KUMBUKUMBU SI KARATASI TU-MRISHO MPOTO

 


Adeladius Makwega – MBAGALA

 

Ukumbi wa Mkutano wa 14 wa Chama cha Wataalamu wa Kumbukumbu na Nyaraka Tanzania (TRAMPA), jijini Dodoma, ulikuwa umetulia wakati Firimin Msiangi akisimama mbele ya washiriki.

 

Mkurugenzi huyo wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa hakutarajia kwamba muda huo ungekuwa maalumu kwake.

Mgeni rasmi wa mkutano huo, Waziri wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, kwanza alikabidhi shilingi milioni 10 kwa Mwenyekiti wa TRAMPA, Bi. Devota Mrope, kama mchango binafsi wa kuanza ujenzi wa Ofisi ya TRAMPA.

Baada ya hapo, akaanza kutoa zawadi kwa baadhi ya wadau waliotambuliwa kwa mchango wao katika kada ya Kumbukumbu na Nyaraka. Miongoni mwao alikuwa Firimin Msiangi.

 

Nilikuwa ukumbini nikishuhudia tukio hilo. Makofi yalipotulia, likanijia swali moja: Zawadi hii ina maana gani zaidi ya kumpongeza Firimin Msiangi?

Kwangu, jibu ni kwamba ni heshima kwa mtu, lakini wakati huo huo ni heshima kwa taaluma nzima ya Kumbukumbu na Nyaraka.

 

Kwa miaka mingi, wataalamu wa kada hii wamekuwa wakifanya kazi ambayo mara nyingi haionekani mbele ya jamii. Wanatunza nyaraka na taarifa ambazo huenda leo zisionekane kuwa na umuhimu mkubwa, lakini kesho zinaweza kuwa ushahidi muhimu wa historia ya Taifa.

 

Na hapa ndipo maneno yaliyowahi kusemwa na mwanamuziki Mrisho Mpoto katika igizo fupi wakati wa ufunguzi wa mkutano huu yanapopata maana kubwa:

“Kumbukumbu si karatasi tu.”

 

Ndani ya kumbukumbu kuna historia ya Serikali, taasisi, maamuzi na matukio yaliyolijenga Taifa. Kuzihifadhi ni kuhakikisha kwamba kizazi cha sasa na kijacho kinapata nafasi ya kujua tulikotoka na kuelewa tulikofika.

 

Ndiyo maana tukio lile la ukumbini lilikuwa na ujumbe mpana zaidi ya zawadi yenyewe. Kumtambua mtaalamu mmoja kulikuwa pia kukumbusha jamii kuhusu thamani ya kada nzima inayobeba jukumu la kulinda kumbukumbu za Tanzania.

 

Nimefurahi pia kusikia Msiangi akiielekeza heshima hiyo kwa Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, akitambua kuwa kazi ya kulinda kumbukumbu si ya mtu mmoja, bali ni matokeo ya juhudi za taasisi na wataalamu wengi.

Na hapa ndipo kauli mbili nilizozisikia zinapokutana.

 

Mrisho Mpoto anatukumbusha kwamba kumbukumbu si karatasi tu; zina maana, zina historia na zina ujumbe kwa Taifa. Latifa Binti Kibadeni, Mtunzaji Kumbukumbu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, anatukumbusha upande mwingine wa jambo hilo: kwamba anayezihifadhi kumbukumbu hafanyi kazi kwa ajili ya leo pekee, bali anaziweka salama kwa ajili ya kesho na hata kwa ajili ya watu ambao bado hawajazaliwa.

 

Kwa hiyo, Mpoto anatueleza kwa nini kumbukumbu zina thamani; Latifa anatueleza kwa nini tunapaswa kuzilinda. Na kati ya hoja hizo mbili ndipo tunapopata maana pana ya kumtambua Firimin Msiangi: ni kutambua mchango wa mtu anayeshiriki kuhakikisha kwamba historia hiyo haipotei.

Kwa hiyo, ndugu Firimin Msiangi, hongera kwa kutambuliwa kwa mchango wako.

Na kwa TRAMPA, hongereni kwa kutukumbusha kwamba anayelinda kumbukumbu, analinda pia sehemu ya historia ya Taifa.

Kumbukumbu ni historia.
Kumbukumbu ni ushahidi.
Kumbukumbu ni urithi.

Hongera ndugu Firimin Msiangi.

makwadeladius@gmail.com

0717649257












 

0/Post a Comment/Comments