KUMSIKILIZA MTOTO NI SEHEMU YA MALEZI BORA


Emakulata Msafiri 

Mwanakwetukids 

Mtoto anapokua hahitaji chakula, mavazi na elimu pekee. Anahitaji pia mzazi au mlezi anayemsikiliza, anayempa nafasi ya kueleza hisia zake na anayemsaidia kuelewa changamoto anazokutana nazo.

Watoto wengi hupitia mambo mbalimbali shuleni na nyumbani lakini wakati mwingine hushindwa kuyaeleza kwa sababu wanaogopa kukosolewa au kuadhibiwa. Mtoto anapokosa mtu wa kumsikiliza anaweza kuanza kubeba matatizo yake kimya kimya.

Kumsikiliza mtoto hakumaanishi mzazi kukubaliana na kila anachosema. Maana yake ni kumpa nafasi ya kuzungumza, kumuuliza maswali kwa utulivu na kujaribu kuelewa anachopitia kabla ya kutoa hukumu.


Mzazi anaweza kutenga muda wa kuzungumza na mtoto bila kutumia simu au kufanya shughuli nyingine wakati mtoto anaeleza jambo. Pia ni muhimu kuepuka kumcheka, kumkatisha maneno au kumlinganisha na watoto wengine.

Wakati mwingine mtoto hahitaji jibu kubwa. Anahitaji tu mtu wa kumwambia “Ninakusikiliza niambie kilichotokea”

Kumsikiliza mtoto ni sehemu muhimu ya malezi bora. Mtoto anayesikilizwa hujifunza kuwa hisia na mawazo yake vina thamani. Familia inapojenga utamaduni wa mazungumzo watoto hupata mazingira salama zaidi ya kukua, kujifunza na kuzungumza kuhusu changamoto zao.


emakulatemsafiri@gmail.com 

0653903872





0/Post a Comment/Comments