Ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Dodoma.
Zawadi imekuwa ishara ya heshima, lakini kwa Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi, zawadi aliyoipokea Septemba 23, 2026, imebeba ujumbe mpana zaidi—kutambua safari yake ya miaka mingi katika kulinda na kuendeleza kada ya Kumbukumbu na Nyaraka nchini Tanzania.
Msiangi alisimama mbele ya washiriki wa Mkutano wa 14 wa Chama cha Wataalamu wa Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), jijini Dodoma, ambapo alikabidhiwa zawadi maalumu kama ishara ya kuthamini mchango na juhudi zake katika kada hiyo.
Wakati maelezo ya zawadi hiyo yakisomwa, jina la Msiangi liliambatana na maneno ya heshima, yakieleza namna mchango wake ulivyogusa kada hiyo kwa kipindi kirefu.
“Mkurugenzi Msiangi ni miongoni mwa wadau ambao mchango wao unatambuliwa na kuheshimika na TRAMPA. Mchango huu ni wa miaka mingi, ukiwa ni mchango uliotukuka,” ilielezwa.
Baada ya kupokea zawadi hiyo, Msiangi aliielekeza heshima hiyo kwa taasisi anayoiwakilisha.
Kwa sauti ya shukrani, aliwashukuru wanachama wa TRAMPA kwa kutambua mchango wake,
“Ninawashukuru wana TRAMPA kwa kutambua mchango wangu. Huku ni kutambua pia mchango wa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa. Asanteni TRAMPA,” alisema Msiangi.
Kutambuliwa huko kumekuja katika wakati ambao wataalamu wa Kumbukumbu na Nyaraka wamekusanyika Dodoma kwa ajili ya Mkutano wa 14 wa TRAMPA, mkutano ambao umefunguliwa Septemba 23, 2026, na Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Ridhiwani Jakaya Kikwete.
Kwa Msiangi, zawadi hiyo inaweza kuwa imechukua muda mfupi kukabidhiwa, lakini ujumbe wake umebeba historia ndefu—historia ya mchango, juhudi na utumishi katika eneo ambalo kazi yake mara nyingi hubaki nyuma ya pazia, lakini huhakikisha historia na kumbukumbu za taifa zinalindwa kwa ajili ya kizazi cha sasa na kijacho.
0717649257



Post a Comment