MTOTO ALIYEFIKIRI KUOMBA MSAMAHA NI UDHAIFU


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Kuna mtoto aliyekuwa na tabia moja iliyowasumbua sana watu waliokuwa karibu naye. Alikuwa akifanya makosa lakini hakuwahi kupenda kuomba msamaha.

Akipewa ushauri na mzazi wake mara nyingi alikaa kimya. Akiambiwa amuombe msamaha mtu aliyemkosea aligeuza uso na kuendelea na shughuli zake kana kwamba hakuna kilichotokea.

Siku moja akiwa shuleni alichukua bila ruhusa kitu cha mwanafunzi mwenzake. Alipokuwa akikitumia kilidondoka na kuvunjika.

Mwanafunzi huyo alipomuuliza kilichotokea alikaa kimya.

Mwalimu alipofahamu tukio hilo alimwita na kumuuliza kwa nini hakusema ukweli wala kuomba msamaha.

Mtoto alijibu kwa sauti ndogo

“Nikiomba msamaha watu watafikiri mimi ni dhaifu"

Mwalimu alimtazama na kumwambia

“Kuomba msamaha hakufanyi uwe dhaifu. Kunamaanisha umetambua kosa lako na una ujasiri wa kulirekebisha"


Maneno hayo yalimfanya afikirie sana.

Alimfuata mwanafunzi mwenzake na kwa mara ya kwanza akasema

“Samahani kwa kuchukua kitu chako bila ruhusa na kukivunja nilikosea"

Mwanafunzi mwenzake alimsamehe.

Kuanzia siku hiyo mtoto huyo alianza kuelewa kwamba hakuna mtu anayekamilika. Kila mtu anaweza kukosea lakini jambo muhimu ni kukubali kosa, kuomba msamaha na kujitahidi kutolirudia.

Aligundua pia kuwa kuomba msamaha hakumpunguzi thamani yake. Badala yake kulimfanya aaminike zaidi na watu waliomzunguka.


emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments