TUNALALAMIKA KWA SABABU YA WIVU

 


Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Mungu ni mwaminifu kwa neno lake. Mungu daima hutimiza sehemu yake. Mungu ni mkarimu na mwenye neema kwa wote. Wakati mwingine tunalalamika, si kwa sababu ya haki, bali kwa sababu ya wivu.”

Haya ni miongoni mwa maneno ya tafakari katika mahubiri ya Kadinali Luis Antonio Tagle, katika Dominika ya 25 ya Mwaka A wa Liturujia ya Kanisa.

Katika Injili ya Dominika hii, tunasikia mfano wa wafanyakazi walioajiriwa kwenda kufanya kazi katika shamba la mizabibu.

Yesu anaeleza kwamba kulikuwa na mwenye shamba aliyekwenda kuajiri wafanyakazi kwa nyakati tofauti za siku.

 

Kundi la kwanza lilikubaliana na mwenye shamba kuhusu mshahara wa kawaida wa siku. Kwa makundi yaliyofuata, mwenye shamba aliahidi kuwapa kile alichoona kuwa ni haki.

Jioni ilipofika, wafanyakazi wote waliitwa ili walipwe mishahara yao.

Lakini jambo likawa gumu pale kundi la kwanza lilipoona kwamba wale walioajiriwa mwishoni mwa siku nao walilipwa kiasi kilekile.

 

Wakajisikia kutotendewa haki.

 

Kwa mtazamo wao, wao ndio waliobeba mzigo wa kazi na kuvumilia joto la mchana mzima. Kwa hiyo, waliona kwamba walistahili zaidi kuliko wale waliofanya kazi kwa muda mfupi.

 

Tunaweza pia kujiuliza: Je, mwenye shamba alikuwa si mwadilifu?

 

Lakini katika tafakari hii, jibu ni tofauti.

Mwenye shamba alitimiza makubaliano yake na kundi la kwanza. Kwa wale wengine, alitoa kwa ukarimu kile alichoona kinafaa.

 

Hapa ndipo tunapokutana na namna Mungu anavyotenda na jinsi anavyoshughulika nasi.

 

Mungu ni mwaminifu kwa neno lake. Mungu hutimiza ahadi zake. Mungu ni mkarimu na mwenye neema kwa wote.

Na wakati mwingine, tunapolalamika, si kwamba tunadai haki; tunalalamika kwa sababu ya wivu.

 

Katika Dominika hii, Mwanakwetu alisali katika Kanisa la Bikira Maria Immakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma, katika Ibada ya Misa ya Pili.

 

Lakini katika Misa hii, kuna jambo moja ambalo Mwanakwetu anapenda kulishirikisha na msomaji wake: sauti za miitikio katika Misa.

 

Kwa kawaida, katika ibada ya Misa, kuna sauti mbalimbali zinazotengeneza mandhari ya ibada.

Kuna sauti ya kengele, makofi, milio ya chetezo wakati wa ubani, pamoja na miitikio ya waamini baada ya Padri au mchungaji kuanzisha sala au mwitikio.

Kwa mfano:

“Bwana awe nanyi.”

Waamini:

“Na awe nawe.”

Au:

“Bwana akae nanyi.”

Waamini huitikia kwa pamoja.

Hizi zote ni sauti zinazojenga mandhari halisi ya Kanisa katika ibada.

Na hapa ndipo Mwanakwetu anakumbuka somo moja muhimu alilowahi kufundishwa katika misingi ya utangazaji wa redio.

 

Mwalimu wangu aliyenifundisha Misingi ya Utangazaji wa Redio pale DW Akademie, mwaka 2012, aliwahi kunieleza jambo ambalo hadi leo nimelibeba kichwani.

 

Alisema:

“Mwanahabari anaporipoti au kutayarisha makala kuhusu Kanisa, lazima sauti za msingi za mazingira zisikike katika ripoti, makala au matangazo ya moja kwa moja. Hili linaipa uhai mkubwa kazi hiyo.”

 

Alisisitiza kwamba angalau sauti mbili au tatu za mazingira zisikike ili kumsaidia msikilizaji kutambua kwamba mwandishi yupo katika mazingira ya ibada ya Misa.

Kwa maneno mengine, sauti za mazingira zinamleta msikilizaji ndani ya tukio.

 

Mwalimu huyo, Mjerumani, alisisitiza pia:

“Jitahidi mashine yako ya kurekodia, au kipaza sauti chako wakati wa matangazo ya moja kwa moja, ikamate vizuri sauti hizo.”

