NATAKA NIPOSE RUBANI HUYU! ✈️❤️

 


 

Adeladius Makwega – MBAGALA

 

“Malalamiko yake yanahusu uendeshaji wa sehemu ya oparesheni, ambapo wanaume ambao hawana umahiri wala saa nyingi za uzoefu alizonazo yeye hupewa nafasi na vyeo kwa hoja ya uanaume wao. Hili si jambo la haki.”

 

Mwanakwetu aliyasikia maneno haya vizuri kabisa.

 

Abiria wawili—dada mmoja aliyesuka rasta nzuri na mwanaume mmoja ambaye umri wake haukuwa mbali sana na wake—walikuwa wakizungumza kwa uhuru ndani ya daladala. Waliongea kana kwamba hakuna mtu mwingine aliyekuwa akiwafuatilia.

Ilikuwa Jumamosi, Septemba 5, 2026. Mwanakwetu alikuwa amepanda daladala akielekea katikati ya jiji aliloishi wakati huo kwa ajili ya kufanya manunuzi.

 

“Unajua hata kibali chake cha kusafiria wamempokonya. Ukiuliza, hawakupi majibu yoyote. Sasa mtu mahiri kama yule, kwa nini wasimpangie majukumu yanayolingana na umahiri wake? Kama hawamhitaji, kwa nini wanakaa na kibali chake? Wamuachie akatafute fursa nyingine.”

 

Mwanakwetu alikuwa ndani ya basi, usingizi ukimnyemelea. Lakini mazungumzo ya ndugu hawa wawili—ambao alihisi huenda walikuwa mume na mke—yaliuvunja usingizi wake.

 

Masikio yake yakawa makini.

Mazungumzo yale yalikuwa kama mtu anayekula ugali, maharage na nyama yenye pilipili nyingi; kila sentensi ilikuwa ikimfanya Mwanakwetu atake kusikia inayofuata.

 

Kwa namna walivyovaa, ndugu hawa walionekana kuwa watu nadhifu sana. Walikuwa wamebeba begi, na Kiswahili chao kilikuwa safi. Hata Kiingereza chao kilikuwa kizuri, chenye sarufi na mantiki.

 

Hilo lilimvutia zaidi Mwanakwetu.

 

Kwa nini?

 

Kwa sababu yeye mwenyewe ni mwalimu wa Kiingereza na Kiswahili, akiwa na Stashahada ya Ualimu kutoka Chuo cha Ualimu Kasulu, alikosoma kati ya mwaka 2001 na 2003.

Wale wawili waliendelea kuzungumza kwa uhuru mkubwa, wakidhani Mwanakwetu ni mzee wa kawaida tu “muuza madafu wa Mbagala”, asiyejua Kiingereza.

 

Walidanyanyika kwa sababu Mwanakwetu alikuwa amevaa jinsi jeans iliyopauka, shati la visanduku lililofifia na makubadhi miguuni—lakini masikio yake yalikuwa kazini!

 

“Unajua Kapteni Neema Swai hawampi safari ndefu za ndege. Walipaswa kumpa safari kubwa kwa sababu yeye ni hodari, hasa katika kurusha ndege kubwa. Lakini mambo hayaendi hivyo…”

 

Mwanakwetu akawa makini zaidi.

 

“Na hili wanalolifanya wanajua wenyewe. Ndiyo maana, kwa maoni yangu, wamezuia hata kibali chake cha kusafiria. Labda wanajua anaweza kupata fursa katika mashirika mengine ya kimataifa na kuondoka.”

 

Mwanakwetu akawa anajiuliza:

 

Huyu Kapteni Neema Swai ni nani?

 

Mzungumzaji akaendelea:

 

“Mpenzi, si unamkumbuka yule dada injini? Alipoona mambo yake yanakwama, alifungasha virago na kuondoka. Akaenda kufanya kazi kwenye kampuni ya kurusha parachuti mbugani. Aliona mambo pale ATCL ni magumu, kuna ukiritimba na mizengwe. Kama kiongozi hawezi kumpangia mtu majukumu yanayoendana na umahiri wake, basi amrudishie kibali chake cha kusafiria.”

Mwanakwetu alikuwa tayari amesahau kabisa safari yake ya kwenda kufanya manunuzi.

 

ATCL?

Kapteni Neema Swai?

 

Haya majina mawili yakaanza kuzunguka kichwani mwake.

 

Hapo ndipo Mwanakwetu alipogundua kuwa mazungumzo yale yalihusu Shirika la Ndege Tanzania—Air Tanzania Company Limited (ATCL).

 

Lakini swali moja lilibaki:

KAPITENI NEEMA SWAI NI NANI?

Abiria wale wawili waliendelea na mazungumzo yao, huku Mwanakwetu akiwa amejifanya anasikiliza muziki.

 

Ukweli ulikuwa tofauti.

 

Hakuwa anasikiliza muziki.

 

Alikuwa akisikiliza kila neno.

Mara mwanaume akamtoa uchafu uliokuwa kwenye nywele za mwanamke. Mara akamfuta lipstick iliyokuwa imekaa vibaya. Mwanamke naye akampiga kichwani kwa utani, kana kwamba ni shukrani.

 

Mwanakwetu akatabasamu kimoyomoyo.

 

Walipofika kituo kimoja, takribani vituo viwili kabla ya mwisho, wale wawili wakashuka.

Kiti cha nyuma kikabaki tupu.

Mwanakwetu akabaki mkiwa lakini alikuwa majina mawili:

ATCL na Kapteni Neema Swai.

 

Baada ya kufika mjini, Mwanakwetu alifanya manunuzi yake. Lakini akili yake haikuwa kwenye manunuzi tena.

Alitaka kujua zaidi.

Akaanza kufuatilia taarifa kuhusu ATCL na Kapteni Neema Swai.

Baadaye, katika harakati zake za kutafuta taarifa, zake alikutana na mdaua mmoja pale ATCL na kupata fursa ya kuzungumza naye.

 

Akamvuta pembeni na kusema:

“Mimi hunifahamu. Kazi yangu ni mwalimu wa sekondari. Lakini mapenzi yananisumbua sana. Nipo mbele yako kwa sababu nina shida moja—nataka kujua taarifa za kina za Kapteni Neema Swai. Nataka kumuoa!”

 

Jamaa akacheka kisha akasema;

 

“Kwa kuwa unazungumzia mambo ya ndoa, haya ni mambo ya heri,” akasema kwa mzaha. “Nitakupa taarifa kadhaa, lakini usinitaje.”

 

Mwanakwetu akacheka, akakubaliana na masharti hayo, kisha mazungumzo yakaendelea.

 

Mdau huyo akamwambia kwa mtazamo wake kuwa Neema ni mtu mwenye uwezo mkubwa anapendeza kuwa mke lakini mambo ya kazi kuna changamoto za hapa na pale.Huku maelezo haya yalioana na wale jamaa ndani ya daladala.

Katika taarifa alizokusanya, Mwanakwetu alikutana na maelezo kwamba Kapteni Neema Swai alipitia elimu katika maeneo mbalimbali ya Afrika Mashariki na baadaye akaendelea na mafunzo ya urubani nchini Afrika Kusini.

 

Taarifa zinazomhusu zinaeleza

“Alisoma Juja, Nairobi, kisha Kaboja Secondary School, Kampala, Uganda, na baadaye akaendelea na mafunzo ya urubani katika Blue Chip Flying Academy, Pretoria, Afrika Kusini.”

Pia, taarifa mbalimbali zimemtaja kama mmoja wa marubani wanawake Watanzania waliofanya vizuri katika sekta ya anga, huku akihusishwa na safari za ndege kubwa za Air Tanzania, ikiwamo Boeing 767-300F.

Hata hivyo, baadhi ya madai kuhusu mazingira yake ya kazi, vyeo, safari anazopewa au kibali chake cha kusafiria ni madai ambayo yanahitaji uthibitisho kutoka kwa wahusika na mamlaka husika kabla ya kuchukuliwa kama ukweli uliothibitishwa.

Mwanakwetu ana jambo moja la msingi:

 

ATCL ni shirika la umma.

Kwa hiyo, kama kuna malalamiko kutoka kwa watumishi/wananchi kuhusu namna majukumu, nafasi, vyeo au fursa za kikazi zinavyotolewa, basi malalamiko hayo hayapaswi kupuuzwa. Yanapaswa kufuatiliwa, kuchunguzwa na kujibiwa kwa uwazi.

Mwanakwetu anashauri Waziri mwenye dhamana ya sekta husika pamoja na uongozi wa ATCL kulichunguza kwa kina suala hili na kuhakikisha kwamba kila mfanyakazi anapewa haki yake kwa kuzingatia uwezo, taaluma, uzoefu na utendaji, bila ubaguzi wa aina yoyote.

Kwa sababu, mwisho wa siku, kinacholindwa siyo jina la mtu mmoja. Kinacholindwa ni heshima ya shirika letu la taifa.

Na pale ATCL inapolalamikiwa, Mwanakwetu anaona kama sehemu ya heshima ya taifa letu nayo inaguswa.

 

Na kuhusu “Nataka nipose rubani huyu”, Mwanakwetu anaweka wazi. Hakuwa na mpango wa kweli wa kumuoa Kapteni Neema Swai.Ilikuwa ni “gia” ya Mwanakwetu kupata mazungumzo ya kina na taarifa zaidi kuhusu rubani huyu Mtanzania.Lakini, kama ambavyo waswahili husema:

“Wambeya hawakosi maneno.”

Msije mkasema:

“Mwanakwetu sasa anahamia Upareni!” 😂

Kwa rubani Neema, kama siku moja utasoma makala hii, tambua jambo moja: Mwanakwetu hakukufuata kwa nia ya kukuvunjia heshima.

Alikutana na jina lako ndani ya daladala, akaanza kujiuliza wewe ni nani, akafuatilia, akaona safari yako ya taaluma na akasema:

“Huyu ni mwanamke anayestahili kujulikana zaidi.”

Na ndiyo maana akaandika.Si kwa sababu ya jina lako pekee.Bali kwa sababu nyuma ya jina Kapteni Neema Sway kuna simulizi ya mwanamke Mtanzania aliyeingia katika taaluma ambayo si rahisi, akapanda ndege, akafikia nafasi kubwa na kuwa sehemu ya historia ya anga la Tanzania.

Na sasa…

“NATAKA NIPOSE RUBANI HUYU!” 😂

Lakini ukweli mkubwa ni kwamba nilitaka tu kumfahamu zaidi mwanamke huyu wa anga.

Nakutakia siku njema.


📧 makwadeladius@gmail.com
📱 0717649257




















 

0/Post a Comment/Comments