MTOTO MKAIDI NA FIMBO YA BABA

 


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Hapo zamani za kale aliishi mzee mmoja na mwanawe wa pekee. Mzee huyo alikuwa mkulima mwenye bidii na aliyependa sana kumfundisha mwanawe tabia njema. Hata hivyo mwanawe alikuwa mtoto mbishi ambaye hakupenda kusikiliza ushauri wa mtu yeyote.

Kila baba yake alipomwambia afanye jambo mtoto huyo alibishana naye. Alipoambiwa aende kuchota maji alidai kuwa alikuwa na shughuli nyingine. Alipotakiwa kwenda shambani kusaidia kazi alijifanya kuwa amechoka. Hata alipoonywa kuhusu tabia yake alisisitiza kuwa yeye ndiye aliyejua mambo mengi kuliko wengine.

Siku moja baba yake alimwita na kumwambia waende shambani pamoja. Walipofika mzee huyo alimpa mwanawe jukumu la kuondoa magugu katika sehemu ndogo ya shamba.

Mtoto alikataa na kusema kuwa kazi hiyo ilikuwa ngumu sana kwake. Baba yake alimweleza kuwa kazi ilikuwa rahisi ikiwa angeianza mapema lakini mtoto hakutaka kusikia.

Mzee aliamua kutomlazimisha. Alimwacha mwanawe akae chini ya mti huku yeye akiendelea kufanya kazi.

Baada ya muda mtoto aliona baba yake akifanya kazi kwa bidii. Jua lilipozidi kuwa kali alianza kujuta kwa kukataa kusaidia. Hata hivyo kwa sababu ya kiburi chake hakutaka kumwomba baba yake msamaha.


Jioni waliporudi nyumbani baba yake alimwita tena. Safari hii alikuwa ameshika kifurushi cha vijiti vidogo.

Alimwomba mwanawe avunje kijiti kimoja. Mtoto alikivunja kwa urahisi. Kisha baba yake akamwomba avunje vijiti kadhaa vilivyofungwa pamoja. Mtoto alijitahidi kwa nguvu zake zote lakini hakufanikiwa.

Baba yake akamwambia “Mwanangu kijiti kimoja ni rahisi kuvunjika lakini vijiti vingi vinapounganishwa huwa vigumu kuvunja. Vivyo hivyo mtu anayekataa kusikiliza wengine hujikuta akishindwa katika mambo ambayo angeweza kuyatimiza kwa msaada wa wengine".

Mtoto alikaa kimya kwa muda. Alitambua kuwa tabia yake ya kubishana ilikuwa imemfanya akose nafasi nyingi za kujifunza na kusaidia familia yake.

Kuanzia siku hiyo alianza kubadilika. Alijifunza kusikiliza ushauri wa baba yake, kushiriki kazi za nyumbani na kuomba msamaha alipokosea.

Baada ya muda baba yake alifurahi kuona mwanawe akigeuka kuwa mtoto mwenye heshima, bidii na ushirikiano.

emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments