MTOTO ANAPOKATAA KULA: SABABU NA NJIA ZA KUMSAIDIA


Emakulata Msafiri

Mwanakwetukids

Kumwona mtoto akikataa kula kunaweza kumtia mzazi hofu hasa ikiwa hali hiyo inajirudia mara kwa mara. Hata hivyo watoto wengi hupitia vipindi vya kuchagua au kukataa baadhi ya vyakula. Jambo muhimu ni mzazi kuelewa sababu na kutumia njia sahihi za kumsaidia mtoto.

Mara nyingi mtoto anaweza kukataa chakula kwa sababu hana njaa. Watoto wadogo wana matumbo madogo na mahitaji yao ya chakula hubadilika siku hadi siku. Kwa hiyo si lazima kila mlo ale kiasi kikubwa. Wazazi wanashauriwa kumpa mtoto chakula chenye lishe na kumruhusu aamue kiasi anachoweza kula.

Sababu nyingine inaweza kuwa mtoto hapendi aina fulani ya chakula ladha au muonekano wake. Hii haimaanishi kwamba chakula hicho hakifai. Mzazi anaweza kuendelea kumpa chakula hicho kwa nyakati tofauti bila kumlazimisha. Utafiti unaonesha kwamba mtoto anaweza kuhitaji kupewa chakula kipya mara kadhaa kabla hajakizoea.


Pia mazingira ya wakati wa kula yana umuhimu. Mtoto anayekula huku akiangalia simu au televisheni anaweza kutokuwa makini na chakula. Ni vizuri familia kutengeneza muda maalumu wa kula bila usumbufu mwingi na wazazi kuwa mfano kwa kula vyakula vyenye afya pamoja na watoto.

Hata hivyo kukataa kula kunapaswa kuchukuliwa kwa uzito ikiwa mtoto anaonesha dalili kama kupungua uzito, udhaifu, kutokua vizuri, kutapika mara kwa mara au matatizo wakati wa kumeza. Katika hali hiyo ni muhimu kumpeleka mtoto kwa mtaalamu wa afya kwa uchunguzi.


Mtoto kukataa kula si lazima iwe sababu ya hofu kila wakati. Kwa kumpa chakula chenye virutubisho, mazingira mazuri ya kula na kumruhusu ajifunze kula bila kulazimishwa, mzazi anaweza kumsaidia kujenga tabia nzuri ya ulaji. Muhimu zaidi ni kufuatilia ukuaji na afya yake kwa ujumla.


emakulatemsafiri@gmail.com

0653903873




0/Post a Comment/Comments