MTOTO WA MJINI ALIYEDHARAU USHAURI WA MAMA YAKE


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Katika mji mmoja uliokuwa na maduka mengi, barabara kubwa na nyumba zilizojengwa kwa matofali aliishi mtoto mmoja na mama yake. Mama yake alikuwa mfanyabiashara aliyekuwa akijitahidi kuhakikisha mtoto wake anapata mahitaji yote muhimu na elimu bora.

Mtoto huyo alisoma katika shule iliyokuwa katikati ya mji. Ingawa alikuwa na uwezo mzuri darasani, alikuwa na tabia ya ubishi na kupenda kufanya mambo kwa matakwa yake. Alipopewa ushauri aliona kama watu wanataka kumzuia kufurahia maisha.

Kila asubuhi mama yake alimkumbusha kuamka mapema kujiandaa kwenda shule na kuhakikisha amebeba vitabu vyake vyote. Lakini mtoto huyo hakupenda kuambiwa mambo yale yale kila siku. Mara nyingi alijibu kwa hasira na kudai kuwa alikuwa amekua na angeweza kujisimamia mwenyewe.

Siku moja mama yake alimwonya asitumie muda mwingi kucheza michezo ya simu kwa sababu alikuwa na mtihani wa mwisho wa muhula. Mtoto huyo alibishana naye na kusema kuwa angeweza kusoma usiku bila kupata shida yoyote.


Mama yake alijaribu kumweleza kuwa kujifunza kunahitaji muda na maandalizi lakini mtoto hakutaka kusikiliza. Alitumia muda mwingi kucheza kwenye simu na kutazama video huku akiahirisha masomo yake kila mara.

Siku ya mtihani ilipofika aliketi darasani akiwa na matumaini makubwa. Alipopewa karatasi ya maswali aligundua kuwa mengi yalihitaji maarifa ambayo hakuwa ameyasoma vizuri. Alijaribu kujibu kadiri alivyoweza lakini alishindwa kumaliza maswali yote.

Wiki iliyofuata matokeo yalipotangazwa aligundua kuwa alikuwa amepata alama za chini kuliko alivyotarajia. Wanafunzi wenzake walipokuwa wakizungumzia matokeo yao alijisikia vibaya na kuanza kujilaumu.

Alipofika nyumbani mama yake alimkuta akiwa kimya. Alipomuuliza kilichotokea mtoto alieleza kuhusu matokeo yake. Mama yake hakumcheka wala kumkaripia bali alikaa naye na kuzungumza naye kwa utulivu.

Alimweleza kuwa hakukuwa na ubaya katika kufanya makosa lakini ilikuwa muhimu kutambua sababu iliyomfanya ashindwe na kujifunza kutokana nayo. Alimkumbusha kuwa ushauri aliokuwa akimpa haukuwa wa kumzuia kufurahia maisha bali wa kumsaidia kupanga muda wake vizuri.


Mtoto huyo alitafakari maneno ya mama yake. Aligundua kuwa mara nyingi alikuwa akibishana bila kufikiria matokeo ya maamuzi yake.

Kuanzia siku hiyo alianza kupanga ratiba ya kusoma kupunguza muda wa kutumia simu na kufanya kazi za shule kwa wakati. Alipopewa ushauri alijifunza kusikiliza kwanza badala ya kujibu kwa hasira.

Mwanzoni ilikuwa vigumu kubadilika lakini aliendelea kujitahidi. Hatimaye alifanya vizuri zaidi katika mitihani iliyofuata na kuanza kuelewana vizuri na mama yake.

Mtoto huyo aligundua kuwa maisha ya mjini yalihitaji nidhamu uwajibikaji na uwezo wa kufanya maamuzi sahihi. Pia alielewa kuwa mtu anaweza kuwa na uhuru wa kufanya mambo yake bila kupuuza ushauri wa watu wanaomtakia mema.



emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments