Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Karatasi ya mtihani ilipofika kwenye dawati lake mtoto huyo aliitazama kwa muda bila kuifungua.
Alikuwa amezoea kupata alama za chini katika somo hilo. Kila alipofanya mtihani aliingia darasani akiwa na hofu kwamba angeona tena namba ndogo juu ya karatasi yake.
Alipofungua, aliona amepata alama 42 kati ya 100.
Alijisikia vibaya lakini safari hii hakumlaumu mwalimu wala kusema somo lilikuwa gumu. Alitazama majibu yake na kugundua kuwa makosa mengi aliyafanya kwenye maswali aliyokuwa amepewa nafasi ya kujifunza.
Jioni hiyo alirudi nyumbani na kuanza kupitia mada moja baada ya nyingine. Hakusoma kwa muda mrefu sana alijifunza kwa dakika chache kila siku.
Alipoelewa sehemu aliyokuwa akikosea alianza kumuuliza mwalimu maswali darasani. Wakati mwingine alisoma na rafiki yake aliyekuwa akimudu somo hilo vizuri.
Mtihani uliofuata uliporudishwa alama yake ilikuwa 68.
Haikuwa alama ya juu zaidi darasani lakini kwake ilikuwa ushindi mkubwa.
Aliangalia karatasi ile na kutabasamu. Aligundua kwamba wakati mwingine kushindwa si mwisho wa safari. Kunaweza kuwa mwanzo wa kujua unahitaji kubadilisha nini.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872


Post a Comment