Shabaha ya Ustadh Zayd Ibrahimu

 

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Mijadala, midahalo na mabishano baina ya Waislamu na Wakristo si jambo geni nchini Tanzania.

 

Mwanakwetu, ambaye ana umri wa miaka 52 kwa mwaka 2026, ameshuhudia hali hii tangu mwishoni mwa mwaka 1987 katika viwanja vya Mnazi Mmoja.

“Nilikuwa natoka Shule ya Msingi Mnazi Mmoja majira ya saa nane mchana, na nilipokuwa nikipita katika viwanja vya Mnazi Mmoja, jirani na Hospitali ya Mnazi Mmoja, nilikuta makundi ya Waislamu na Wakristo wakibishana. Nilisimama na kuangalia walipokuwa wakibishana.

 

Nilishangaa katika mjadala huo hata kwa dakika 15, kisha nikaondoka zangu nikiwa na rafiki yangu wa utoto, Alexzanda.

 

Kwangu, hayakuwa mabishano tu, bali nilijifunza kitu. Miongoni mwa wabishani hao alikuwepo Ndugu Apolinari Nyema, ambaye alikuwa Baba wa Ubatizo wa mdogo wangu, Modestus Makwega, pale Parokia ya Mbagala. Ndugu Nyema alikuwa katika kundi la watetezi wa Ukristo.”

 

Kwa hakika, hali ya mijadala iliongezeka na kuwa ya kasi mno kati ya mwaka 1990 na 2000, kukiwa na matukio mengi ambayo Mwanakwetu aliyashuhudia na ambayo yaliandikwa na wanahabari wengi.

 

Nikirudi nyuma zaidi, nikiwa nyumbani kwetu Mbagala, siku ya Jumapili asubuhi wakati tunakwenda kanisani kusali Dominika, vijana wa mtaani walikuwa wakiimba nyimbo mbalimbali za watoto.

Na leo hii nazitaja nyimbo mbili:

 

“Mkomangi, Makwega, Kazimbaya, Katutu, Makengele, Kavuruga upala (hatuna nywele)…”

 

Huu ulikuwa wimbo wa watoto wa mtaani wakitutania wakati tunakwenda kusali Jumapili katika Kanisa la Buruda (Kituo cha Kiroho Mbagala, Kanisa la Mtakatifu Antony wa Padua).

 

Mara zote watoto hawa waliokuwa wakiimba na kututania walikuwa Waislamu; hawakuwa watoto wa familia za Wakristo.

 

Kwa wale wanaokumbuka, watakuwa mashahidi, hasa wale ndugu zangu wa damu. Kundi la watoto hao liliimba nyimbo nyingine mbaya sana zilizokuwa na utani wenye matusi hadi katika dini, na hili lilileta shida na wakati mwingine likimtusi hata Yesu Kristo.

 

Nautaja huu wimbo kwa nia ya kutoa elimu kwa umma, ashakum si matusi:

 

“Nani kajamba kanisa, fulani huyo, na kwa nini kajamba kanisani yamporonyoka…”

Katika huu wimbo wa pili, yalikuwa yanatajwa majina yetu moja baada ya lingine, na kibaya zaidi baadhi ya watoto ambao walikuwa hawana adabu walimtaja hadi Yesu Kristo katika wimbo huu wa pili.

 

Jambo hili lilileta ugomvi mkubwa sana. Nadhani wadogo zangu kama Gerald Steve (Mkomangi Mkundi), Piensia Nyema (Katutu), Nasilika Happiness Nyema na wengineo tuliyokulia Mbagala watakuwa mashahidi wa huu wimbo na namna tulivyokuwa tunakasirika.

 

Hawa watoto waliokuwa wakiimba nyimbo hizi za dhihaka walikuwa wanafunzi wa madrasa.

 

Hali hii ilileta magomvi sana ya watoto, lakini jambo la kushangaza ni kwamba wakati wa sikukuu, iwe za Idd, nyumbani kwetu tuliletewa vyakula vya kila aina kutoka nyumba zote za majirani. Sisi Wakristo hadi tulijua ni nyumba gani akina mama wa nyumba hizo walijua kupika vizuri kuliko nyumba nyingine kupitia vyakula hivyo.

