Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kila siku baada ya masomo mtoto mmoja alipenda kukaa dakika chache darasani kabla ya kurudi nyumbani. Hakupenda kukimbia na wenzake alipenda kuchora kwenye daftari lake.
Siku moja alichora picha ya shule yao. Akaichora kwa makini akaweka madarasa, miti, uwanja na watoto waliokuwa wakicheza.
Alipoimaliza aliiangalia kwa muda mrefu. Aliona haikuwa kamili. Baadhi ya mistari ilikuwa imepinda na rangi hazikuwa zimekaa vizuri.
Alitaka kuichana. Lakini badala yake aliibeba na kuipeleka kwa mwalimu.
Mwalimu aliitazama na kumuuliza kwa nini alikuwa anataka kuitupa.
Mtoto akasema kuwa hakupenda kwa sababu haikuwa nzuri vya kutosha.
Mwalimu akamwambia jambo moja ambalo hakulisahau.
“Usiharibu kitu kwa sababu bado hujakifikisha pale unapotaka".
Mtoto aliirudisha picha yake nyumbani.
Siku zilizofuata aliendelea kuchora. Kila mchoro mpya ulikuwa bora kidogo kuliko uliopita.
Miezi kadhaa baadaye shule ilipotaka kupamba ukuta wa darasa mtoto huyo alipewa nafasi ya kuchora picha kubwa.
Aliposimama mbele ya ukuta alikumbuka mchoro wake wa kwanza.
Ulikuwa bado umehifadhiwa kwenye daftari lake.
Hakukuwa mzuri sana lakini ndio uliomfundisha kuendelea kujaribu.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment