NITAKOMUNIKA JUMAPILI IJAYO

 



Adeladius Makwega – DODOMA.

 

Ndugu zangu wapendwa katika Kristo,

Leo ni Jumapili ya 23 ya Mwaka A wa Kanisa. Injili ya leo inatufundisha jambo ambalo sote tunalihitaji katika maisha yetu: jinsi ya kushughulikia makosa, kutoelewana na migogoro inayoweza kujitokeza kati yetu.

Ukweli ni kwamba, tunapoishi pamoja, hatuwezi kukosa kutofautiana. Katika familia, kazini, katika jumuiya na hata ndani ya Kanisa, wakati mwingine tunakwazana, tunakoseana na kutendeana mambo yanayoweza kuumiza mioyo yetu.

 

Swali si kama tutakutana na migogoro au la. Swali muhimu ni: Tutaitatuaje migogoro hiyo?

Yesu anatupa njia nzuri sana.

Anasema:

“Ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonye mkiwa ninyi wawili.”

Angalia jambo hili. Yesu hasemi: “Nenda ukawaambie watu wengine.” Hasemi: “Nenda ukamsengenye.” Wala hasemi: “Mkomeshe na umlipizie kisasi.”

Badala yake, anasema:

“Nenda ukazungumze naye faraghani.”

 

Hii ni hekima kubwa sana.

Mara nyingi tunapokasirishwa na mtu, jambo la kwanza tunalofanya ni kwenda kuwaambia wengine. Tunamweleza rafiki yetu, jirani, ndugu au familia. Wakati mwingine tunafikisha jambo hilo hata kwenye mitandao ya kijamii.

Lakini Yesu anatufundisha njia tofauti:

Mtafute huyo mtu. Zungumza naye. Sikilizeni kila mmoja. Tafuteni suluhisho.

Kwa nini?

Kwa sababu lengo si kumdhalilisha mtu. Lengo ni kumpata tena ndugu yako na kujenga upya uhusiano.

Yesu anasema:

“Akikusikiliza, umempata tena ndugu yako.”

Hapa ndipo tunapoona moyo wa Kristo. Yesu hataki tushinde mabishano; anataka tushinde chuki. Hataki tuonyeshe kwamba sisi tuko sahihi pekee; anataka tuokoe uhusiano.

Ndugu zangu, wakati mwingine tunaweza kuwa sahihi katika jambo fulani, lakini namna tunavyosema ukweli inaweza kumuumiza mwingine. Tunaweza kuwa na hoja nzuri, lakini tukazitoa kwa hasira, kiburi au dharau.

 

Kwa hiyo, tunapokwenda kumkabili ndugu yetu, tujiulize:

 

Je, ninakwenda kumsaidia au kumuumiza?

 

Je, ninakwenda kutafuta suluhisho au kulipiza kisasi?

Je, ninataka kumrudisha karibu au kumfukuza mbali?

 

Na hapo ndipo tunapohitaji sala.

Yesu anasema:

“Kwa maana walipo wawili au watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo hapo katikati yao.”

Hili ni jambo la muhimu sana.

Tunapokuwa na ugomvi, tumwite Yesu.

Tunapokuwa na majeraha moyoni, tumwite Yesu.

Tunaposhindwa kusamehe, tumwite Yesu.

Tunapokaa chini kutatua tofauti zetu, tumwite Yesu.

Kwa sababu wakati Yesu yupo katikati yetu, mioyo yetu inaweza kubadilika. Hasira inaweza kuwa utulivu. Chuki inaweza kuwa msamaha. Mgawanyiko unaweza kuwa umoja.

 

Ndugu zangu, migogoro si lazima iwe mwisho wa uhusiano. Wakati mwingine inaweza kuwa mwanzo wa uhusiano mpya wenye kuelewana zaidi, kusameheana zaidi na kupendana zaidi.

 

Lakini hilo linawezekana tu ikiwa tutaacha kiburi na kumweka Kristo katikati.

 

Leo basi kila mmoja wetu ajiulize:

Je, kuna mtu ambaye bado nina kinyongo naye?

Je, kuna ndugu ambaye sijaongea naye kwa muda mrefu kwa sababu ya jambo lililotokea?

Je, kuna mtu ninayemzungumzia vibaya badala ya kwenda kuzungumza naye?

 

Labda leo Yesu anatualika kuchukua hatua moja tu:

Kwenda kuzungumza.

Si kwa hasira.

Si kwa lawama.

Si kwa kulipiza kisasi.

Bali kwa upendo.

Na kama tunakwenda kuzungumza, twende na Yesu pamoja nasi.

Kwa sababu wakati mwingine msamaha huanza na hatua ndogo sana: mtu mmoja kuamua kwenda kwa mwenzake na kusema, “Tuzungumze.”

Ndugu zangu, tuwe watu wa kujenga madaraja, si kubomoa madaraja. Tuwaonye wanaokosea, lakini kwa upendo. Tuseme ukweli, lakini kwa unyenyekevu. Tusamehe, kwa sababu nasi tunahitaji kusamehewa.

Na zaidi ya yote, tuwe tayari kuwaandama wale waliopotea njia, kama Yesu alivyokuwa tayari kuwaandama wenye dhambi.

Bwana atupe moyo wa kusamehe, moyo wa kusikiliza, moyo wa kupatana na moyo wa kupendana.

Na kila tunapokutana kutatua tofauti zetu, Yesu awe katikati yetu.

Amina.

 

Haya ni ya Kadinali Luis Antonie Tagle Kiranja wa Propaganda Fide ya Kanisa Katoliki Ulimwenguni inayosimamia Uinjilishaji wa watu duniani.

 

Katika Dominika hii ya Septemba 6, 2026, ya Mwaka A wa Liturujia ya Kanisa, Mwanakwetu alishiriki ibada katika Kanisa la Bikira Maria Imakulata, Parokia ya Chamwino Ikulu, Jimbo Kuu Katoliki la Dodoma.

 

Katika ibada hii ya Misa, jambo linalonukuliwa na Mwanakwetu lilitokea wakati wa Komunyo Takatifu.

 

Padri aliyeongoza Misa alisimama upande wa kushoto, karibu na mlango wa katikati wa kutoka katika kanisa hilo, huku makatekista wawili wakigawa Komunyo upande wa kulia na mwingine upande wa kushoto.

 

Katika upande aliokuwa Padri, muumini mmoja wa mwisho kuelekea kupokea Komunyo alikuwa mzee mwenye umri mkubwa, aliyekuwa akitumia mkongojo.

 

Padri alimuuliza maswali kadhaa, lakini kwa kadiri ilivyoonekana, mzee huyo hakufanikiwa kujibu maswali hayo. Padri akainamisha kichwa na kukitikisa huku akimtazama mzee huyo.

Hatimaye, Padri hakumruhusu mzee huyo kupokea Komunyo wakati huo.

 

Baadhi ya waamini waliokuwa wameketi nyuma kabisa katika kanisa hilo walishangazwa na tukio hilo. Wakawaeleza akina dada wawili waliokuwa wakitoka katika jumuiya iliyokuwa inasimamia Misa hii:

“Kwa nini Padri hajamkomunisha yule mzee? Viongozi wa Parokia wawe karibu na Padri wakati wa Komunyo ili waweze kumsaidia kufanya maamuzi sahihi.”

 

Muda mfupi baadaye, msomaji wa matangazo alielezwa kuhusu jambo hilo na kufika, lakini halikupatikana jibu .

 

Wakati huo, upande wa altareni, Padri alikuwa tayari ameweka Tabenakulo Ekaristi zilizobaki, huku Misa ikiendelea kuelekea ukingoni.

 

Yule mzee alisimama na baadaye akaketi pembeni kwenye benchi.

 

Baadaye, makatekista wawili walifika walikokuwa wamekaa waamini nyuma. Wakaelezwa kilichotokea. Wakamfuata yule mzee na baadaye wakarudi kwa waamini na kutoa maelezo kwamba mzee huyo huchelewa kuitikia “Amina” na kwamba Padri aliyekuwa akiongoza Misa alikuwa mgeni.

 

Wakaeleza kuwa:

 

“Huyu mzee wetu atapokea Komunyo katika Misa ya pili.”

 

Muda wa matangazo ulipofika, matangazo yalitolewa bila kulizungumzia jambo hilo.

Hata hivyo, baadaye wanaume Wakatoliki waliobaki baada ya Misa ya kwanza walifanya kikao, na suala hilo likajitokeza tena.

 

Hoja iliyojadiliwa ilikuwa kwamba wakati Padri anapogawa Komunyo, iwepo pia nafasi ya kiongozi mmoja kutoka Baraza la Walei kuwa karibu naye, ili kumsaidia pale inapohitajika kufanya maamuzi sahihi yanayohusu waamini.

Ingawa kikao cha wanaume Wakatoliki kilikuwa na ajenda nyingine, hasa kuhusu michango, hoja ya mzee ambaye hakupokea Komunyo ilipokelewa na kujadiliwa.

 

Baadaye, Mwanakwetu alipokuwa akirejea nyumbani, alimuona mbele yake mzee mmoja aliyevaa kofia, akitembea taratibu kwa msaada wa mkongojo.

Alimsalimia na alipomtazama kwa makini akagundua kuwa alikuwa yuleyule mzee ambaye hakupokea Komunyo katika Misa ya kwanza.

Mwanakwetu akamuuliza:

 

“Mzee, unaitwa nani?”

Mzee huyo akajibu:

 

“Mimi naitwa Yohane Mazoea.”

Mwanakwetu akamuuliza:

“Mzee, naomba nikuulize, kwa nini Padri hakukomunisha?”

 

Mzee Yohane akajibu:

 

“Mimi sifahamu. Lakini Katekista alikuja akaniambia nitakomunika katika Misa ya pili.”

 

Mwanakwetu akamuuliza tena:

“Sasa Mzee Yohane Mazoea, kwa nini unaondoka wakati Misa ya pili ndiyo inaanza?”

Mzee huyo akajibu:

 

“Nitakomunika Jumapili ijayo.”

 

Mwanakwetu akatania:

“Mzee Yohane, au Padri huyu ni mgeni anazaliwa katika jumuiya yako na amebaini kuwa Yohane Mazoea ana wadala(wake) wawili?”

Mzee Yohane akacheka sana.

Kisha akasema:

“Sina wake wawili. Hilo ni kosa mbele ya Kanisa. Wanini mie, Katika umri huu nitawapeleka wapi? Mwanangu, unajua hata sijakunywa chai.”

Mwanakwetu akampa Mzee Yohane Mazoea shilingi 1,000, kisha wakaagana.

Kwa kumtazama, Mzee Yohane Mazoea alionekana kuwa na umri wa kati ya miaka 80 na 90.

 

Tukio hili linatufanya turudi kwenye ujumbe wa Injili ya leo: tunapokutana na changamoto, kutokuelewana au hali inayohitaji ufafanuzi, tunahitaji kusikilizana na kutafuta suluhisho kwa upendo.

Mzee Yohane alikuwa mzee mwenye umri mkubwa na mwenye mkongojo. Pamoja na changamoto zake za uzee, bado alikuwa sehemu ya jumuiya ya waamini.Tukio hili linatukumbusha kwamba Kanisa ni familia. Na katika familia, wazee, vijana, watoto, wagonjwa na wenye changamoto mbalimbali wanahitaji nafasi ya kusikilizwa, kueleweka na kuhudumiwa kwa upendo. Ndiyo maana ujumbe wa Kristo katika Injili ya leo ni muhimu sana:

“Ndugu yako akikukosea, nenda ukamwonye mkiwa ninyi wawili.”

 

Katika kila changamoto, tusikimbilie hukumu. Tusikimbilie lawama. Tusikimbilie kuzungumza nyuma ya mtu.

Tuanze kwa kuzungumza. Tusikilize. Tuelewane. Tutafute suluhisho.

 

Kwa sababu hatujui kila jambo linalomkabili mtu mwingine.

Na zaidi ya yote, tusimsahau Kristo aliyesema yupo katikati yetu tunapokusanyika kwa jina lake.

Kanisa linapokuwa na Kristo katikati, hata tofauti ndogo zinaweza kuwa nafasi ya kujifunza, kusameheana, kuelewana na kujenga umoja.

 

Bwana atupe moyo wa kuuona uanadamu kabla ya kosa, kusikiliza kabla ya kuhukumu, na kupenda kabla ya kulaumu.

Amina.

Kumbuka:

“Nitakomunika Jumapili Ijayo.”

Nakutakia siku njema.

 

makwadeladius@gmail.com

0717649257














 

 

0/Post a Comment/Comments