Adeladius Makwega-MARA
Wanachuo kutoka Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, kilichopo wilayani Kwimba, mkoani Mwanza, walitembelea makazi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, yaliyopo Mwitongo, Butiama, mkoani Mara, Mei 26, 2023. Katika ziara hiyo, walipata fursa ya kusali kando ya kaburi lake na kutembelea maeneo mbalimbali ya makazi hayo ili kujifunza kuhusu maisha halisi ya kiongozi huyo aliyeongoza Tanzania kwa miaka 23, Mwanakwetu aliambatana nao.
Ziara hiyo ilichukua zaidi ya saa sita, ambapo wanachuo walitembelea maeneo mbalimbali ya makazi hayo, wakipiga picha, wakipata maelezo kuhusu historia ya Mwalimu Nyerere na kuuliza maswali yaliyojibiwa kwa kina na wasimamizi wa makazi hayo.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo, mkufunzi mwandamizi wa chuo hicho, Denis Kayombo, alisema kuwa kwa sehemu kubwa, wanachuo wake walikuwa wamejifunza kuhusu maisha ya Mwalimu Nyerere kupitia masomo ya Historia katika ngazi mbalimbali za elimu nchini. Hata hivyo, ziara ya Mwitongo iliwapa fursa ya kuona kwa vitendo baadhi ya mambo waliyokuwa wamejifunza darasani.
“Kubwa ni kuona baadhi ya kumbukumbu zilizohifadhiwa na kupata uhalisia wa maisha ya kiongozi wetu,” alisema Kayombo.
Wanachuo hao walielezwa kuwa Mwalimu Nyerere alipokuwa akifundisha katika Shule ya Sekondari ya Pugu, mojawapo ya masomo aliyofundisha lilikuwa Elimu ya Viungo na Michezo (Physical Education), somo ambalo pia ni sehemu ya mafunzo ya wanachuo hao. Aidha, Mwalimu Nyerere alifundisha somo la Biolojia na Historia.
Akifafanua uhusiano kati ya masomo hayo, mkufunzi Monika Kalonga, ambaye pia aliambatana na wanachuo hao, alisema kuwa watu wengi hushangazwa na jinsi Mwalimu Nyerere alivyoweza kufundisha masomo ambayo kwa mtazamo wa haraka yanaonekana kutofautiana.
“Watu wengi wanashangazwa ilikuwaje Mwalimu Nyerere alifundisha masomo ambayo ukiyaangalia hayaendani. Lakini sisi tunafahamu kuwa Elimu ya Viungo na Michezo ina uhusiano mkubwa na Elimu ya Viumbe Hai, hasa tunapozungumzia misuli na jinsi viungo vya binadamu vinavyofanya kazi,” alisema Kalonga.
Katika hatua za mwisho za ziara yao, wanachuo hao walitembelea makumbusho ya Baba wa Taifa, yaliyopo Butiama. Huko waliona vifaa mbalimbali vilivyotumiwa na Mwalimu Nyerere, vikiwamo mavazi, viatu, majembe, vigoda na zana nyingine.
Miongoni mwa vitu vilivyowavutia zaidi ni redio kubwa yenye uzito wa takribani kilogramu 20.
“Tumeambiwa Mwalimu Nyerere wakati wa ziara zake zote alikuwa akitembea na redio hiyo, ambayo alipewa huko Ujerumani, na alikuwa akiitumia kusikiliza taarifa mbalimbali za dunia. Kumbe Mwalimu Nyerere alikuwa mpenzi wa kufahamu ulimwengu unavyokwenda,” alisema Tabu Masele, mmoja wa wakufunzi wa chuo hicho na mratibu msaidizi wa ziara hiyo.
Kabla ya kuingia ndani ya makumbusho hayo, wanachuo walipiga picha ya pamoja. Kabla ya hapo, kulikuwa na kipindi cha maswali na majibu, ambapo maswali mbalimbali kuhusu maisha ya Baba wa Taifa yaliulizwa na kujibiwa.
Miongoni mwa waliohoji ni Tabu Masele, ambaye aliuliza kama Mwalimu Nyerere alikuwa na watoto wengine zaidi ya wale wanaotajwa katika historia yake.
Swali hilo, lililogusa maisha binafsi ya kiongozi huyo, lilijibiwa kwa maelezo kwamba Mwalimu Nyerere hakuwa na watoto wengine zaidi ya wale wanaofahamika. Pia, ilielezwa kuwa askari aliyefariki katika vita vya Uganda, ambaye wakati mwingine amekuwa akihusishwa na familia ya Nyerere, hakuwa mtoto wa Mwalimu Nyerere, bali alizaliwa katika kijiji jirani na Mwitongo.
Hata hivyo, maswali mengine yaliyoulizwa yalifungua mjadala kuhusu kipengele kingine cha maisha ya Mwalimu Nyerere ambacho kilionekana kuwashangaza wanachuo hao.
Katika maelezo yaliyotolewa na wasimamizi wa makazi hayo, wanachuo waliambiwa kuwa Mwalimu Nyerere alipokuwa mwanafunzi katika Shule ya Sekondari ya Tabora, familia moja ilimkabidhi mwanamke kwa matarajio ya kuwa mke wake. Hata hivyo, kwa mujibu wa maelezo hayo, Nyerere hakumuoa wala kuishi naye, lakini aliendelea kumtunza mwanamke huyo katika kipindi chote cha maisha yake.
Aidha, wanachuo hao walielezwa kuwa mwanamke pekee aliyemuoa na kuishi naye alikuwa Mama Maria Nyerere.
Maelezo hayo yaliibua maswali kadhaa, hasa kuhusu namna Mwalimu Nyerere alivyoweza kuendelea kumtunza mwanamke huyo kwa muda mrefu. Kwa mujibu wa maelezo waliyopata wanachuo hao, mwanamke huyo alikuwa bado hai wakati walipotembelea makazi ya Mwalimu Nyerere.
Mjadala huo uliendelea hata baada ya wanachuo kuingia ndani ya basi lao. Wakiwa safarini, baadhi yao walieleza kuwa walimchukulia Mwalimu Nyerere kama babu yao, hivyo waliona ni muhimu kufahamu zaidi maisha yake binafsi, mbali na historia yake kama kiongozi wa taifa.
Miongoni mwa maswali yaliyoibuka katika mjadala huo ni kuhusu nafasi ya mwanamke huyo katika historia ya familia ya Nyerere na sababu zilizofanya maisha yake binafsi yasifahamike sana kwa umma.
“Wanaume wengi wa Kiafrika ni hodari wa mitala. Kama Julius Nyerere alipewa mke na familia yake na akaendelea kumtunza mwanamke huyo hadi alipofariki dunia mwaka 1999, kwa nini mwanamke huyo asipewe nafasi ya kusikilizwa ili jamii ya Watanzania imfahamu na apate fursa ya kujibu maswali yanayoweza kuwepo kuhusu maisha yake?”
liliibuka swali katika mjadala huo ndani ya basi.
Hata hivyo, swali hilo halikupata jibu wakati huo, kwani wanachuo hao walikuwa tayari wanaendelea na safari yao kuelekea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Mjadala huo unaonyesha namna ziara katika maeneo ya kihistoria inavyoweza kuibua maswali mapya na kuchochea hamu ya kujifunza zaidi kuhusu maisha ya viongozi waliotoa mchango mkubwa katika historia ya taifa.
Siku nyingine Mwanakwetu akienda Butiama atamtafuta mama huyu.
Mwanakwetu, upo?
Kumbuka:
“Mwalimu Nyerere Akiwa Tabora Alipewa Mke.”
Nakutakia siku njema.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717649257




Post a Comment