MTOTO ALIYEFICHA HUZUNI YAKE NYUMA YA TABASAMU

 

Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Kila asubuhi mtoto huyo aliamka mapema, akaoga, akavaa sare yake ya shule na kuondoka akiwa na tabasamu usoni. Watu waliomwona walidhani alikuwa mtoto mwenye furaha kuliko watoto wote.

Alipofika shuleni aliwasalimia wenzake na kushiriki katika shughuli mbalimbali kama kawaida. Hakuwahi kutaka mtu aone macho yake yakijaa machozi. Kila alipohisi huzuni alijifunza kuificha kwa kucheka.

Nyumbani hali haikuwa tofauti. Alipoulizwa kama alikuwa amechoka alijibu kwa kifupi "Niko sawa”

Lakini ukweli ulikuwa tofauti. Ndani ya moyo wake kulikuwa na mambo mengi ambayo hakujua jinsi ya kuyaeleza. Wakati mwingine alihisi upweke, wakati mwingine alikumbuka maneno yaliyokuwa yakimuumiza na wakati mwingine alitamani tu mtu amsikilize bila kumhukumu.


Usiku baada ya kila mtu kulala ndipo tabasamu lake lilipotoweka. Alikaa kitandani kimya akifikiria mambo yaliyokuwa yakimsumbua. Hakutaka kulia kwa sauti kwa sababu aliogopa kuulizwa maswali ambayo hakuwa tayari kuyajibu.

Siku moja shuleni mwalimu wake aligundua kuwa mtoto huyo alikuwa tofauti. Ingawa alikuwa akicheka na wenzake alikuwa amepoteza hamu ya kushiriki darasani.

Baada ya kipindi mwalimu alimuita pembeni na kumwambia.

“Huhitaji kuonekana mwenye furaha kila wakati kama kuna jambo linakukwaza unaweza kulisema. Kuna watu wanaoweza kukusikiliza".

Maneno hayo yalimfanya anyamaze kwa muda.

Kwa mara ya kwanza alihisi kwamba hakulazimika kuendelea kujifanya yuko sawa.

Machozi yakaanza kumtoka.

Hakusema mengi lakini kulia kwake kulikuwa kama mlango uliofunguliwa baada ya muda mrefu. Alianza kueleza yale yaliyokuwa moyoni mwake kidogo kidogo.


Baada ya hapo alianza kuelewa jambo muhimu la kuwa na huzuni hakumaanishi kuwa yeye ni mtoto dhaifu.

Alijifunza kuzungumza pale anapoumizwa, kuomba msaada anapouhitaji na kuwaambia watu anaowaamini anapokuwa na jambo linalomsumbua.

Kuanzia siku hiyo tabasamu lake lilianza kuwa la kweli zaidi.





emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872



0/Post a Comment/Comments