KAZUNGU AANZA SAFARI YA UTUMISHI WA UMMA


 






Adeladius Makwega – DODOMA

 

Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, mapema mwezi Septemba 2026 imepokea watumishi wapya 13 katika idara na vitengo mbalimbali vya taasisi hiyo ya umma nchini Tanzania.

 

Akizungumza Septemba 7, 2026, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Rasilimali Watu wa taasisi hiyo, Bi. Salama Said Mohamed, amesema watumishi hao wapo ambao wameajiriwa moja kwa moja na wengine waliohamia kutoka taasisi nyingine za umma.

 

“Katika watumishi hao 13 wapo walioajiriwa wapya na wapo watumishi waliohamia kutoka taasisi nyingine za umma. Miongoni mwao wapo maafisa kumbukumbu, maafisa uendeshaji wa ofisi, mchumi, maafisa manunuzi pamoja na maafisa habari,” amesema.

 

Akizungumzia ajira hizo mpya, Bi. Salama Said Mohamed ameipongeza Serikali kwa kutoa ajira kwa vijana hao, ambao wametoka katika mikoa mbalimbali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

 

“Matumaini yetu ni kwamba wamekuja kuongeza nguvu katika idara yetu,” amesema.

Akizungumzia mapokezi ya watumishi hao, Mkuu wa Kitengo cha TEHAMA Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Dismas Mbando, amesema watumishi wote 13 tayari wameingizwa katika mifumo mbalimbali ya TEHAMA inayotumika katika utekelezaji wa majukumu yao.

 

“Katika mapokezi haya, tayari watumishi wote 13 wameingizwa katika mifumo ya TEHAMA ya kufanya kazi, ikiwemo barua pepe za Serikali, mfumo wa saini ya kielektroniki wa nyaraka za Serikali, mfumo wa tathmini ya utendaji kazi (PEPMIS) pamoja na mfumo wa Ofisi Mtandao. Tunatarajia kuwapatia mafunzo ya namna bora ya kutumia mifumo hii,” amesema.

 

Ameongeza kuwa anaamini watumishi hao, ambao wengi wao ni vijana, wataweza kutumia mifumo hiyo kwa ufanisi kutokana na uelewa wao wa teknolojia ya kidijitali.

 

“Lakini nina imani na vijana wetu wa sasa. Wengi wanajua vizuri teknolojia hii, maana wengi ni vijana wa kidijitali na si vijana wa analojia,” amesema.

 

Akizungumza kandoni mwa hafla hiyo ya kuwapokea watumishi wapya, Prince Eric Kazungu, ambaye ameajiriwa kama mchumi, amesema ana furaha kuwa miongoni mwa watumishi wa umma.

 

Kazungu, mzaliwa wa Jiji la Arusha na mwenye Shahada ya Uchumi katika Sera na Mipango kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, amesema yuko tayari kutumia taaluma yake kulitumikia Taifa.

 

“Nina furaha kuwa miongoni mwa watumishi wa umma hapa. Nitafanya kazi kwa moyo wangu wote kuitumikia nchi yangu Tanzania,” amesema.

 

Akizungumzia mapokezi ya Kazungu, Mkuu wa Kitengo cha Mipango, Ufuatiliaji na Tathmini, Edwin Philbert Katundu, amesema amemkaribisha katika utumishi wa umma na kwamba tayari ameanza kutekeleza majukumu yake.

“Nimempokea ndugu Kazungu na nitafanya naye kazi vizuri. Ninamkaribisha katika utumishi wa umma na ameshaanza kufanya kazi kwa kishindo,” amesema.

 

Kwa mujibu wa takwimu zilizopatikana kupitia utafiti mdogo uliofanyika katika Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa inakaribia kuwa na watumishi 120 wanaofanya kazi katika kanda mbalimbali pamoja na Makao Makuu yaliyopo Dodoma.

 

Watumishi hao wapya na waliohamia kutoka taasisi nyingine za umma, ambao ni 13, ni sawa na takribani asilimia 11 ya idadi ya watumishi wote wa idara hiyo.

 

makwadeladius@gmail.com
0717649257

 

 

0/Post a Comment/Comments