Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Katika mtaa mmoja jijini Mbeya aliishi mtoto wa miaka kumi na miwili aliyekuwa akitegemea mama yake kufanya karibu kila kitu kwa ajili yake. Mama yake ndiye aliyekuwa akimwandalia sare za shule, kupanga vitabu vyake na kumkumbusha kila hatua aliyopaswa kuchukua kabla ya kuondoka nyumbani.
Kwa sababu ya mazoea hayo mtoto huyo hakujifunza kujitegemea. Kila asubuhi alichelewa kujiandaa huku akimlaumu mama yake kwa kutomwamsha mapema au kutomtafutia soksi zake.
Siku moja mama yake aliugua na kushindwa kufanya shughuli zake za kawaida. Mtoto alilazimika kujiandaa mwenyewe kwenda shule. Alishindwa kupata sare yake akasahau daftari la somo la kwanza na kuchelewa kufika shuleni.
Aliporudi nyumbani alikuta mama yake bado hajisikii vizuri. Kwa mara ya kwanza alitambua kuwa mama yake hakuwa na nguvu za kufanya kila kitu kwa niaba yake.
Siku zilizofuata alianza kujifunza kupanga sare zake usiku, kuweka vitabu kwenye begi na kuamka kwa wakati. Pia alianza kusaidia kazi ndogo za nyumbani bila kusubiri kukumbushwa.
Baada ya mama yake kupona alishangaa kuona mabadiliko hayo. Mtoto alimweleza kuwa alikuwa amegundua umuhimu wa kujifunza kufanya mambo yanayolingana na umri wake.
Tangu wakati huo aliendelea kujitegemea na kuwajibika zaidi. Alielewa kuwa msaada wa wazazi ni muhimu lakini kila mtoto anapaswa kujifunza hatua kwa hatua kutekeleza majukumu yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment