JAJI MKUU, NAOMBA UPOKEE MAWAZO YANGU

 

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Tarehe 5 Oktoba 2026, nilisoma habari iliyochapishwa na Mahakama ya Tanzania, iliyoandikwa na Eleotherius Ponera, kuhusu kikao maalumu cha Mahakama ya Rufani kinachotarajiwa kufanyika Iringa. Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari: “Mahakama ya Rufani Kusikiliza Mashauri 59 Iringa.”

 

Kwa ufupi, habari hiyo ilieleza:

 

“Mahakama ya Rufani inatarajia kusikiliza mashauri 59 katika kikao maalumu kitakachofanyika Mahakama Kuu Iringa kuanzia Oktoba 5 hadi 30, 2026. Mashauri hayo yanajumuisha rufaa 24 za jinai, rufaa 12 za madai, ombi moja la jinai na maombi 22 ya madai.

Kikao hicho kitahusisha Majaji wanne, ambao ni Mhe. Jacobs Mwambegele, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo, Mhe. Leila Mgonya na Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim. Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Majaji watatu watakuwa katika jopo, huku Jaji mmoja akiwa katika chemba. Majaji wote wanne watakuwa wakibadilishana majukumu kulingana na orodha ya mashauri.”

 

Kwa hakika, kazi ya Mahakama ya Tanzania ya kusikiliza na kuamua mashauri inaendelea. Hata hivyo, baada ya kusoma habari hiyo, nilijikuta nikiwa na maswali mengi, hasa kuhusu mpangilio wa majukumu ya Majaji waliotajwa.

 

Jambo lililonifanya nitafakari zaidi ni jukumu la Mhe. Jacobs Mwambegele kuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo.

Nilijiuliza kwa nini jukumu hilo limekabidhiwa kwake badala ya Jaji mwingine kati ya wale waliotajwa? Maswali yangu haya yanatokana na wasiwasi wangu kuhusu umuhimu wa kulinda imani ya wananchi katika Mahakama ya Tanzania, hususan Mahakama ya Rufani.

 

Mashauri 59 si idadi ndogo. Kila shauri linaweza kuwa na umuhimu mkubwa kwa wahusika wake, na maamuzi yanayotolewa na mahakama yana nafasi muhimu katika kulinda haki na kuimarisha imani ya wananchi katika mfumo wa utoaji haki.

 

Kwa sababu hiyo, niliona ni muhimu kutafakari kwa kina kuhusu upangaji wa majukumu katika kikao hicho.

 

Katika mtazamo wangu, huenda jukumu la kuongoza jopo hilo lingeweza kukabidhiwa kwa Jaji mwingine kati ya waliotajwa. Hata hivyo, natambua kwamba upangaji wa majukumu ya Majaji ni suala linalopaswa kuzingatia taratibu na vigezo vinavyotumika katika Mahakama.

 

Nilipoendelea kutafakari, nilirejea sehemu ya habari hiyo iliyonipa matumaini kidogo. Afisa wa Mahakama, Mhe. Dianess Lyimo, alieleza kuwa Majaji wote wanne watakuwa wakibadilishana majukumu kulingana na orodha ya mashauri.

 

Kauli hiyo ilinifanya nijiulize ikiwa utaratibu huo utatoa nafasi kwa Majaji wote kushiriki katika majukumu mbalimbali ya kikao hicho kwa namna inayozingatia taratibu za mahakama.

 

Katika tafakari yangu, nilianza kujiuliza kuhusu nafasi ya Mhe. Jacobs Mwambegele katika majukumu haya, nikitumia mfano wa kibiblia wa Yakobo mwana wa Zebedayo, ambaye alikuwa ndugu wa Mtume Yohana na mmoja wa mitume wa Yesu Kristo.

 

Nilijiuliza: Je, Jaji Mwambegele anaweza kutekeleza majukumu yake kwa uhuru, utulivu na kujiamini, huku akizingatia wajibu wake wa kisheria na kimaadili katika mazingira ya sasa ya utoaji haki nchini?

 

Swali hili lilinifanya nitafakari pia kuhusu Majaji wengine waliotajwa katika habari hiyo.

 

Kwa mtazamo wangu, Mhe. Dkt. Paul Kihwelo na Mhe. Leila Mgonya sina mashaka nao natambua majukumu yao ya kutekeleza kwa kuzingatia sheria na maadili ya mahakama.

 

Kuhusu Mhe. Ibrahim Mzee Ibrahim, ambaye binafsi simfahamu kwa undani, ninaamini kuwa naye anapaswa kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi hiyo hiyo ya haki na uwajibikaji.

 

Hata hivyo, msimamo wangu si kwamba Jaji yeyote anapaswa kuhukumiwa kwa jina, historia yake au hisia za mtu binafsi. Ninachotamani ni kuona kila Jaji akifanya kazi katika mazingira yanayomwezesha kutekeleza wajibu wake kwa uhuru, uadilifu na kujiamini, kwa kuzingatia sheria.

 

Ninapotumia mfano wa mti unaohitaji kumwagiliwa na kutunzwa ili ukue vizuri, ninamaanisha kuwa taasisi yoyote inahitaji mazingira bora ili iweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo. Kwa mantiki hiyo, ninadhani ni muhimu kwa Mahakama kuhakikisha kuwa majukumu yanapangwa kwa kuzingatia maslahi ya haki na imani ya wananchi kwa kila jaji.

Pamoja na hayo, suala la umri wa Jaji, muda wake wa utumishi au uwezekano wa kustaafu, mashaka ya jamii linapaswa kujadiliwa kwa kuzingatia taarifa sahihi na taratibu zinazotumika katika mahakama yetu huku mahakama ipime mawazo ya jamii juu ya kila jaji na wajibu wake kwa kila kazi anayoifanya iwe ndani ya kuta za mahakama au nje.

Iwapo kuna hoja kuhusu namna majukumu yanavyopangwa au mazingira ya utendaji wa Jaji, naamini ni muhimu hoja hizo zikafanyiwa tathmini kwa kuzingatia ushahidi, sheria na taratibu husika.

 

Ombi langu kwa Jaji Mkuu na

msomaji wangu, haya ni mawazo yangu kuhusu Mahakama ya Tanzania, hususan Mahakama ya Rufani. Nimeamua kuyaandika baada ya kusoma taarifa kuhusu kikao maalumu cha kusikiliza mashauri 59 mjini Iringa.

 

Ninapenda kusisitiza kuwa lengo langu ni kutoa maoni yangu kuhusu namna ya kuimarisha taasisi hii muhimu katika nchi yetu. Mahakama ni nguzo muhimu katika kulinda haki za wananchi, na imani ya umma katika taasisi hiyo ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele.

Kwa hiyo, kwa heshima kubwa, namwomba Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ayapokee mawazo haya na, kwa kadiri atakavyoona inafaa, ayafanyie tathmini pamoja na washauri wake.

Ninatamani kuona Mahakama ya Tanzania ikiendelea kuimarika, ikitekeleza majukumu yake kwa uhuru, uadilifu, uwazi na weledi, ili wananchi waendelee kuwa na imani nayo,lakini makala haya ni wajibu wa kila hakimu au jaji kila analolifanya iwe nje mahakama au mahakamani mjitahidi liwe na maswali yanayojibika

Jaji Mkuu, naomba upokee mawazo yangu. Lengo langu ni kuona Mahakama ya Tanzania inazidi kusimama imara katika kulinda haki na kuimarisha utawala wa sheria nchini.

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com 0717649257

 








0/Post a Comment/Comments