 

Na kwa ukweli wa Mungu, Mwanakwetu nakumbuka hili:

 

“Mama Faida alikuwa mpishi mzuri sana wa pilau kuliko nyumba nyingine.Pilau kutoka kwa mama Faida kila mmoja aliikimbilia. Huku wengine tukiwadanganya kuwa pilau ya mama faida ipo katia chombo kingine ili sisi tule pilau ya mama Faida.”

Wakati wa Krismasi na Pasaka, nyumbani kwetu Bibi yangu wa upande wa Baba, Edwiki Binti Omari Mkomangi, alipika pilau vizuri na kwa wingi, na sisi tuliagizwa kubeba sufuria hizo na kuzitawanya kwa majirani Waislamu kadhaa. Wengine walifika nyumbani na tukala nao sikukuu vizuri sana.

 

Huku Bibi wa Mwanakwetu alikuwa hodari sana wa kupika togwa.

 

Utani tuliyokuwa tunafanyiwa njiani tulikuwa tunaujadili njiani, katika Shule ya Jumapili na hata katika mafundisho ya Komunyo ya Kwanza na Kipaimara tukiwa wenyewe.

Kwa wale wanaokumbuka wakati huo, mafundisho ya Komunyo ya Kwanza na Kipaimara yalikuwa yanafundishwa na Makatekista wawili, Bunda na Kidiwa.

 

Makatekista hawa wakawa wanatusimulia visa vya simulizi za Yesu, hasa simulizi ya Msamaria Mwema na ile ya “Jirani yako ni yupi?” Rejea Luka 10:25–35.

Hata kama wale walitutania na kumtusi Yesu tukiwa njiani, tulitamani kupambana, lakini kwa kile tulichofundishwa kanisani, ilikuwa ngumu kupambana nao. Ilikuwa ni kupoteza muda, na kupambana nao ilikuwa ni kukiuka mafundisho ya Ukristo.

 

Wewe unacheka zako, unapishana nao, unarudi nyumbani, na hakukuwa na ugomvi hata matusi yale hayakuendelea tena.

 

Hadi sasa Mwanakwetu ni mzee wa Mbagala, huku rafiki zangu sasa ni wazee. Tukikutana nao tunaheshimiana vizuri kabisa na hakuna ugomvi na wakati mwingine tunachangia hadi pesa ya mabati ya madrasa.

 

Swali ni moja tu: Inakuwaje Mwanakwetu amekumbuka visa hivyo?

Hoja ni moja tu. Hivi karibu Ulimwengu wa Kiislamu umepata ndugu mmoja anayefahamika kama Ustadh Zayd Ibrahim. Mwanazuoni huyu wa dini ameibuka na hoja kadhaa ambazo zinabadilisha kabisa mwelekeo wa baadhi ya wanazuoni wa Kiislamu, hasa namna wanavyowatazama watu wa dini nyingine, ikiwamo Ukristo.

 

Jambo hili ni geni katika ulimwengu wa Waislamu, huku Ustadh Zayd Ibrahim akibeba lawama nyingi.

 

Kelele na shutuma hizi dhidi ya Ustadh Zayd Ibrahim ndizo zilizosababisha Mwanakwetu akumbuke simulizi hizi za utoto nyumbani kwao Mbagala na ile ya Mnazi Mmoja, katikati ya jiji la Dar es Salaam.

Hatimaye, kumbukumbu hizi za Mbagala na Mnazi Mmoja zinatukumbusha kwamba tofauti za dini si lazima ziwe chanzo cha chuki, uadui , kashfa au uhasama. Tulikua tunatofautiana katika imani, tukitaniana, wakati mwingine tukibishana, lakini ndani ya jamii hiyo hiyo tusaidiane, tushirikiane katika sikukuu na maisha mengine kama majirani. Labda ndiyo maana simulizi ya Msamaria Mwema bado ina maana kubwa kwetu: si kuuliza tu, “Jirani yangu ni nani?”, bali kujiuliza, “Mimi nimekuwa jirani wa aina gani kwa mwenzangu?” Tanzania inahitaji zaidi moyo huo wa kusikilizana, kuheshimiana na kutendeana mema, bila kujali tofauti zetu za dini, madhehebu au mitazamo, Mwanakwetu ninaamini hii ndiyo Shabaha ya Ustadh Zayd Ibrahimu.

Mwanakwetu, upo?Kumbuka :

Shabaha ya Ustadh Zayd Ibrahimu

 

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

















0/Post a Comment/Comments