WAAJIRI LIPENI STAHIKI ZA WATUMISHI

 

 

 Adeladius Makwega


Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma

 

DODOMA — Serikali imewataka wakuu wa taasisi zote za umma nchini kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kulipa gharama za uhamisho na stahiki nyingine za watumishi wanaohamishwa au kuhamia vituo vipya vya kazi.

 

Hatua hiyo, imeelezwa, itasaidia kupunguza malalamiko miongoni mwa watumishi na kuongeza ufanisi pamoja na tija katika utumishi wa umma.

 

Kauli hiyo imetolewa na Waziri mwenye dhamana ya Utumishi wa Umma, Mhe. Ridhwani Kikwete, aliyemwakilisha Waziri Mkuu, Mhe. Mwigulu Nchemba, wakati wa uzinduzi wa Mkutano Mkuu wa 14 wa Chama cha Menejimenti cha Watunzaji wa Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), unaofanyika jijini Dodoma.

 

Katika hotuba yake, Mhe. Kikwete pia alitoa shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuchangia ujenzi wa jengo la Ofisi ya TRAMPA Makao Makuu jijini Dodoma.

Aidha, Waziri Kikwete alisisitiza umuhimu wa kuendelea kuboresha mifumo ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka kwa kuendana na maendeleo ya teknolojia ya kisasa.

 

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devota Mrope, aliishukuru Serikali kwa kuendelea kushirikiana na chama hicho na kuwa karibu nacho katika utekelezaji wa majukumu yake.

 

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Seleimani Mkomi, alisema wizara hiyo ndiyo mlezi wa TRAMPA.

Akizungumza wakati wa kuwatambulisha baadhi ya wadau katika mkutano huo, Mkomi alisema:

 

“Kumbukumbu na nyaraka zinazotajwa kwa sehemu kubwa zipo chini ya mamlaka yetu. Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ndiyo msimamizi wa eneo hili, na idara hiyo inaongozwa na ndugu Frimin Msiangi.”

 

Mkutano huo wa 14 wa TRAMPA umewakutanisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Zanzibar, huku zaidi ya washiriki 1,000 wakihudhuria.

Miongoni mwa washiriki hao ni Bi. Latifa Kibadeni, Mtunzaji wa Kumbukumbu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ambaye amesema amefurahia kushiriki mkutano huo.

 

“Nimefurahi kushiriki Mkutano huu wa 14. Kila mara nimekuwa mdau wa TRAMPA. Tangu nilipoanza kuwa mtumishi wa umma nimekuwa nikishiriki shughuli zake, na huu ni mkutano wangu wa sita. Namshukuru Katibu Tawala Mkoa wa Mbeya kwa mara kwa mara kuniwezesha kushiriki,” alisema.

 

Naye Izack Aloyce, Mtunzaji wa Kumbukumbu kutoka Halmashauri ya Jiji la Mbeya, amesema huo ulikuwa mkutano wake wa kwanza wa TRAMPA tangu alipoajiriwa mwaka 2024.

 

“Nashukuru Mungu kwa kuona namna mambo yanavyofanyika. Nitarudi kazini nikiwa na ari mpya ya kufanya kazi. Hongera TRAMPA na hongera kwa watunzaji wa kumbukumbu,” alisema.

 

Ofisi ya Rais – Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ilishiriki kikamilifu katika mkutano huo kupitia viongozi na wakurugenzi mbalimbali, akiwamo Frimin Msiangi, pamoja na Salumu Kyando, Mkurugenzi wa Waasisi wa Taifa, na Athanas Kolokota, Mkurugenzi wa Nyaraka.

 

Mkutano huo unaendelea jijini Dodoma ukiwa na lengo la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu taaluma ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, maendeleo ya taaluma hiyo pamoja na namna ya kuimarisha usimamizi wa kumbukumbu katika taasisi nchini.


Simu: 0717 649 257
Barua pepe: makwadeladius@gmail.com

 










0/Post a Comment/Comments