Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Neema alikuwa msichana wa miaka tisa aliyeishi na mama yake mjini. Siku yake ya kuzaliwa ilikuwa imekaribia na alitamani sana kuwa na keki nzuri kama alizokuwa akiziona kwenye mitandao ya kijamii.
Wiki moja kabla ya siku hiyo mama yake alimweleza kwa upole "Neema mwaka huu hatutaweza kununua keki kubwa kwa sababu tunatumia fedha kulipa ada ya shule na mahitaji mengine"
Mwanzoni Neema alihuzunika. Lakini alipotafakari aligundua kuwa elimu yake ilikuwa muhimu zaidi.
Siku ya kuzaliwa ilipofika Neema na mama yake walioka keki ndogo nyumbani kwa kutumia unga, mayai na sukari walizokuwa nazo. Waliipamba kwa matunda na kuandika juu yake "Heri ya Kuzaliwa Neema!"
Jioni marafiki wachache walifika nyumbani. Waliimba nyimbo za kuzaliwa, wakacheka na kucheza michezo. Kila mmoja aliondoka akiwa na tabasamu.
Usiku huo Neema alimkumbatia mama yake na kusema "Asante mama. Leo nimegundua kuwa furaha haitokani na ukubwa wa keki bali na upendo wa familia na marafiki"
Mama yake alitabasamu na kumwambia "Huo ndiyo zawadi kubwa kuliko zote".


Post a Comment