ERB Yapongezwa kwa Kukamilisha Mwongozo wa Kuhifadhi na Kuteketeza Kumbukumbu

 

 

 Adeladius Makwega


Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa – Dodoma.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ndugu Firimin Msiangi, ameipongeza Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) kwa kufanikisha maandalizi na kukamilisha Mwongozo wa Kuhifadhi na Kuteketeza Kumbukumbu, hatua iliyofikia kilele kwa utiaji saini wa mwongozo huo Oktoba 15, 2026 Jijini Dodoma.

 

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini, Msiangi alisema ERB ni miongoni mwa taasisi zilizotekeleza utaratibu huo, na kuipongeza bodi hiyo kwa hatua hiyo muhimu.

 

“Nyinyi ni taasisi ya pili iliyotekeleza taratibu hizi kwa kutia saini pamoja hadharani. Hongereni sana Bodi ya Usajili wa Wahandisi,” alisema Msiangi.

 

Hafla hiyo ilihusisha pande mbili, ambazo ni Bodi ya Usajili wa Wahandisi na Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ambayo ina jukumu la kusimamia na kuratibu taratibu za usimamizi wa kumbukumbu katika taasisi za umma na hata zile binafsi inapobidi.

Akifafanua umuhimu wa zoezi hilo, Msiangi alisema kuwa utayarishaji wa mwongozo wa kuhifadhi na kuteketeza kumbukumbu ni takwa la kisheria linalolenga kuhakikisha nyaraka za Serikali zinasimamiwa kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

 

Alisema hatua hiyo ni muhimu katika kuzuia nyaraka za Serikali kutumika au kuonekana katika maeneo yasiyostahili, ikiwemo madukani zikiwa zimefungashia bidhaa, jambo ambalo linaweza kushusha hadhi na heshima ya taasisi za umma.

 

Alifafanua kuwa Sheria ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa (Records and Archives Management Act, Cap. 309, R.E. 2023) inaweka wajibu wa kisheria kwa taasisi za umma kuhakikisha kumbukumbu zinasimamiwa na kulindwa ipasavyo.

 

Kwa mujibu wa maelezo yake, Kifungu cha 9 cha sheria hiyo kinaweka wajibu kwa wakuu wa taasisi za umma kuhakikisha kumbukumbu zinalindwa na kusimamiwa ipasavyo, pamoja na kuandaa ratiba za uhifadhi na uteketezaji kwa msaada wa Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.

 

Aidha, Kifungu cha 11 kinaweka masharti kuhusu uratibu na makubaliano ya ratiba za uhifadhi na uteketezaji wa kumbukumbu, kuwasilishwa kwa ajili ya kupata idhini inayotakiwa na usimamizi wa utekelezaji wake kwa mujibu wa sheria.

Akihitimisha maelezo yake, Ndugu Msiangi alisisitiza kuwa mchakato wa kuteketeza kumbukumbu hufuata utaratibu maalumu unaohakikisha kila nyaraka inayokusudiwa kuteketezwa inaorodheshwa na mchakato mzima unasimamiwa na wataalamu husika.

 

Alisema utaratibu huo ni muhimu kwa kuwa unatoa uthibitisho kuwa nyaraka husika zimeteketezwa kwa kufuata taratibu za kisheria, hivyo kuweka kumbukumbu sahihi za mchakato huo endapo kutatokea uhitaji wa taarifa kuhusu nyaraka zilizoteketezwa.

Kwa upande wake, Mhandisi Bernad Kavishe aliishukuru Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kwa kutoa mwongozo na ushirikiano katika hatua zote za mchakato huo hadi kukamilika kwa utiaji saini.

 

“Ninaishukuru Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kwa kutuongoza katika hatua zote tangu mwanzo hadi leo tulipokamilisha mchakato huu. Tunaahidi kuzingatia yote tuliyokubaliana,” alisema Kavishe.

 

Utiaji saini wa Mwongozo wa Kuhifadhi na Kuteketeza Kumbukumbu wa Bodi ya Usajili wa Wahandisi (ERB) ni hatua muhimu katika utekelezaji wa wajibu wa kisheria wa taasisi za umma wa kusimamia kumbukumbu zao kwa kuzingatia Sheria ya Usimamizi wa Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Sura ya 309.

 

Mwongozo huo unalenga kuweka utaratibu rasmi wa kuhifadhi, kusimamia na kuteketeza kumbukumbu kwa kuzingatia matakwa ya sheria, huku ukilinda usalama wa nyaraka na kuimarisha uwajibikaji katika usimamizi wa kumbukumbu za taasisi za umma.

makwadeladius@gmail.com 0717649257









 











 

 

0/Post a Comment/Comments