SAKRAMENTI ISIYOJALI UMBALI

 

 




 

Adeladius Makwega – DODOMA

 

Tuko katika Jumapili ya 24 ya Mwaka A wa Liturujia ya Kanisa. Katika Injili ya leo, Bwana anatuhimiza kusamehe saba mara sabini.

 

Hilo ndilo jibu na pendekezo la Bwana kwa Petro. Kwa nini? Kwa sababu wanafunzi wake wanapaswa kuakisi tabia ya Mungu ya kusamehe.

 

Hebu tuangalie mfano huu wa rejea. Kulikuwa na mfalme ambaye aliamua kufanya hesabu na watumishi wake. Mmoja wao alimsihi sana bwana wake, na hatimaye deni lake likasamehewa.

Hata hivyo, mtumishi huyu hakuweza kuonyesha huruma hiyo hiyo kwa mtumishi mwenzake ambaye alikuwa na deni dogo sana kuliko lile alilokuwa anadaiwa na bwana wake. Alimkamata, akamkaba, na kumfanya afungwe gerezani.

 

Mfalme alipopata habari kuhusu jambo hilo, akamkabidhi mtumishi huyo mwovu kwa watesaji mpaka atakapolipa deni lake lote.

Ndugu zangu, Mungu anatukomboa na kutusamehe dhambi zetu ili nasi tuweze kusameheana. Kwa kufanya hivyo, nasi tunakuwa sura na vielelezo vya msamaha wa Mungu katika jumuiya zetu.

 

Upendo wa Mungu hauna kipimo. Hauishii baada ya kusamehe mara saba.

 

Haya ni mahubiri ya Kardinali Luis Antonio Tagle, Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki, taasisi inayoshughulikia Uinjilishaji wa watu ulimwenguni, yenye makao yake makuu Vatican, katika Dominika hii ya Septemba 13, 2026.

 

Naye Mwanakwetu katika Dominika hii, Kigulu na Njia, alisali katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma. Ibada ya kwanza, tukio ambalo lililorekodiwa na Mwanakwetu kanisani, ni hili:

 

“Padri aliyesalisha Misa hii, wakati wa kuwapatia waamini Komunyo Takatifu, aliwakutanisha wale waliojiandaa kumpokea Bwana wote pale mbele ya altare.

 

Baadaye akamuona mzee mmoja anakuja mwisho kabisa kupokea Komunyo. Padri alitoka kule madhabahuni na kwenda kumkomunisha mzee huyu, ambaye alikuwa na mkongojo. Nadhani ni mzee yuleyule aliyekuwa na mkongojo wake ambaye hakukomunishwa Jumapili ya 23 ya Mwaka A wa Kanisa (Yohane Mazoea).”

 

Kwa kupima umbali kutoka alipokuwepo mzee huyu, ilikuwa mbali kama robo tatu ya urefu wa kanisa. Kama kanisa lilikuwa na urefu wa mita 400, maana yake Padri huyu alimfuata mzee huyu umbali wa takribani mita 300.

 

Kwa desturi, waamini walio wazima kiafya na walio tayari kiroho kumpokea Bwana mara zote humfuata Padri pale mbele, labda wakiwa mapadri na wakomunishaji wengi, ndipo umbali unapungua.

 

Wakati Mwanakwetu anarudi nyumbani baada ya Misa hii, alikumbuka matukio makubwa mawili ya miaka mingi nyuma: moja la Kigango cha Vikindu na tukio lingine lililotokea katika Kigango cha Mtoni Mtongani, vigango vya Parokia ya Mbagala wakati huo, mwaka 1988–1989 Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam

.

“Tulifika Kigango cha Mtoni Mtongani na Padri Fidelis akasalisha Ijumaa Kuu. Wakati Misa ilipomalizika, alikuja ndugu mmoja akasema kwake Mtoni Relini ana mgonjwa aliye katika hatari ya kufa.

 

Sisi watumikiaji na Padri wetu tukaingia ndani ya gari hadi huko Mtoni Relini bondeni. Gari hii ndogo aina ya Gofu iliishia kando ya reli, tukaanza kutembea kwa miguu sisi na Padri wetu Mzungu. Yule muumini alitangulia na baiskeli kuwahi kumweka vizuri mgonjwa kwa ajili ya Mpako Mtakatifu.

 

Wakati tunafika, tukawa tunatafuta nyumba hiyo. Kumbuka, Ijumaa Kuu Padri na watumikiaji huvaa kanzu na majoho mekundu. Wakati huo Kigango cha Mtongani ndicho kinajengwa huku kikizungukwa na nyumba watu wengi na kina eneo dogo; hakuna hata pahala pa kubadilisha nguo.

Tukiwa Mtoni Relini, watu wakaanza kupiga mayowe:

 

‘Wanyonya damu hao! Hao! Hao! Wanyonya damu hao! Hao! Hao!’

 

Eneo hili lilikuwa na Wakatoliki wengi wenye asili ya Wafipa, akiwamo Mzee Maembe (baba wa mwanamuziki Vital Maembe) na Mzee Kisunga (dunguye Kisunga Steven wa RTD). Katika hali ya vurugu ya kupigwa mawe na fimbo, akaja Mzee Kisunga akasema:

 

‘Jamani, hawa jamaa siyo wanyonya damu, bali wamekuja kumpa huduma ya kiroho mgonjwa wetu. Ni waumini wetu; muumini mwenyewe ni mgeni, ametoka Sumbawanga.’

 

Hali ikawa na utulivu na baadaye tukafika kwa mgonjwa, na Padri Fidelis akatoa Sakramenti hiyo, kisha tukarudi Mbagala Msalabani.

 

Tukio la pili lilikuwa ni Kigango cha Vikindu, ambacho nacho kilikuwa chini ya Parokia ya Mbagala wakati huo.

 

Alifika muumini kwa Padri Wolfram akasema Kigango kwao Vikindu kuna mgonjwa. Kigango cha Vikindu kilikuwa na Wakatoliki wa aina nne. Kwanza, familia za Wamakonde; pili, watumishi wa Serikali, ambao wengi wao walikuwa wakufunzi wa Chuo cha Ualimu Vikindu; na aina ya nne ilikuwa wanachuo wa Chuo cha Ualimu Vikindu. Lakini pia kulikuwa na wakaazi wachache.

 

Siku hii tulikwenda nyumbani kwa mama mmoja wa Kiganda kando ya Kanisa la Kigango hicho. Nadhani hii ilikuwa mwaka 1989, na nadhani hadi leo eneo hili ndipo lilipo Parokia ya Vikindu.

 

Padri Wolfram akawasha gari akasema:

‘Antony Masele Gogali na wewe, Makwega Mpogoro wa Luhombero, twendeni Vikindu kuna mgonjwa.’

 

Padri akajitayarisha haraka haraka, akachukua Sakramenti. Huyu jamaa aliyetoa taarifa alikuwa na udugu na mama wa Kiganda. Jamaa alikuwa na gari yao ndogo; yeye akatangulia, sisi tukaingia ndani ya gari hadi Vikindu.

 

Hapo kando alikuwa anakaa bibi mmoja wa Kiganda huku akiwalea watoto wenye maambukizi ya VVU. Mama huyu alikuwa wa familia yenye uwezo na mara nyingi tulikuwa tukifika hapo kula chakula kilichoandaliwa nao siku za Dominika.

 

Nakumbuka malezi ya watoto wenye VVU lilikuwa jambo geni kwetu. Watu pale walisema mama huyu alikuwa akiwachukua watoto yatima kutoka Mkoa wa Kagera na kuwalea hapo Vikindu. Kwa wakati huo, tukawa tunastaajabu.

 

Padri akaingia ndani akatoa ile Sakramenti kwa mama mmoja mgonjwa, kisha tukarudi naye katika kibanda cha kumpumzisha. Padri akawa anaongea na mama huyu wa Kiganda na kaka yake. Mimi na Antony Masele Gopali tulikaa kibanda kingine, tukaletewa chakula tukala, na kisha kuondoka zetu kurudi Mbagala.

 

Ninachotaka kusema ni kwamba, katika suala la Sakramenti hii wakati wa dharura, ugonjwa na hatari ya kufa, Padri hawezi kusema, ‘Nipo bize.’ Anawajibika kumfuata mwenye mahitaji pahala alipo, bila kujali gharama za usafiri, umbali au changamoto nyingine zozote.

 

Kumbuka, Padri Fidelis na Mwanakwetu mwaka 1988 walitaka kuuawa kisa cha kuitwa wanyonya damu kule Mtoni Relini.Padri Fidelis akukata tamaa kuwa hudumia watu wa Mbagala aliifanya kazi hiyo, aliwasamehe watu wa Mtoni Mtongani hadi anafariki mwaka 1993 na sasa watu wa Mtoni Mtongani wana Parokia yao.

 

Mwanakwetu, upo? Kumbuka.

Sakramenti Isiyojali Umbali.”

Nakutakia Jumapili Njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments