Na: Adeladius Makwega
Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma
Dodoma, Oktoba 13, 2026
Kuna watu ambao wanapopita duniani huacha pengo kubwa, lakini pia huacha alama zisizofutika katika maisha ya watu na maendeleo ya taifa. Miongoni mwao ni Profesa Geoffrey Mmari, msomi na mtaalamu wa elimu ambaye mchango wake katika sekta ya elimu nchini Tanzania unastahili kukumbukwa na kuenziwa.
Kifo chake ni pigo kwa familia yake, jumuiya ya wasomi, walimu, wanafunzi na taifa kwa ujumla.
Hata hivyo, mawazo yake, maandiko yake na mchango wake katika maendeleo ya elimu vitaendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya elimu nchini.
Kwa kutambua umuhimu wa mchango wa Profesa Mmari, Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ilifanya kazi ya kupitia rejea mbalimbali zilizohifadhiwa katika maghala yake ya kumbukumbu jijini Dodoma na Dar es Salaam kwa muda wa siku mbili, kwa lengo la kupata taarifa zaidi kuhusu maisha na mchango wa msomi huyu.
Kazi hiyo ilifanywa na maafisa wawili, ndugu Ali Athumani Litongelele, mpiga chapa kutoka Dar es Salaam, na Bi. Neema Milinga, mkutubi kutoka mkoani Shinyanga. Ingawa msako huo haukuzaa matunda kwa ndugu Litongelele, jitihada za Bi. Milinga zilizaa matunda yaliyowezesha kupatikana kwa makala muhimu iliyoandikwa na Profesa Mmari.
Kwa hakika katika kazi hii Wamakonde walishindwa kufua dafu kwa Wasukuma, huku Mpogolo akiwa refarii.
Bi Milinga kwa heshima na taadhima alikuja na makala yenye kichwa cha habari “Miaka Kumi ya Hesabu Mpya 1962–1972”, iliyochapishwa katika jarida la The Tanzania Education Journal, Na. 3, Juzuu ya 2, mwaka 1973.
Kwa hakika upatikanaji wa makala hii ni ukumbusho wa thamani ya nyaraka za kihistoria katika kuhifadhi fikra, maarifa na mchango wa watu waliochangia maendeleo ya taifa letu.
Katika makala hii, Profesa Mmari anaeleza historia na maendeleo ya ufundishaji wa Hesabu Mpya nchini Tanzania kuanzia mwaka 1962 hadi 1972. Anaangazia sababu zilizochochea kuanzishwa kwa mbinu hizo mpya za ufundishaji, ikiwemo mabadiliko ya sayansi na teknolojia duniani pamoja na haja ya kuimarisha elimu ya hisabati ili iendane na mahitaji ya wakati huo. Aidha, makala inaeleza changamoto zilizojitokeza wakati wa utekelezaji wa mpango huo, zikiwemo upungufu wa vitabu, maandalizi ya walimu na umuhimu wa kuwajengea walimu uwezo wa kutumia mbinu mpya za kufundishia.
Licha ya changamoto hizo, juhudi mbalimbali zilifanyika kupitia mafunzo, semina na ushirikiano wa taasisi zinazohusika na elimu. Haya yanaonesha kuwa mageuzi ya elimu yanahitaji mipango madhubuti, walimu wenye ujuzi, vitabu na vifaa vya kutosha, pamoja na ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Kwa maana hiyo, maandishi ya Profesa Mmari si kumbukumbu ya yaliyopita pekee, bali pia ni rejea inayoweza kuwasaidia wataalamu wa elimu kutafakari mafanikio, changamoto na mwelekeo wa maendeleo ya elimu nchini.
Mchango wa Profesa Mmari unatukumbusha kuwa maendeleo ya elimu hayawezi kutenganishwa na utafiti, ubunifu, uhifadhi wa maarifa na maandishi yenye manufaa kwa vizazi vijavyo. Kazi aliyoiacha inatupa fursa ya kutazama tulikotoka, kutathmini tulipo na kutafakari tunakotaka kwenda katika safari ya kuboresha elimu ya Tanzania.
Katika kipindi hiki cha maombolezo, kupatikana kwa makala yake ya mwaka 1973 kunatupa sababu nyingine ya kuenzi urithi wake. Ni ushahidi wa namna kumbukumbu za taifa zinavyoweza kuunganisha vizazi vya sasa na historia ya waliotangulia, huku zikihifadhi maarifa ambayo yangepotea iwapo yasingetunzwa kwa uangalifu.
Kwa heshima ya marehemu Profesa Geoffrey Mmari, makala yake inaambatanishwa ili wasomaji wapate fursa ya kufahamu mawazo yake na kutafakari mchango wake katika elimu ya Tanzania. Hatua hii pia inasisitiza umuhimu wa kuhifadhi na kuendeleza nyaraka za kihistoria kama hazina ya maarifa kwa watafiti, walimu, wanafunzi na wananchi kwa ujumla.
Katika wakati huu wa huzuni, Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, inatoa pole za dhati kwa familia ya marehemu Profesa Geoffrey Mmari, ndugu, jamaa, marafiki, wanafunzi wake na wote walioguswa na msiba huu. Tunawaombea faraja, nguvu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu.
Buriani, buriani Profesa Geoffrey Mmari. Umeondoka kimwili, lakini mchango wako, maandishi yako na alama uliyoiacha katika historia ya elimu vitaendelea kukumbukwa. Urithi wako utaendelea kuzungumza kupitia maarifa uliyoyaandika na kumbukumbu ulizoziacha kwa taifa.
“Bwana alitoa, na Bwana ametwaa; jina la Bwana lihimidiwe.” (Ayubu 1:21)
Amina.
Barua pepe: makwadeladius@gmail.comSimu: 0717649257
.gif)







Post a Comment