 

Hii ni elimu ambayo, kwa Mwanakwetu, bado ina maana kubwa kwa wanafunzi wa habari wanaojifunza taaluma ya utangazaji wa redio.

 

Sasa turudi katika Misa ya Pili ya Dominika hii katika Kanisa la Bikira Maria Immakulata.

 

Kulikuwa na sauti moja iliyosikika vizuri sana na kuitikiwa na waamini kwa pamoja.

Ilikuwa wakati wa mwaliko wa kuimba ambapo Padri alisema:

 

“IMBENI!”

Na waamini wakaitikia kwa nguvu:

“Imbeni, imbeni kwa furaha,
msifuni, msifuni Ekaristi,
alimo, alimo Yesu Kristo,
Kristo alimo mzimaaaa…”

 

Hapo ndipo Mwanakwetu alipata hisia kwamba mandhari ya Kanisa ilikuwa imekamilika.

 

Waamini walishiriki.

Hakukuwa na mtu aliyebaki kimya.

Kila mmoja alijaribu kuitikia.

Sauti za waamini zilisikika kwa pamoja.

Na jambo hilo lilimvutia sana Mwanakwetu.

Kwa muda huo, nikajikuta nikikumbuka tena yale maneno ya mwalimu wangu wa DW Akademie mwaka 2012: “Sauti za mazingira zinaipa kazi ya mwanahabari uhai.”

Kweli.

Mwanakwetu alihisi kama yale mafunzo ya zamani yalikuwa yamepata mfano hai mbele yake.

 

Hata hivyo, kuna jambo moja ambalo Mwanakwetu aliligundua.

Wakati kwaya ilipoimba baadhi ya nyimbo nyingine, hata Mwanakwetu mwenyewe alijikuta hazifahamu vizuri.

Akaanza kujaribu huku na kule.

Anafuata wengine.

Anaangalia maneno.

Anajaribu kuimba.

Lakini moyoni akajiuliza:

Je, si vizuri nyimbo nyingi zinazotumika katika Misa zikawa zinajulikana na waamini wengi ili kila mmoja aweze kushiriki ibada kwa moyo wote?

Kwa sababu Misa si tamasha la kwaya.

Kwaya ipo kwa ajili ya kusaidia waamini kushiriki katika ibada kwa pamoja.

Hivyo, pale waamini wanapozifahamu nyimbo, wanapata nafasi kubwa zaidi ya kushiriki kwa moyo, kwa sauti na kwa umoja.

 

Lakini pia, tusilaumu kwaya pekee.

Na sisi waamini tuna wajibu wa kujifunza nyimbo hizo.

Katika tafakari yake ya Dominika hii, Kadinali Tagle anasema:

“Mungu ni mwaminifu kwa neno lake. Mungu daima hutimiza sehemu yake. Mungu ni mkarimu na mwenye neema kwa wote.”

Kisha anatukumbusha jambo ambalo linaweza kutufanya kila mmoja wetu ajitazame ndani:

“Wakati mwingine tunalalamika, si kwa sababu ya haki, bali kwa sababu ya wivu.”

 

Hapa ndipo Mwanakwetu anapomtumia ujumbe Kadinali Tagle.

Anamuuliza:

“Je, Kardinali Tagle, mimi ninapoona na kujiuliza kwa nini baadhi ya makanisa yetu yanapenda kutumia nyimbo mpya kila wakati, huku baadhi ya nyimbo za zamani zinazojulikana na waamini wengi zikiendelea kutoimbwa, hili Baba Kadinali linaniuzi, je, huo nao ni wivu?”

 

Au labda ni hamu ya kuona waamini wengi zaidi wakishiriki kwa pamoja?

Hapo ndipo swali linabaki kwa kila mmoja wetu.

Labda si lazima tulijibu kwa haraka.

Labda tunahitaji kwanza kujitazama.

Kwa sababu ujumbe wa Dominika hii unatukumbusha:

“Wakati mwingine tunalalamika, si kwa sababu ya haki, bali kwa sababu ya wivu.”

Mwanakwetu upo? Kumbuka hili.

Tukiona jambo halijatokea kama tulivyotarajia, kabla ya kulalamika, tujiulize:

Je, ninadai haki — au ninachochewa na wivu?

Nakutakia Dominika njema.

📧 makwadeladius@gmail.com
📱 0717 649 257

 

0/Post a Comment/Comments