
Adeladius Makwega na Tumaini Muungurumo
Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma
Karibu msomaji, msikilizaji na mtazamaji katika muhtasari wa habari za Jarida la Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Toleo Na. 02, Oktoba 2026.
Muhtasari huu unajumuisha habari zote zilizochapishwa katika jarida husika, kwa lugha rasmi, fupi na inayoeleweka. Lengo ni kuwafikia wasomaji, wasikilizaji na watazamaji, hususan wale ambao hawapati fursa ya kusoma jarida letu la maandishi.
Jarida letu la mwezi Oktoba 2026 limeangazia shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, pamoja na matukio muhimu ya kitaifa yanayohusu maendeleo, utendaji kazi, vijana na uhifadhi wa kumbukumbu. Katika matukio hayo, waandishi na maafisa habari wetu walikuwepo kuhakikisha wanatuletea taarifa hizo.
Tunaanza kwa kuangazia habari iliyofungua ukurasa wa jarida letu yenye kichwa kisemacho:
ERB YAPONGEZWA KWA KUKAMILISHA MWONGOZO WA KUHIFADHI NA KUTEKETEZA KUMBUKUMBU
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi, ameipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa kukamilisha na kusaini Mwongozo wa Kuhifadhi na Kuteketeza Kumbukumbu.
Mwongozo huo unalenga kuweka utaratibu rasmi wa kuhifadhi, kusimamia na kuteketeza kumbukumbu kwa kuzingatia sheria na taratibu zilizowekwa. Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sura ya 309.
Tukitoka katika shughuli za ERB jijini Dodoma, sasa tunasafiri hadi mkoani Rukwa, ambako tunakutana na habari ya:
MAKABIDHIANO YA MWENGE WA UHURU KATIKA KILELE CHA MBIO ZA MWENGE 2026
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2026, Bw. Wazo Mwang’onda, alimkabidhi Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratias Ndejembi, Mwenge wa Uhuru katika kilele cha mbio hizo kilichofanyika mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Mbio hizo zililenga kuimarisha umoja, mshikamano na uzalendo miongoni mwa Watanzania, pamoja na kuhamasisha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo ya taifa. Aidha, ziliendeleza mapambano dhidi ya rushwa, maradhi na ujinga.
Tukiwa bado mjini Sumbawanga, jarida letu lilimshuhudia Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, akivutiwa na ubunifu wa vijana.
WAZIRI MKUU AVUTIWA NA UBUNIFU WA VIJANA
Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba, amevutiwa na bunifu mbalimbali zilizobuniwa na vijana wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 yaliyofanyika mjini Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Katika maadhimisho hayo, alisisitiza umuhimu wa kuwawezesha vijana kupata mafunzo, mitaji na masoko ili waweze kuendeleza mawazo yao na kuyageuza kuwa miradi yenye tija.
Serikali imeendelea kuhamasisha vijana kutumia fursa zilizopo katika sekta za teknolojia, kilimo, biashara na nishati safi kwa lengo la kuongeza ajira, kipato na kuchangia maendeleo ya taifa.
Kutoka Sumbawanga, tunarejea tena jijini Dodoma, ambako tulipata habari inayosisitiza umuhimu wa mawasiliano na uwajibikaji katika utendaji kazi.
MAWASILIANO BORA, WELEDI NA UWAJIBIKAJI NGUZO ZA UTENDAJI IMARA
Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Bw. Firimin Msiangi, amewataka watumishi kuzingatia weledi, uwajibikaji na mawasiliano bora katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisisitiza kuwa watumishi wanapaswa kutoa taarifa zinazoonesha matokeo ya kazi zilizotekelezwa badala ya kueleza michakato pekee.
Aidha, alihimiza matumizi sahihi ya mifumo, taratibu na maelekezo ya Serikali ili kuongeza ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma.
Safari ya kukamilisha jarida hili ilikuwa ndefu, huku watayarishaji wake wakipata nafasi ya kufurahia burudani mbalimbali, zikiwemo mazungumzo na muziki wa nyumbani Tanzania.
Hata hivyo, inaonekana Sumbawanga ilikuwa na mambo mengi kiasi kwamba tulikaribia kusahau habari nyingine muhimu. Lakini hatuwezi kuiacha habari hii ipite bila kuizungumzia.
MKURUGENZI KYANDO ATEMBELEA MAONESHO YA WIKI YA VIJANA KITAIFA
Mkurugenzi wa Idara ya Waasisi wa Taifa, Bw. Salum Kyando, alitembelea mabanda ya maonesho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2026 yaliyofanyika katika Viwanja vya Shule ya Msingi Ndua, mjini Sumbawanga.
Ziara hiyo ililenga kujionea bunifu, bidhaa, teknolojia na shughuli mbalimbali zinazofanywa na vijana pamoja na taasisi zilizoshiriki katika maonesho hayo.
Maadhimisho hayo yalifanyika kuanzia Oktoba 8 hadi 14, 2026, chini ya kaulimbiu isemayo: “Mazingira Tofauti, Fursa Sawa kwa Vijana.”
Sasa jarida letu limerejea kikamilifu jijini Dodoma, ambako tunakutana na habari inayohusu huduma kwa wateja.
MHADHIRI WA CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM ASHIRIKI WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ilimpokea Mtafiti na Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bw. Mtechura Brighton, aliyefika kufanya utafiti kuhusu utamaduni na filamu nchini.
Mtafiti huyo alipokelewa na kuhudumiwa na Afisa Kumbukumbu, Bi. Leaclara Ngair.
Tukio hilo lilifanyika wakati wa Wiki ya Huduma kwa Wateja, ambayo inalenga kuhamasisha utoaji wa huduma bora zinazozingatia mahitaji ya wateja.
Makala yetu ya mwezi Oktoba haikuishia hapo. Pia imeangazia nyaraka muhimu ya kihistoria inayohusiana na Shirika la Utangazaji Tanzania, TBC.
NYARAKA YA MWEZI: HISTORIA YA ENEO LA MVUMI
Jarida limeangazia nyaraka ya kihistoria iliyokuwa hati ya maandalizi ya makala ya Shirika la Utangazaji Tanganyika (TBC), iliyoandaliwa na kurushwa hewani Septemba 10, 1961.
Makala hiyo ilihusu historia ya eneo la Mvumi, ambalo kwa sasa linapatikana katika Mkoa wa Dodoma.
Nyaraka hiyo inaonesha umuhimu wa kuhifadhi kumbukumbu za kihistoria kwa ajili ya kupata, kutunza na kuendeleza maarifa kuhusu historia ya taifa letu.
Tukiendelea na safari yetu ya kuangazia yaliyomo katika jarida hili, tunakutana na mada muhimu inayohusu usalama wa taarifa binafsi.
WAFANYAKAZI WAASWA KUWA MAKINI NA ULINZI WA TAARIFA BINAFSI
Wafanyakazi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa wamehimizwa kulinda taarifa zao binafsi ili kuepuka matumizi yasiyoruhusiwa.
Wito huo ulitolewa wakati wa mafunzo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yaliyofanyika jijini Dodoma.
Akizungumza katika mafunzo hayo, Afisa Utumishi Mkuu, Bi. Happiness Masija, alisisitiza umuhimu wa kutosambaza taarifa nyeti bila sababu za msingi. Pia alieleza umuhimu wa kupata ridhaa kabla ya kutumia picha au taarifa binafsi za watu wengine, hususan kwa madhumuni ya kibiashara.
Aidha, wafanyakazi wametakiwa kuwa waangalifu wanapotumia mitandao ya kijamii ili kuhakikisha wanazingatia usalama na faragha ya taarifa.
Mada hii iliwasilishwa na Afisa TEHAMA, Ndugu Ally Ally.
HITIMISHO
Kwa ujumla, Jarida la Oktoba 2026 limeonesha umuhimu wa kuimarisha usimamizi na uhifadhi wa kumbukumbu za Serikali, kuongeza uwajibikaji na weledi kwa watumishi, kulinda taarifa binafsi na kuboresha utoaji wa huduma kwa wateja.
Aidha, jarida limeonesha juhudi za Serikali katika kuwawezesha vijana kutumia bunifu na fursa zilizopo katika sekta mbalimbali kwa ajili ya maendeleo yao na taifa kwa ujumla.
Ujumbe mkuu unaojitokeza katika jarida hili ni kwamba utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka ni msingi muhimu wa utendaji wenye ufanisi, uwazi, uwajibikaji na ufanyaji wa maamuzi sahihi.
Wasomaji, wasikilizaji na watazamaji wetu, huo ndio ulikuwa muhtasari wa habari mbalimbali zilizomo katika Jarida la Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Toleo Na. 02, Oktoba 2026.
Jarida hili limetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
Kwa niaba ya mtayarishaji mwenzangu, Tumaini Muungurumo, mimi ni Adeladius Makwega.
Asanteni kwa kuwa nasi. Kwa heri!
Mawasiliano:
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com
Simu: 0717649257









Post a Comment