Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Ilipofika saa mbili asubuhi wanafunzi walikuwa wameingia madarasani kuanza masomo kama kawaida. Lakini Hamisi mwanafunzi wa darasa la sita alikuwa akitembea mitaani na marafiki zake badala ya kuwa shuleni. Kwa wiki kadhaa, alikuwa amekuwa akitoroka masomo bila wazazi wake kujua.
Mwanzoni Hamisi alitoroka siku ambazo hakumaliza kazi za nyumbani kwa sababu aliogopa kukemewa na mwalimu. Baadaye alianza kutoroka hata siku ambazo hakukuwa na kazi. Alivutiwa na uhuru alioupata akiwa nje ya shule bila kutambua kuwa alikuwa akiharibu maisha yake ya baadaye.
Siku moja mwalimu wake alipowaita wanafunzi kufanya mtihani wa ghafla Hamisi hakuwepo darasani. Alikuwa amekwenda kucheza mpira na marafiki zake katika uwanja uliokuwa karibu na shule.
Aliporudi nyumbani jioni baba yake alimwuliza kuhusu masomo. Hamisi alijibu kuwa siku hiyo walikuwa wamepewa muda wa kujisomea. Hata hivyo siku chache baadaye baba yake aliitwa shuleni na kuambiwa kuwa mwanawe alikuwa amekosa masomo mara nyingi.
Alipofika nyumbani Hamisi aliogopa kuadhibiwanlakini baba yake aliamua kuzungumza naye kwanza. Alimuuliza kwa nini alikuwa akitoroka shule na baada ya muda Hamisi alikiri kuwa alikuwa amepoteza hamu ya kusoma kwa sababu aliona masomo fulani kuwa magumu.
Baba yake alimweleza kuwa kukimbia tatizo hakulifanyi litoweke. Badala yake alimshauri amwambie mwalimu kila anaposhindwa kuelewa somo ili apate msaada.
Hamisi alianza kuhudhuria masomo kwa uaminifu na kuomba msaada pale alipokwama. Taratibu alianza kuelewa masomo yaliyokuwa yakimpa shida na kurudisha nidhamu yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment