🌴 URODA WA TAWI LA MNAZI 🌴

 


Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Je, umeshakula mboga iliyoungwa na nazi?Je, umeshajipaka mafuta yaliyotengenezwa kutokana na nazi?
Je, umeshatumia kifaa chochote kilichotengenezwa kwa mti wa mnazi?”

 

Kwa hakika, kati ya watu kumi, ni vigumu kumpata hata mmoja ambaye hajawahi kutumia kitu kinachopatikana kutokana na mti au tunda la nazi.

 

Kati ya hao, Mwanakwetu wa Mbagala ni mmoja wao.

 

Nina hakika wewe unayesoma makala haya, umejikuta ukirudi katika yale maswali matatu. Hebu tafakari kidogo, kisha jiulize: Jibu lako ni lipi?

 

Baada ya kutafakari majibu ya maswali hayo, sasa Mwanakwetu msomaji wangu, nakuomba nikuongezee jambo jingine:

 

“Mti wa mnazi unaweza kutumika kutengeneza samani za aina mbalimbali. Majani yake hutumika kuezekea nyumba, huku makumbi na vipande vya mti wake vikitumika kama kuni.”

🌴 Lakini kuna jambo moja la kipekee ambalo Mwanakwetu analikumbuka...

“Nakumbuka nilipokuwa mdogo, kuti la mnazi—ile sehemu yake nene—lilitumika kama chombo cha kuchezea. Tulilipanda na kisha tukateleza nalo kutoka mlimani hadi bondeni, kwa furaha na vicheko visivyo na mwisho.Haya ni mambo ya sisi watoto na wajukuu wa wakulima wa nazi, siye kiungo chetu cha mboga kipo angani, wewe unayeungia karanga na ufuta utaniweza? ”

 

Huo ndio ulikuwa uroda wa tawi la mnazi.

 

Si kila kitu kizuri kinahitaji fedha. Wakati mwingine, furaha hujificha katika vitu vidogo tunavyoviona kila siku, lakini vinavyobeba utoto, kumbukumbu, utamaduni na maisha yetu.

🌴 Mwanakwetu, haya nimeyakumbuka Septemba 2, 2026—Siku ya Nazi Duniani.

 

Siku hii ilianza kuadhimishwa mwaka 2009, kwa kutambua umuhimu wa zao la nazi kwa mataifa yanayolima na kuzalisha nazi kwa wingi.

 

Na kwa kuwa ndugu zetu wa Mbagala, Kilwa, Mafia na Mkuranga ni miongoni mwa watu wenye uhodari katika kilimo cha minazi na maeneo yanayojulikana kwa uzalishaji wa nazi nchini Tanzania, Mwanakwetu leo ameamua kuikumbuka na kuiadhimisha siku hii ya Nazi Duniani.

Kwa hiyo, Mwanakwetu...

🌴 UPO? KUMBUKA! 🌴

 

“URODA WA TAWI LA MNAZI.”

Nazi si tunda tu. Mnazi si mti tu.

Ni chakula, mafuta, kivuli, kuni, malighafi, ajira, utamaduni na kumbukumbu za maisha yetu.

 

Nakutakia Siku Njema ya Nazi Duniani! 🌴🥥

 


📧 makwadeladius@gmail.com


📞 0717 649 257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments