MAYENGO AANZA KUPIGA KASIA LA UTUMISHI WA UMMA






Adeladius Makwega

Ofisi ya Rais Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa

 

Septemba 6, 2026 ilikuwa siku ya kipekee kwa Phinias Mayengo, kijana kutoka Kijiji cha Bwai, Musoma Vijijini mkoani Mara. Baada ya kuhitimu Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) jijini Dar es Salaam, siku hiyo alianza safari mpya ya maisha yake baada ya kupata ajira yake ya kwanza katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, akifanya kazi kama Afisa Ugavi.

 

Kwa Mayengo, ajira hiyo si kazi tu, bali ni fursa ya kutumia elimu yake na kuanza kuitumikia Tanzania. “Hii ndiyo ajira yangu ya kwanza, ninamshukuru Mungu sana. Nitajituma kwa nguvu na moyo wangu wote kuwatumikia ndugu zangu Watanzania,” anasema.

Safari yake inagusa changamoto kubwa inayowakabili vijana wengi nchini ya kupata ajira baada ya kuhitimu. Kadiri idadi ya vijana inavyoongezeka, ndivyo mahitaji ya ajira yanavyoongezeka pia, hali inayofanya Serikali, sekta binafsi na wadau wengine kuhitajika kushirikiana katika kutafuta suluhisho la kudumu.

 

Ajira ya Mayengo imepatikana kupitia mchakato unaoratibiwa na Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, ambayo husimamia hatua mbalimbali kuanzia kutangazwa kwa nafasi, kupokea maombi kupitia Ajira Portal, kuchambua waombaji hadi kuendesha usaili. Waombaji wanaofaulu huendelea na taratibu za ajira katika taasisi husika.

 

Mkuu wa Kitengo cha Ugavi na Manunuzi katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Agusteno Swai, alisema Septemba 7, 2026 kuwa amempokea Mayengo na kumpangia majukumu. “Kazi yake ya kwanza, Ndugu Mayengo ameifanya Septemba 6, 2026,” alisema Swai.

 

Kutoka Bwai hadi Dodoma, simulizi ya Mayengo ni mfano wa kijana ambaye elimu yake imekutana na fursa. Ni simulizi inayotukumbusha kuwa nyuma ya kila ajira kuna ndoto ya kijana na familia inayotazamia kuona ndoto hiyo ikitimia. Hata hivyo, pamoja na ajira za Serikali, nafasi ya sekta binafsi, ujasiriamali na uwekezaji bado ni muhimu katika kuongeza fursa kwa vijana wengi zaidi wanaoingia katika soko la ajira kila mwaka.

Wizara inayosimamia ajira nchini Tanzania inaongozwa na Katibu Mkuu Juma Seleiman Mkomi na Waziri wake ni Ridhiwani Kikwete.

 

Mwanakwetu upo?Kumbuka:

“Mayengo aanza kupiga kasia la utumishi wa umma.”

Nakutakia siku njema.

makwadeladius@gmail.com

0717649257

 

 

 

0/Post a Comment/Comments