VIKAO VYA KIUTENDAJI, JUKWAA LA KUJENGA MAAMUZI YENYE TIJA

 



Adeladius Makwega

Ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

 

Wakati mwingine, uamuzi mkubwa huanza na wazo dogo. Swali moja linaweza kufungua mjadala, mjadala ukaibua mitazamo mbalimbali, na mitazamo hiyo ikasaidia kujenga uamuzi unaobeba maslahi ya taasisi na utekelezaji bora wa majukumu ya Serikali.

Ndani ya kikao, si kila anayezungumza huwa na jibu la mwisho, lakini kila hoja inaweza kuwa sehemu ya kulifikia jibu sahihi. Mmoja anatoa wazo, mwingine anaongeza mtazamo, mwingine anahoji, na mwingine anajibu. Hatua kwa hatua, hoja hupevuka na maamuzi hujengwa kwa pamoja.

 

Ni kwa msingi huo, Mkurugenzi wa Idara ya Waasisi wa Taifa na Maktaba ya Viongozi, kutoka Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Ndugu Salum Kyando, amesisitiza umuhimu wa watendaji kushiriki kikamilifu katika vikao vya kiutendaji kwa kutoa mawazo, kuchangia hoja na kujibu hoja.

 

Ndugu Kyando amesema hayo Septemba 7, 2026, wakati akiongoza kikao cha kiutendaji cha Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, kilichojadili utekelezaji wa majukumu mbalimbali ya Idara.

 

Amesema vikao vya kiutendaji vinapaswa kuwa majukwaa ya majadiliano ya wazi na yenye tija, ambapo kila mshiriki anapata fursa ya kutoa maoni yake, kuchangia hoja na kusikiliza mitazamo ya wengine kabla ya kufikia uamuzi.

 

“Hoja inatolewa na kujadiliwa kwa kina, huku kila mmoja akitoa mawazo yake kuhusu hoja iliyo mezani, kisha tunafanya maamuzi,” amesema Ndugu Kyando.

 

Kwa mtazamo huo, ushiriki wa watendaji katika vikao hauishii katika kutoa maoni pekee, bali ni sehemu ya mchakato wa kujenga taasisi yenye uwezo wa kufanya maamuzi yanayozingatia uzoefu, maarifa na mitazamo mbalimbali ya watendaji wake.

 

Kikao hicho kilichowakutanisha Wakuu wa Idara na Vitengo pamoja na wajumbe watatu wa Sekretarieti ya ajenda husika, kilidumu kwa takribani saa tatu, muda ambao ulitumika kujadili masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Idara.

 

Katika taasisi za umma, vikao vya aina hiyo vina nafasi muhimu katika kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano miongoni mwa watendaji, kwa kuwa vinatoa nafasi ya changamoto kubainishwa, mawazo kubadilishana na hatua za utekelezaji kuwekwa kwa pamoja.

 

Wakati Ofisi hiyo ikiendelea kutekeleza majukumu yake ya kiutendaji, pia ina jukumu kubwa la kulinda na kuhifadhi historia ya Taifa kupitia kumbukumbu na nyaraka zinazohifadhiwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.

 

Miongoni mwa majukumu ya Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, ni kufanya tathmini (appraisal) ya majalada tuli, yaani majalada yaliyofungwa, ili kubaini majalada yenye umuhimu wa kudumu kwa ajili ya kuhifadhiwa na kutambua yale yasiyo na umuhimu kwa ajili ya kuteketezwa kwa mujibu wa Sheria.

 

Aidha, Idara ina jukumu la kuhifadhi nyaraka kwa kutumia teknolojia za kisasa ili kurahisisha upatikanaji wake na wakati huo huo kulinda nakala halisi. Pia inakusanya, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu pamoja na vitu vya Waasisi wa Taifa kwa lengo la kuhifadhi na kudumisha fikra na falsafa zao kwa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo.

 

Kazi hiyo inaifanya Idara kuwa sehemu muhimu katika kulinda historia ya Taifa, kwani nyaraka na kumbukumbu zinazohifadhiwa leo ndizo zitakazosaidia vizazi vijavyo kuelewa safari ya Taifa, misingi iliyolijenga na maamuzi yaliyofanyika katika nyakati mbalimbali.

Aidha, Idara inaendelea kuhamasisha umma ili kufahamu na kutumia huduma zinazotolewa, hatua inayolenga kuhakikisha kuwa kumbukumbu za Taifa zinakuwa rasilimali inayotumiwa na wananchi, watafiti, taasisi na wadau mbalimbali kwa ajili ya maarifa na utafiti.

 

Hatimaye, umuhimu wa kikao unadhihirika si kwa idadi ya watu walioketi mezani wala muda uliotumika ndani ya chumba cha kikao, bali kwa ubora wa hoja zilizotolewa, namna zilivyojadiliwa na maamuzi yaliyofikiwa.

 

Kwa sababu taasisi imara hujengwa na watu wanaosikilizana, wanaothubutu kutoa mawazo, wanaoheshimu mitazamo tofauti na wanaoweza kubadilisha hoja kuwa maamuzi na maamuzi kuwa vitendo.

Na katika kila uamuzi unaofanywa leo, kuna nafasi ya kujenga taasisi bora zaidi kwa ajili ya kesho.

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“VIKAO VYA KIUTENDAJI, JUKWAA LA KUJENGA MAAMUZI YENYE TIJA”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257


















 

 

0/Post a Comment/Comments