Emakulata Msafiri
Shukuru alipenda sana kusoma. Kila siku aliwahi shuleni, alifanya kazi zake za nyumbani kwa wakati na alipenda kutumia muda wake wa ziada kupitia vitabu. Walimu na wazazi wake walifurahia kuona jinsi alivyokuwa na bidii katika masomo.
Hata hivyo Shukuru alipata changamoto ya kuelewa masomo darasani kwa haraka. Mara nyingi alihitaji maelezo ya ziada kabla hajaelewa vizuri. Wenzake walipokuwa wameelewa somo yeye bado alikuwa akijitahidi kufuatilia. Hali hiyo ilimfanya apate alama za chini katika baadhi ya mitihani jambo lililomhuzunisha.
Badala ya kukata tamaa Shukuru aliendelea kujitahidi. Alisoma kila siku alifanya mazoezi ya maswali na aliomba msaada kwa walimu pale alipokuwa hakuelewa. Wazazi wake walimtia moyo kwa kumkumbusha kwamba mafanikio yanahitaji subira na juhudi za kila siku.
Kadiri siku zilivyopita Shukuru alianza kuelewa masomo vizuri zaidi. Alianza kujibu maswali darasani kwa ujasiri na matokeo yake yakaanza kuimarika. Ingawa hakuwahi kuwa wa kwanza darasani mara moja alifurahia kuona maendeleo aliyokuwa akiyafanya kila siku.
Shukuru alijifunza kuwa mafanikio hayaji kwa haraka kwa kila mtu. Alitambua kuwa bidii, uvumilivu na kutokata tamaa humsaidia mtoto kufikia malengo yake.
emakulatemsafiri@gmail.com
0653903972




Post a Comment