SIRI ILIYOBANWA NA PINI

 



 

Na Adeladius Makwega – Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma

 

Wakati mwingine historia haijifichi kwenye vitabu vikubwa wala kwenye makaburi ya watu mashuhuri. Wakati mwingine historia hujificha kwenye karatasi moja iliyochakaa, mwandiko wa mkono na hata pini ndogo iliyobana karatasi mbili.

 

Ndivyo ilivyokuwa tarehe 23 Septemba 2026, nilipotembelea mojawapo ya maktaba katika ghala la Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dodoma.

 

Hapo nilikutana na Bi. Neema Milinga, mkutubi, ambaye kwenye meza yake kulikuwa na mafaili matatu yaliyohusiana na nyaraka za Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Idara ya Elimu.

 

Bi. Neema aliniambia:

“Haya mafaili matatu kuna mtafiti amekuja hapa kuyasoma; anafanya utafiti wake.”

 

Kwa hisani yake, nikapata nafasi ya kuyatazama mafaili hayo.

 




Nilipoanza kuyapitia, sikujua kwamba ndani yake ningekutana na kitu ambacho kingeifanya historia ionekane kana kwamba imeacha alama yake yenyewe kwenye karatasi.

 

 

Miongoni mwa nyaraka hizo kulikuwa na barua yenye mwandiko wa mkono, kutoka Shule ya Msingi Rufita, Tabora.

Barua hiyo ilikuwa ya mwaka 1972, na maudhui yake yalihusu jambo ambalo leo linaweza kuonekana la kawaida, lakini wakati huo lilikuwa sehemu ya maandalizi ya shughuli za kitaifa.

 

Shule ilikuwa ikiomba msaada wa kufundishwa wanafunzi wake ngoma za utamaduni kwa ajili ya maandalizi ya sherehe za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

Barua hiyo ilipanga pia muda wa mafunzo. Yalitarajiwa kufanyika kuanzia 20 Novemba hadi 5 Desemba 1972, katika muda uliotajwa kuwa takribani saa 9:00 hadi saa 10:30 jioni.

Hapo ndipo nilipoanza kujiuliza:

 

Wanafunzi hao walikuwa kina nani? Walifundishwa ngoma gani? Na je, siku ya sherehe walitumbuiza mbele ya nani?

 

Maswali hayo yote yanaweza kuwa sehemu ya utafiti mwingine wa kihistoria.

 

Barua hiyo ilikuwa imeandikwa na Bi Martha Lina, Mkuu wa Shule (Headteacher) wa Rufita Primary School, Tabora. Lakini jambo lililonishangaza zaidi halikuwa jina wala maudhui ya barua  tu bali kwenye barua hiyo kulikuwa na pini iliyobana karatasi mbili.

Kwa mtazamo wa kwanza, ni kitu kidogo sana. Pengine mtu angeweza kuipita bila hata kuiona lakini fikiria kwa muda. Barua iliandikwa mwaka 1972. Leo ni mwaka 2026.

 

Hiyo ina maana kwamba karatasi hizo zimekaa salama hadi wakati huu baada ya kupita zaidi ya miaka 54, na pini hiyo bado inaonekana ikiwa sehemu ya hati hiyo.

 

Kwa kuitazama bila shaka inathibitisha kwa uhakika kwamba pini hiyo iliwekwa na Martha Lina mwenyewe mwaka 1972 na kwa uhakika tunaweza kusema kwamba pini hiyo imeendelea kuwepo pamoja na barua katika historia yake ya uhifadhi.

 

Na hapo ndipo pini hii ndogo inapogeuka kutoka kuwa kifaa cha kawaida na kuwa sehemu ya simulizi ya nyaraka.

“Pini iliyobana karatasi hii inaonekana kama kitu kisicho na maana. Lakini baada ya zaidi ya nusu karne, bado ipo pamoja na barua yenyewe—ikitoa picha ya namna hati hii ilivyowahi kushikwa, kubanwa na kuhifadhiwa.”

 



Tukio hili linatukumbusha jambo moja muhimu kuhusu nyaraka na kumbukumbu.

“Tunapofungua faili la zamani, hatupaswi kuangalia maneno pekee. Tunaweza pia kuangalia pini, paper clip, muhuri, bahasha, stempu, mikunjo ya karatasi, maandishi ya pembeni na hata alama ndogo zilizobaki kwenye hati.”

 

Haya ni maelezo ya ndugu Athanas Kolokota Mkurugenzi wa Huduma za Nyaraka za Taifa hapa Ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.

 

“Vitu hivi vinaweza kuwa sehemu ya historia ya hati yenyewe. Pini hii ndogo, kwa mfano, imetufanya tujiulize kuhusu safari ya barua hii: kutoka Rufita Primary School mwaka 1972, hadi kwenye jalada, na hatimaye kufika kwenye ghala la nyaraka ambako mtafiti anaweza kuifungua zaidi ya miaka 50 baadaye.”

 

Pia Mkutubi wetu Bi Neema Milinga alimwambia Mwanakwetu maneno haya;

“Karatasi imebeba maneno.Mwandiko umebeba kumbukumbu.Na pini imebaki kama alama ya safari yake.Huenda hiyo ndiyo nguvu ya nyaraka za zamani: wakati mwingine kitu kidogo sana ndicho kinachokufanya usimame, uangalie tena, na kuanza kuuliza maswali kuhusu historia.”

Haya yote ndiyo yaliyosababisha Mwanakwetu kuandaa makala haya kama yalivyo na kwa makala haya Mwanakwetu anatuma salama kwa Shule ya Msingi Rufita huku Mkoani Tabora.

Mwanakwetu, upo? Kumbuka:

“Siri Iliyobanwa na Pini.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments