Emakulata Msafiri
Mwanakwetukids
Kila Jumamosi mtoto mmoja alikuwa akisafisha chumba chake. Siku hiyo alipoinua kitanda ili kufagia aliona sanduku dogo la zamani lililokuwa limefichwa chini yake.
Alilifungua kwa udadisi. Ndani kulikuwa na vitu vidogo alivyowahi kutumia akiwa mdogo qmbazo ni picha za shule, kalamu zilizokauka, medali moja na karatasi yenye michoro yake ya zamani.
Alikaa chini na kuanza kuzipitia moja baada ya nyingine.
Kwenye picha moja alijiona akiwa mdogo sana akishika cheti chake cha kwanza. Alikumbuka jinsi alivyokuwa amefurahi siku hiyo.
Lakini kadiri alivyoendelea kutazama vitu hivyo aligundua kuwa baadhi ya vitu alivyovipenda zamani hakuwa tena akivifanya. Kuchora, kusoma vitabu na kuandika mawazo yake vilikuwa vimeachwa kwa sababu ya muda mwingi aliokuwa akitumia kwenye simu.
Akaamua kuanza tena Siku iliyofuata alichukua kitabu na kukaa mezani. Baada ya kusoma akachora picha ndogo kwenye daftari lake.
Haikuwa nzuri sana kama alivyotarajia lakini hakukata tamaa.
Alihifadhi mchoro huo ndani ya lile sanduku.
Chini yake akaandika “Usiache kitu unachokipenda kwa sababu tu umekua"
Tangu siku hiyo sanduku lile halikuwa tena mahali pa kuhifadhi vitu vya zamani. Likawa ukumbusho wa vipaji na ndoto ambazo hakutaka kuzipoteza.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903872



Post a Comment