.gif)
Adeladius Makwega – Ofisi ya Rais –Idara ya Kumbukumu na Nyaraka za Taifa.
“Maktaba ni nini, na kuna aina ngapi za maktaba?”
Swali hili lilizua mjadala mzito katika Septemba Mosi, 2026, katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka.
Miongoni mwa watumishi waliokuwa wakijadili suala hilo alikuwa ndugu Daudi Hokororo, mkutubi kijana kuliko wote waliokuwapo katika kikao fulani.Akiwa amevalia miwani yake maridadi, Hokororo alisimama na kuanza kueleza kwa utulivu:
“Maktaba ni neno la Kiswahili linalotokana na neno la Kiarabu maktab. Katika matumizi ya Kiswahili, neno hili limejengeka kuwa na maana pana zaidi ya eneo au sehemu ya kuhifadhia maarifa.”
Alieleza kuwa kwa maana ya kawaida, maktaba ni jengo, chumba au eneo maalumu linalohifadhi mkusanyiko wa vitabu, magazeti, majarida, nyaraka na machapisho mengine kwa ajili ya kujisomea, kufanya utafiti na kujipatia maarifa.
“Kusudi kuu la maktaba ni kutoa elimu, kukuza hamu ya kusoma na kuhifadhi kumbukumbu pamoja na machapisho mbalimbali kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho,” aliongeza.
Kisha Hokororo akaanza kuzitaja aina mbalimbali za maktaba.
Maktaba za Kitaluma (Shule na Vyuo)
Hizi ni maktaba zinazopatikana katika shule, vyuo na taasisi nyingine za elimu. Huduma zake hulenga zaidi wanafunzi, walimu, wahadhiri na watafiti.
Ni sehemu muhimu kwa kuongeza maarifa nje ya yale yanayopatikana darasani.
Maktaba za Taifa au Umma
Hizi ni maktaba zinazotoa huduma kwa wananchi kwa ujumla mfano Maktaba Kuu ya Taifa TLSB).
Mtu yeyote anayehitaji kusoma, kutafuta taarifa au kufanya utafiti anaweza kunufaika na huduma zinazotolewa na maktaba za aina hii, kulingana na taratibu za maktaba husika.
Maktaba Binafsi
Hii inaweza kuwa chumba, sehemu au mkusanyiko wa vitabu unaomilikiwa na mtu binafsi au familia, kwa matumizi yao ya nyumbani.
Maktaba ya aina hii humsaidia mtu kujenga utamaduni wa kusoma na kuwa na chanzo chake cha maarifa.
Maktaba ya Kidijitali
Hii ni maktaba inayowezesha upatikanaji wa vitabu, nyaraka, machapisho na taarifa kwa njia ya kidijitali, mara nyingi kupitia kompyuta, simu au mtandao.
Kwa maendeleo ya teknolojia, mtu anaweza kupata maarifa mengi bila kulazimika kwenda kwenye jengo la maktaba. Hii huwezeshwa kupitia mifumo ya maktaba kama vile Koha library na Dspace
Baada ya maelezo hayo mjadala ulitulia kwa muda.
Kila mmoja alikuwa akitafakari umuhimu wa maktaba katika maisha ya kila siku. Ilionekana wazi kwamba maktaba si mahali pa vitabu pekee, bali ni hazina ya maarifa, kumbukumbu, Rejea na elimu inayoweza kumjenga mtu na jamii kwa ujumla.
Hayo ndiyo yaliyokuwa maelezo ya ndugu Daudi Hokororo, mkutubi kutoka Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka, ambaye siku hiyo alikuwa miongoni mwa watumishi walioshiriki katika mjadala kuhusu mifumo na aina mbalimbali za maktaba.
Na kwa kuwa wewe, msomaji wangu, ulikuwa hujui baadhi ya aina hizi za maktaba, naamini sasa umeanza kupata picha pana zaidi.
Mwanakwetu, upo?
Kumbuka:
ZIJUE AINA ZA MAKTABA
Kwa sababu katika ulimwengu wa maarifa, maktaba ni daraja linalotuunganisha na elimu, historia na hazina ya fikra za wanadamu.
Nakutakia siku njema.
📞 0717649257














.gif)
Post a Comment