hilo. Hivyo, Profesa Mmari alilelewa katika mazingira ya kanisa.’”
Baada ya kupokea ujumbe huu, nikarejea wasifu wa Profesa Mmari:
Profesa Mmari aliwahi kufanya kazi kama Makamu Mkuu wa Chuo (Vice-Chancellor) katika vyuo vikuu vitatu nchini Tanzania:
- Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA): Alikuwa Makamu Mkuu wa Chuo wa kwanza, yaani mwanzilishi, kuanzia mwaka 1984 hadi 1988.
- Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM): Alihudumu kama Makamu Mkuu wa Chuo kuanzia mwaka 1988 hadi 1991.
- Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT): Alihudumu kama Makamu Mkuu wa Chuo kuanzia mwaka 1993 hadi 2005.
Baadaye, kuanzia mwaka 2005 hadi 2013, alishika pia wadhifa wa Mkuu wa Chuo (Provost) katika Tumaini Dar es Salaam College (TUDARCo), ambacho kwa sasa kinajulikana kama DarTU.
Mwanakwetu anasema nini siku ya leo?
Mosi, ukiupitia wasifu wa msomi huyu, utabaini kuwa alikuwa msomi ambaye taarifa zake na maisha yake yanaonekana kuhusiana na jamii kwa namna ya pekee. Hebu tazama:
“Adeladius Francis Makwega (MwAnAkWeTu) na Mohammed Kherefu tulikuwa Makamu wa Rais wa Serikali za Wanachuo wa vyuo vya Tumaini, kile cha Iringa na kile cha Dar es Salaam. Huu ni wakati ule ule ambao Profesa Mmari alikuwa akihudumu katika vyuo vya Kanisa. Pia, rejea taarifa kuhusu mke wa Profesa Mmari akiwa mwalimu wa Shule ya Msingi Bungo, Morogoro. Katika miaka inayotajwa, unamuona Profesa Mmari akiwa katika mazingira yaleyale ya Morogoro (SUA) na Dar es Salaam (UDSM).”
Jambo la mwisho, unapokuwa kijana kutoka familia ya Kikristo, na tena wewe ni mtoto wa mchungaji, si lazima na wewe uwe mchungaji. Lakini je, huko unapopita, unaliwakilisha vema Kanisa lako? Unamwakilisha vipi Yesu Kristo? Je, una mchango gani kwa Kanisa lako?
Kwa hakika, Profesa Mmari, akiwa mtoto wa mchungaji, alijitahidi kuliwakilisha vema Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Ni Watanzania wachache wanaoweza kuwa na sifa zinazofanana na zake.
“Utoke SUA, utoke UDSM, na kisha OUT, ukishika nafasi hiyo hiyo ya Makamu Mkuu wa Chuo? Na isitoshe, mchango wako unakuja kutumika katika kufanikisha azma ya Kanisa lako kuwa na vyuo vikuu kadhaa kwa muda mfupi? Huu ni umahiri mkubwa.”
Mwanakwetu ninasema haya:
“Profesa Mmari alikuwa Mchungaji Mwema katika Elimu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Akiwa Provost wa Chuo Kikuu cha Tumaini Dar es Salaam, aliendeleza vyema mchango wake katika elimu ya Tanzania. Hapa, uchungaji wake katika elimu ya Tanzania aliuweka katika msingi imara.”
Kwa wanaokumbuka, mwaka wa 2005, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ndilo lililokuwa linamiliki vyuo vikuu vingi kuliko taasisi yoyote ya dini. Ndilo pia lililokuwa na kundi kubwa la wanachuo kuliko taasisi nyingine za dini katika mwaka huo.
Huo wote ni mchango wa Profesa Mmari.
Mwanakwetu, upo? Kumbuka:
PROFESA MMARI: MCHUNGAJI MWEMA WA ELIMU YA TANZANIA
Nakutakia siku njema.
0717649257
.gif)














Post a Comment