MTAFITI ACHIMBA HISTORIA YA MAPAMBANO DHIDI YA MALARIA KUPITIA NYARAKA ZA TAIFA

 

Adeladius Makwega

Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Dodoma

 

DODOMA, Ijumaa, Oktoba 16, 2026. Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, imemhudumia mtafiti Mtechura Brighton Winghton, ambaye pia ni Mhadhiri Msaidizi katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, aliyefika katika ofisi hiyo kwa ajili ya kukusanya nyaraka zinazohusu historia ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa malaria nchini Tanzania.

 

Akielezea kuhusu huduma iliyotolewa kwa mtafiti huyo, afisa wa Idara hiyo, Bi. Ngairo, alisema mtafiti huyo ni mmoja wa wadau wanaotumia nyaraka za taifa katika kukamilisha tafiti zao.

 

“Huyu ni mdau wetu. Leo ameomba mafaili kadhaa yanayohusu ugonjwa wa malaria na namna Watanzania walivyokuwa wakipambana na ugonjwa huu tangu kabla ya uhuru. Miongoni mwa nyaraka tulizozikumbuka ni zile zilizomo katika faili la Waziri Mkuu lenye kichwa ‘MALARIA: Notes on Its Cause, Prevention and Cure’, la mwaka 1952, lililotolewa na Mkurugenzi wa Huduma za Afya wa Tanganyika,” alisema Bi. Ngairo.

Akizungumza akiwa katika shughuli ya kupitia kurasa za mafaili ya kihistoria, Winghton alisema ameridhishwa na ushirikiano anaoupata kutoka katika taasisi hiyo na kwamba utafiti wake unaendelea vizuri.



“Ninashukuru kwa kupata fursa ya kusoma mafaili kadhaa, na kazi hii inaendelea vizuri. Utafiti wetu umejikita katika ugonjwa wa malaria maeneo ya Ifakara, Morogoro, na Malale, Tinde, Shinyanga. Pia, ninatembelea taasisi mbalimbali kukusanya taarifa zaidi kuhusu namna ndugu zetu walivyopambana na magonjwa hayo kwa kutumia rasilimali chache walizokuwa nazo,” alisema.

Aidha, mtafiti huyo aliishukuru Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kwa ushirikiano ambao amekuwa akiupata kila anapofika katika taasisi hiyo. Hata hivyo, alieleza kuwa bado anatafuta nyaraka muhimu zinazohusu historia ya Taasisi ya Utafiti wa Malaria ya Ifakara.

 

“Nimeomba hotuba ya Mwalimu Julius Nyerere aliyoitoa Oktoba 18, 1973, wakati wa uzinduzi wa Taasisi ya Malaria ya Ifakara. Mhadhiri mwenzangu alipokuwa nje ya nchi alipata video inayoonyesha Mwalimu Nyerere akitembelea taasisi hiyo, lakini hotuba aliyotoa siku hiyo bado hatujaipata. Tunaendelea kuitafuta,” alisema Winghton.

 

Kwa upande wao, maafisa wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma, wakiongozwa na Bi. Ngairo, walilipokea ombi hilo na kueleza kuwa tayari wameanza kutafuta hotuba hiyo ili kumsaidia mtafiti huyo katika kukamilisha utafiti wake.

 

Winghton ni miongoni mwa watafiti wanaotembelea taasisi hii ya umma kwa ajili ya kupata taarifa na nyaraka mbalimbali zinazowasaidia kukamilisha tafiti zao.


makwadeladius@gmail.com 0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments